Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimesimama hapa kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kama ambavyo imewasilishwa kwa uzuri. Pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, pia natumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote katika Wizara Kuu inayosimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, natumia fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati, Taarifa zilizowasilishwa hapa, zimefanya uchambuzi mzuri unaoturahisishia sisi kuchangia katika hotuba hii. Ni jambo la msingi na kimsingi tumeelezwa hapo kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, utekelezaji ama taarifa yake hii aliyoitoa hapa akiomba fedha za utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika bajeti ijayo itakayoanza mwezi Julai mwaka huu umeongozwa na mambo matatu; moja ni ule Mpango Mkuu wa Miaka Mitano, lakini pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ujumla wetu hapa ni pamoja na kutoa ushuhuda wa namna ambavyo Serikali imekuwa ikitekeleza yale ambayo tumeyaahidi. Nasimama kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema kuwathibitishia Watanzania wenzangu kwamba, Serikali inatenda inayoahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza hapa, lakini moja kubwa ambalo nataka niwakumbushe Watanzania ambalo linaendelea sasa hivi katika Jimbo la Sengerema na Jimbo la Misungwi ni ule mpango wa ujenzi wa daraja kuu litakalounganisha Wilaya ya Misungwi na Wilaya ya Sengerema na hasa Jimbo la Sengerema. Tenda ilishatangazwa na imeshafunguliwa tayari na sasa wanaendelea na tathmini kumpata mkandarasi atakayefanya ujenzi. Hili ni jambo kubwa sana, linaunganisha sio Tanzania tu wala sio mikoa ya Tanzania, lakini ni pamoja na nchi za jirani zinazotoka upande wa Mashariki Kenya, lakini pia upande wa Magharibi DRC, Burundi, Rwanda na hata majirani zetu wa Uganda. Kwa hivi, jambo hili litaongeza, litasisimua uchumi, lakini pia, litapunguza bughudha na usumbufu ambao tumekuwa tukiupata abiria ama wasafiri tunaounganisha maeneo hayo ya kanda ya ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumesikia ujenzi wa meli katika Ziwa Viktoria, lakini Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Mambo haya ni makubwa ambayo yanakuja kuleta impact kubwa katika uchumi wa Taifa. Katika kutekeleza haya na kuhakikisha kwamba, Serikali inatekeleza na kutenda iliyoyaahidi ufuatiliaji wake pia, unafanywa na Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu hata Naibu Makatibu Wakuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa nikitoa shukrani za dhati kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema kwa ugeni ambao tumeupata hivi karibuni, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mheshimiwa Kandege pamoja na Mheshimiwa Engineer Nditiye kutoka Wizara ya Ujenzi walifika Sengerema kujionea utekelezaji wa haya ambayo tunayazungumza. Katibu Mkuu Wizara ya Maji pia, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na wengine wametutembelea hivi karibuni, yote haya ni kutaka kuonesha kweli Serikali inachokizungumza ndio kile ambacho kinawafikia na wananchi kutendwa kwa ajili ya maslahi na manufaa yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi haya ni mambo makubwa ambayo tusipoyazungumza, kama ambavyo wenzangu wamekuwa wakiyasema, pengine mawe yatakuja yazungumze siku moja, lakini Serikali inafanya kazi kubwa na chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu kama mtendaji mkuu tukiongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kazi inafanyika. Hii kazi inayofanyika wala haihitaji hata majadiliano kwa sababu ni mambo ya kuyaona moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaitafuta kuifikia nchi ya viwanda Tanzania tunafahamu kwamba, tuna mzigo mkubwa wa miradi viporo. Nimesikia akitajwa hapa Mheshimiwa Chumi hapa na Mheshimiwa Chumi ni mwanzilishi wa hoja ya miradi viporo hapa kwa kadiri ambavyo tumeizungumza miaka miwili iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kutoa chagizo kwa Serikali. Najua sasa hivi fedha za miradi hasa ya sekondari zimeshaanza kutoka, lakini tuna miradi mingi inayohusu elimu ya msingi, miundombinu, nyumba za Walimu wa shule za msingi, lakini sekta ya afya kwa mfano, zahanati na baadhi hata ya maeneo ya vituo vya afya na ujenzi wa nyumba za Serikali za Vijiji pamoja na baadhi ya majengo katika ngazi ya kata. Naiomba Serikali kwa kadiri ambavyo iliahidi na hasa mwaka jana, tuliahidiwa hapa na Serikali kwamba, ilikuwa inakwenda kutimiza ahadi yake ya kupeleka fedha katika miradi yote ambayo imeanzishwa miaka iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii