Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniweka hadi leo kuwa nina afya na uzima. Kwanza, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi, inayoongozwa na jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote waliomo ndani ya Wizara hii ya Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dada yangu Jenista Mhagama na Mheshimiwa Angellah Kairuki, pamoja na Naibu Mawaziri wote kwa nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao na kuwaletea wananchi wetu maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana nilichangia kuhusu kusamehewa VAT kwa umeme tunaouziwa kutoka TANESCO kwenda ZECO Zanzibar. Napenda nichukue nafasi hii kwa heshima kubwa kwa niaba ya Wazanzibar kuipongeza kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marais wetu wawili kwa kutafakari na kufikiria hili kwa lengo la kuimarisha Muungano kwa vitendo na kuudumisha kwa kutusamehe deni la umeme la shilingi bilioni 22.9 na pia kutuondelea VAT kwenye umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaongeza ari ya pamoja kwamba Tanzania tuna dhamira ya dhati kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa sababu viwanda vingi vinategemea umeme. Kwa hiyo, kupungua kwa bei ya umeme kutaongeza chachu ya wawekezaji Zanzibar, ajira itapatikana na uchumi utakua kwa pande zote mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia na kuipongeza Wizara hii ya Uwekezaji kwa kuendelea kuandaa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji ndani ya nchi. Naomba juhudi hizo ziendelee kwa kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji wetu ili kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali na hatimaye kuongeza ajira, kukuza uchumi na kufikia hatua ya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naipongeza sana Wizara ya Kilimo lakini pia naipongeza Wizara ya Mifugo kwamba tayari wameshaanza kuanzisha viwanda vya nyama pamoja na usindikaji wa ngozi. Kama tunavyofahamu ngozi yetu ilikuwa haina soko lakini sasa ngozi yetu itapata masoko kwa kusindikwa hapa nchini na pia kuanzisha viwanda vya nyama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta vitambulisho vya wafanyabiashara au wajasiriamali wadogo ili waweze kufanya biashara zao bila ya kubughudhiwa. Pamoja na hilo napenda tuendelee kuzishauri Halmashauri zetu ambazo baadhi yao zinawabughudhi hawa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogowadogo kwa kuwatoza kodi ndogo ndogo. Mheshimiwa Rais amelikemea hilo, kwa hivyo na sisi tumuunge mkono kwa kulikemea ili wafanyabiashara na wazalishaji wetu wadogowadogo waweze kufanya biashara zao bila kubughudhiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uwekezaji tuhakikishe malighafi za ndani zinapata masoko na yataanzia kwenye viwanda vinawekezwa hapa nchini. Nashauri tuhakikishe viwanda vyetu vinavyowekezwa hapa nchini vinatumia malighafi zetu za ndani ili kuwapa wakulima wetu masoko, masoko yetu yaanzie humu ndani ya nchi kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, ili tupate masoko na bidhaa bora ambazo zitahitajika katika viwanda vitakavyoanzishwa ni lazima tuwekeze vizuri kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuendeleza utafiti ili tupate mbegu bora za mifugo na kilimo ili bidhaa zetu kwenye viwanda hivyo ziwe na tija. Tuwe na bidhaa chache tunazozalisha lakini tunapata tija kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la uvuvi, naomba Serikali iendelee na harakati za kuwekeza kwenye uvuvi wa bahari kuu. Nashauri iwekeze kwa kujenga gati za uvuvi na kununua meli uvuvi kwa ajili ya kujipanga sasa kuingia kwenye soko la kimataifa kwa uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inayochukua katika kuwaletea wananchi wetu maendeleo ikiwemo kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwa bidhaa mbalimbali za kilimo na ufugaji. Serikali imepunguza tozo na naomba iendelee kuangalia tozo mbalimbali ambazo zinakwamisha wawekezaji na wazalishaji wetu wadogo wadogo. Nashauri Serikali iendelee kukaa na wawekezaji na wazalishaji wadogowadogo ili kubadilishana mawazo na kutatua na kuzivumbua changamoto mbalimbali zinazokwamisha shughuli za maendeleo katika nchi yetu ili uwekezaji wetu uwe mzuri na wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kuipongeza Serikali kwa kuwa nchi yetu sasa iko salama, mipaka ya nchi iko salama, shughuli za maendeleo na kiuchumi zinafanyika kwa sababu nchi iko salama, kuna utawala bora, maendeleo yanapatikana, juhudi zinaonekana, wananchi wanafurahia maendeleo, reli zinajengwa, miundombinu inaimarishwa, barabara zinajengwa na ndege watu wanakosa nafasi. Sasa hivi watu wanapotaka kusafiri kwenda nje wanaambiwa ndege ya Air Tanzania imejaa wanaanza kuhangaika kutafuta ndege maeneo mengine ili waweze kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)