Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya uzima tena. Nianze kwa nukuu ya mstari kwenye Biblia, Mithali 10:15 inasema, “Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu, uangamivu wa masikini ni umasikini wao.” Waswahili wanasema, “mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mungu kwa kutupa Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Ni kiongozi mwenye uthubutu na vision, anayetupeleka kule kunakotakiwa. Kwa mtu wa kawaida anaweza asielewe, kwa mtu mwenye macho ya hapa (short sighted) anaweza asione tunapoenda. Miradi anayoifanya Rais Mafufuli ni miradi mikubwa (heavy) ambayo mtu mwepesi asingeweza kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo unaweza ukaanza kuhoji ndege kwamba hujaona faida ya ndege? Watanzania tu kwenda hapa Uganda unafikiria labda uende Kenya upate ndege ya kwenda Uganda au kwenda nchi nyingine. Leo Air Tanzania inaenda Uganda, Kenya na karibia nchi nyingi za Afrika inaenda sasa hivi. Kwa hiyo, ukisema huoni manufaa ya ndege ni wewe, lakini sisi Watanzania tunahitaji ndege ziendelee kununuliwa zaidi na zaidi kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo vinajengwa viwanja vya ndege kila mkoa. Sasa unajenga kiwanja kila mkoa halafu unaendaje huko kama huna ndege? Kwa hiyo, namshukuru Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Stiegler’s Gorge, umeme wa maji ndiyo umeme wa bei ya chini kuliko sources zozote zile unazojua. Leo mtu anasimama anasema tungeenda kwenye gesi, sijui kwenye vitu gani, atuchanganulie gharama za kila source. The cheapest source of electricity ni maji. Tangu nchi hii iumbwe haijawahi kuwa na umeme wa Megawatt 2,115; tunaenda kupata umeme wa Megawatt 2,115 kupitia Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hakuna atakayetuhurumia Watanzania. Hayupo wa kutuhurumia sisi, tutajikomboa kwa resources zetu tulizonazo wenyewe. Wazungu wangependa mpate umeme wa teknolojia kubwa ambayo mtaendelea ku-depend kwao. Ndiyo wanataka! Hawapendi kile kitu ambacho ni rahisi kwetu, wanataka everyday tuendelee ku-import kutoka nje. Ndicho wanachotaka sisi lini tuta-export? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Sisi Wabunge wa CCM na Wabunge wa Upinzani tumuunge mkono Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, songa mbele na Stiegler’s Gorge. Stiegler’s Gorge ilipingwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere. Leo watu wanasema miti, miti; inatusaidia nini Mura kama haituingizii faida? Sisi tunataka umeme wa uhakika. Ukienda leo kila kona unakuta umeme unakatikakatika, hatuna umeme ambao ni stable. Mheshimiwa Rais anasema tunataka umeme wa haraka na wa haraka ni wa Stiegler’s Gorge…

MHE. AHMED ALLY SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ally Salum.

T A A R I F A

MHE. AHMED ALLY SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Mheshimiwa Makamu wa Rais anapambana katika hii nchi kuhakikisha kwamba miti inapandwa kwa wingi sana. Wewe unasema miti inatusaidia kitu gani? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Chacha, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa taarifa gani hiyo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niingie kwenye suala la elimu. Naiomba Serikali yangu na nimwombe Waziri Mkuu na vile vile naomba Mawaziri ambao wapo chini ya Waziri Mkuu wanisikilize vizuri, hususan kwenye elimu. Tunahitaji kubadili Sera ya Elimu. Kwenye suala la vyuo vya ufundi, lazima tuliangalie vizuri kwa upya. Tunahitaji vyuo vya ufundi kila Wilaya kwa sababu tunaenda kwenye uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipokuwa na vyuo hivi, tutafeli. Kwa nini Mataifa mengi yanakimbilia kuwekeza China? Ni kwa sababu ya manpower ambayo ni skillful kwenye eneo hili la ufundi. Kwa hiyo, ili tuendelee na tuendelee kupata viwanda, unaweza ukasema unafungua kiwanda hapa ukakosa wataalam wenye uelewa wa eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kwenye elimu, tunahitaji kuangalia kwa upya mitaala yetu. Kwa mfano, somo la ujasiliamali ni vizuri lifundishwe kuanzia Shule ya Msingi na kuendelea ili mtoto anapomaliza Shule ya Msingi, Sekondari au Chuo asifikirie kwenda kutafuta ajira Serikalini. Leo tuna mamia wame-graduate wanafikiria kwenda kuajiriwa, hiyo hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niongelee kidogo kuhusu tourism. Kwenye tourism Wilaya ya Serengeti, pale katikati Seronera wanapanua uwanja wa ndege. Tunahitaji uwanja wa ndege uwe nje ya hifadhi. Ukiwa nje ya hifadhi, utakuwa na multiplier effect.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba iangaliwe issue ya single entry ambayo ina-affect sana cultural tourism. Leo watalii wanapoingia hifadhini hawawezi kutoka sababu akitoka anaambiwa alipe tena. Kwa hiyo, imeathiri sana cultural tourism. Wale ambao mpo maliasili na utalii, single entry siyo nzuri kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye uzalishaji. Naiomba sana Serikali, kwenye eneo la kilimo, mifugo na uvuvi kama kuna vitu tunaweza kuvitengeneza sisi wenyewe Tanzania, ni bora kuzuia importation ili kusababisha uchumi wetu kukua ili tuweze kuuza nje. Tumeona kwenye suala la korosho ambapo watu wa nje wanatuchezea. Kama tungekuwa na viwanda vyetu, tuna-process korosho, tunasafirisha, tunaenda kuuza huko, inaingiza fedha nyingi za kigeni. Kwa hiyo, nilitaka niseme hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni maji. Naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu mniunge mkono kwenye hili. Mwaka huu kwenye Finance Bill tumwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuongeze shilingi 50/= kwenye maji ili kukamilisha miradi ya maji vijijini.

Naomba Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono kwenye hili, tuungane tumwombe Mheshimiwa Waziri Mpango shilingi 50/= iingie kwenye maji. Ndiyo nakuona Mheshimiwa Mpango unatikisa kichwa lakini hii ni muhimu sana. Kama Mheshimiwa Mpango amegoma kuingiza, atuletee chanzo mbadala cha kwenda ku-finance miradi ya maji. Hiyo tu akituletea sisi tunakubali. Kama hajatuletea chanzo mbadala, tunakula sahani moja naye, shilingi 50/= iingie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema, ninamshukuru Mungu sana, tena ningelijua ningewahi siku nyingi kwenda CCM. (Kicheko/Makofi)

Kabisa! Yaani nimekuja kugundua kumbe nimechelewa sana. Aisee! CCM kuzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, si unaona sina mawazo sasa hivi, nipo vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)