miradi viporo natoa msisitizo tena kuiomba Serikali, speed iliyoanzanayo sasa iendelee ili tuikamilishe hii miradi ili wananchi wetu waone thamani ya nguvu ambavyo tayari wameshakwisha kuitumia kwa sababu, tunafahamu mpango wetu wananchi wanajenga maboma Serikali inakuja kumalizia. Sasa kadiri tunavyochelewa tunawavunja nguvu wananchi, lakini pia tunaanza tena moja kwa majengo ambayo yatapata kuharibika hasa wakati huu wa mvua. Kwa hivi naiomba sana Serikali iikamilishe ahadi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanasengerema tuna jambo la kuishukuru Serikali, tumepata fedha za kuanza ujenzi wa hospitali itakamilikiwa na Serikali kwa ngazi ya wilaya. Tunasema ahsante sana Wizara ya Afya, ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kulisimamia hili. Tunafahamu sasa hivi kwamba, kuna programu ya ujenzi wa hospitali 67, lakini Sengerema pia, tumepewa taarifa kwamba, milioni 500 zimetengwa na zitafika Sengerema hivi karibuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya wilaya. Sisi tunasema ahsante sana kwa sababu, hatuwezi kuifikia nchi ya viwanda kama tuna wananchi dhaifu na ambao hawapati huduma nzuri za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa inaunganika pia na huduma za afya zinavyoimarishwa ngazi ya Kitaifa. Ni jambo jema, sasa hivi tumeona fedha ambazo zinaokolewa badala ya kwenda kutibiwa watu nje kwa maana kwamba, fursa ya kwenda kutibiwa ipo, lakini kwa sasa kwa kweli, kwa sababu, na kutibiwa nje kwa mara nyingi pia zimekuwa ni bajeti za watu binafsi, tunaona kabisa kwamba, ujenzi na uimarishaji wa sekta hizi unatupa afueni sana kama Taifa kuhusu uimarishaji wa huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linanipa msisimko na kuiunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni hili suala la kusisitiza sekta binafsi, limejitokeza sana na wazungumzaji waliozungumza kabla yangu wamelizunguza kwa kina kwamba, tunahitaji kuipa sekta binafsi nguvu na heshima inayostahili. Tunajua tumekuwa katika kipindi cha mpito na ndio maana ukiangalia kwa mfano katika aya ya 143, Ukurasa wa 67 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukiangalia takwimu za ajira kwa hotuba hii tunavyozungumza, kiasi kikubwa kimetoka kwenye sekta ya umma aslimia 66 na asilimia 34 inatoka kwenye sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu inatokana na miradi mikubwa inayofanyika sasa hivi ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, lakini sasa tunakwenda pia kwenye Stiegler’s Gorge, lakini pia, tuna miradi mingi mikubwa inayofanywa na Serikali. Hili ni jambo jema sana, lakini kwa asili tunafahamu kwamba, miradi ya umma mara nyingi ina vipindi vyake, itakapokwisha sekta ambayo itakwenda kututoa na kusisimua ajira kwa Watanzania walio wengi ni sekta binafsi. Ndio maana naungana na wenzangu wote na msisitizo aliotoa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, Serikali inajielekeza sasa kwenda kusisimua ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa Taifa letu. Ni jambo la heri, ni jambo jema, ni muhimu sana kuiunga mkono Serikali katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tunaweza kuyafanya, lakini tumejiwekea utaratibu kuendesha nchi yetu kwa misingi ya kisheria, nazungumzia utungwaji bora wa sheria. Kama unavyofahamu wewe ni Mwenyekiti wetu kwenye Kamati ya Sheria Ndogo, tumekuwa tukitunga sheria bora, sheria mama, lakini sote tunafahamu miongozo inayoongoza utekelezwaji wa sheria nyingi nchini ni sheria ndogo. Nataka kuelezea msingi na umuhimu wa kuimarisha utungwaji wa sheria ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfumo tulionao sisi kama Taifa, sheria ndogo hizi zinatungwa kwanza na Serikali, halafu ndio zinakuja katika Bunge kuzifanyia kazi kupitia Kamati ya Sheria Ndogo, lakini tuna ushahidi na ilifikia wakati fulani hali ilikuwa mbaya sana tulivyoanza Bunge hili. Hata hivyo, kwa kadri ambavyo taarifa zilikuwa zinaletwa kwenye Kamati yetu ilifikia mpaka asilimia 75 ya sheria ndogo zilizokuwa zinaletwa kwenye kamati yetu zina hitilafu, zina kasoro ambazo bila jicho la Bunge hili Tukufu kupitia Kamati yake ya Sheria Ndogo unayoiongoza wewe Mheshimiwa Mtemi Chenge wananchi wengi wangeumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa rai kwa Serikali kuendelea kuboresha utungwaji wa sheria ndogo. Ndio maana na ushahidi upo, juzi tulikuwa na mshikemshike wa suala la kanuni za kikokotoo, wote tunafahamu, Taifa lilisimama… ambazo hazikuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa…
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na kwa hatua hii naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)