Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Vilevile nimshukuru sana Mungu kwa kibali alichotupa katika Bunge hili la Bajeti, tunamwomba aendelee kutulinda na kututunza katika Bunge mpaka tumalize.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sanaMheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kusimamia na kuhimiza maendeleo ndani ya nchi yetu. Vilevile naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika ziara ya nchi yetu kwa ajili ya kuangalia juhudi na maarifa ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na wasaidizi wake, Mheshimiwa Mavunde pamoja na Mheshimiwa Ikupa kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tumeona jinsi gani Mheshimiwa Ikupa anavyokwenda kufanya kazi katika mikoa, kuangalia jitihada za walemavu. Nataka nimkumbushe tu Mheshimiwa Ikupa, ametembea katika mikoa mingi, naomba basi Katavi nako wanamsubiri aje kuongea na walemavu wa Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kutuletea Mkoa wa Katavi bilioni moja kwa ajili ya uanzishwaji wa Hospitali ya Mkoa, tunashukuru sana na vilevile mmetuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkoa pamoja na nyumba ya Mkuu wa Mkoa. Nilizungumzia bajeti ya mwaka jana, lakini utekelezaji umeshafanyika, naomba niipongeze sana Serikali kwa sababu inafanya kazi kwa vitendo. Naomba tuwashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkoa wetu sisi una uhaba mkubwa sana wa watumishi, hususan kwenye Halmashauri zetu pamoja na ndani ya ofisi za mkoa. Ndani ya mkoa wetu kuna takriban ya wafanyakazi elfu sita mia saba na kitu. Ina maana kuwa tunatakiwa tuwe na wafanyakazi elfu sita na kitu, lakini ndani ya mkoa wetu kupitia Halmashauri zote tuna wafanyakazi takriban elfu nne na upungufu wetu kama elfu mbili hivi, kwenye sekta ya afya, kilimo pamoja na elimu. Nategemea Serikali yangu sikivu, hivyo itatuongezea staffskwa sababu mkoa wetu una uhaba sana wa wafanyakazi, tunaomba wasitusahau kwa ajili ya utendaji kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya mkoa wetu sisi na sasa hivi ni sera ya viwanda, hatuna umeme wa uhakika sana, tunaomba Serikali itusaidie kutuletea umeme wa grid ya Taifa ili wananchi wa Katavi waweze kujenga viwanda kwa sababu sera yetu ni ya viwanda. Tunaombasana kwa sababu umeme wetu si wa uhakika kabisa, tunaomba grid ya Taifa iweze kutufikia katika Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Katavi, ma- DC wetu toka wateuliwe, hawajawahi kupata magari mapya na ukizingatia jiografia ya Mkoa wa Katavi ni ngumu sana, wanabahatisha tu magari, wanachukua magari ya watendaji ndio wanafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwa kuwakumbuka kuwajengea nyumba na wameshawaletea fedha kwa ajili ya nyumba za Wakuu wetu wa Wilaya, lakini vitendea kazi, ukianzia mkoani mpaka hata Mkuu wa Mkoa mwenyewe, gari hana, kwa sababu gari lake lilipata ajali, mpaka leo anatumia tu magari ya kubahatishabahatisha.

Sasa niaomba Serikali yangu iangalie sanaMkoa wa Katavi, upande wa ma DC wetu, wanafanya kazi kubwa sana ya kuhamasisha maendeleo ndani ya mkoa wetu na kusimamia maendeleo ndani ya mkoa wetu, lakini vitendeakazi hawana na Halmashauri zetu hazina magari kabisa mpaka mkoa. Naomba Serikali yangu sikivu iangalie Mkoa waKatavi kwa ajili ya vitendea kazi ili waweze kuendelea kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja sasa kwenye mambo yetu ya uchumi, naomba niishauri Serikali yangu, najua Wabunge wengi wamesema, wamezungumzia kuhusu masuala ya uvuvi, najua zamani ndani ya Wizara yetu ya Uvuvi, tulikuwa tuna Shirika lilikuwa linaitwa TAFIRI, lilikuwalinavua samaki na samaki wale walikuwa wanawasaidia sana Watanzania kwa kuwapata kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niipongeze Wizara ya Mifugo, pamoja na Uvuvi kwa kuweka Dawati la Sekta Binafsi kupitia Uvuvi, wamefanya vizuri sana. Naomba nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Mpina pamoja na Naibu wake ninajua dawati hili linafanya kazi vizuri sana na usimamizi unaendelea kuwa mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,naomba niikumbushe Serikali yangu, naomba sana, tununue meli yetu. Kazi aliyofanya Mheshimiwa Mpina na Naibu Waziri wamefanya kazi kubwa, sasa hivi samaki kwenye maziwa ni wakubwa kwelikweli. Tulienda Mwanza, wenyewe tulishuhudia jinsi gani kazi imefanyika, mpaka samaki wakubwa wapo katika maziwa yetu.

Sasa tukinunua meli kupitia bahari, meli ikafanya kazi hiyo ya kuvua kwenye maziwa, nafikiri Tanzania yetu itapata uchumi mkubwa, Taifa litafaidika na vilevile wananchi wetu watafaidika kupitia uvuvi. Ukizingatia sasa hivi wenzetu Uganda na Kenyawamefungua viwanda vingi sana kwa ajili ya kuchakata samaki, sisi ndani ya Tanzania kupitia Mkoa wetu wa Mwanza tuna viwanda vichache sana kwa ajili ya uchakataji wa samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa kazi kubwa kwa upande wa mifugo, tumejenga sana viwanda na tumeshuhudia, Longido tumeona kiwanda kikubwa cha machinjio kwa ajili ya kusindika mifugo yetu.Hata hivyo,ng’ombe wengi wanasafirishwa kupelekwa Kenya.

Naomba, kwa sababu na sisi Tanzania tunataka kusindika mifugo yetu, tupunguze tozo. Tumekuta pale tozo ni kubwa sana kwa upande wetu wa Tanzania, naiomba sana Serikali yetu sikivu ili tuweze kufaidika na usindikaji wa mifugo yetu, basi ninaomba tupunguze tozo ili wale Watanzania wa Longido waweze kuuza mazao yao ndani ya nchi yetu sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, sasa hivi naipongeza Wizara hii, inafanya kazi vizuri, sasa hivi ngozi. Sisi tumesema sera ya viwanda, ngozi nyingi zinasafirishwa nje ya nchi na sisi tunazitaka hizo ngozi zibaki Tanzania. Naomba sana ngozi hizi zibaki katika nchi yetu kwa sababu ni sera yetu ya viwanda, viatu vitengenezwe hapahapa ili uchumi wa Tanzania uweze kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ninakuja kwenye sekta ya maziwa, naomba kuipongeza Serikali, sekta ya maziwa inakuana inatuletea kipato kikubwa ndani ya nchi yetu, tumeona, sisi wenyewe tumefanya ziara, kuna viwanda vya maziwa ambavyo vinafanyakazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupita huko, tumekuta matatizo machache, kwa sababu ndani ya maeneo yetu…

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari!

MBUNGE FULANI: Tayari, unga mkono.

MHE. ANNA R. LUPEMBE:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sanana naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)