Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nilikuwa mbali sana nikiamini kwamba nitachangia mchana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna inavyoendesha nchi na kuwahudumia wananchi wake. Pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri na Makatibu Wakuu na wote ambao wanaomsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika kwa nchi hii ambayo wengi hawakuitarajia lakini ndani ya miaka minne tumeshuhudia mengi na nchi imepiga hatua hasa katika huduma za kijamii. Sina sababu ya kuzitaja kwa sababu kila mmoja wetu anafahamu jambo hili. Naomba niishukuru Serikali hapa karibuni imetoa fedha za kuezeka madarasa na kukamilisha madarasa yetu ya shule za sekondari lakini bado tunauhitaji wa maboma yale ya zahanati zetu pamoja na shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nizungumzie sehemu ndogo sana lakini ni kubwa kwa nchi hii hasa kwenye suala la wastaafu. Watumishi wetu wa Serikali wa kada mbalimbali; walimu, madaktari, wataalam wa ugani na kadhalika, wanaitumikia nchi hii kwa uadilifu mkubwa sana. Hakuna hata mmoja wetu hapa ambaye hajapita kwa mwalimu, daktari na manesi, hata kama hujatibiwa lakini mama yako alipita labour, hata kama hakwenda labour alihudhuria kliniki, kwa hiyo, watumishi hawa wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunasema kwamba walimu ni wito lakini hawa walimu wanaifanya kazi ya Yesu mwenyewe ya kufundisha wanadamu ili waweze kuelewa mambo yote hapa duniani. Huyu daktari na nesi tunasema hiyo kazi ni ya wito lakini hawa nao wanafanya kazi ya Mungu mwenyewe ya kurudisha uhai wa mwanadamu, kazi hizi ni nzito sana. Inapofika sasa wakati wa kustaafu, mafao yao hayaandaliwi kwa wakati. Wako watumishi wamestaafu wamemaliza zaidi ya miezi sita bila kulipwa mafao. Pia wakati huo wakiwa wanasubiri mafao hawalipwi nusu mshahara wao kwa miezi hiyo, tunawatesa sana watumishi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe na kuishauri Wizara kwa sababu taarifa za mtumishi huwa zinafika Wizarani kabla ya miezi sita kustaafu, kwa nini mtumishi huyu asiandaliwe mafao yake kwa uharaka? Tunamfanya mtumishi huyu akiwa anasubiri mafao kwenda kukopa mikopo ambapo anaingia mikopo ya riba kubwa ya asilimia 100, anapokuja kupata mafao yake yanaishia kwenye riba, hatumtendei haki mtumishi huyu. Naishauri Wizara hii iweze kuandaa mapema iwezekanavyo mafao ya watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi huyu anapotumika miaka 35 anafikisha miaka 60 ya kustaafu kimsingi amechoka anahitaji kupata mafao yake kwa uharaka zaidi. Wakati akisubiri mafao yake, wakati mwingine anapokuja kulipwa yale malimbikizo yake ya nusu mshahara hayapati kwa wakati pia. Niiombe Serikali ya Awamu ya Tano kama ambavyo Mheshimiwa Rais alipoangalia Kikokotoo na kuwahurumia watumishi maskini wa nchi hii akarudisha asilimia zote zilizokuwepo na mafao yao yaendane na muda. Tunaimani mifuko hii wanakochangia watumishi orodha ipo tayari ni uvivu tu wa Wizara kupeleka majina yao ili waweze kupata mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii watumishi tunawategemea na watumishi hawa anapokwenda kupumzika anayo mengi ya kufanya. Kama hatutamtendea haki mtumishi mstaafu hatutakuwa tumewatendea haki Watanzania. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Hukubaliani na suala la wastaafu?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni taarifa nampa Mheshimiwa Kiswaga.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Mwakajoka.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Kiswaga na ikiwezekana arekebishe kauli tu yake kuhusiana na Kikokotoo, siyo Mheshimiwa Rais aliyewaonea huruma ni Mheshimiwa Ester Bulaya ndiye aliyepiga kelele sana kama Waziri Kivuli wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo kwa sababu haina kichwa wala miguu. Nataka niseme kwamba mwenye maamuzi na jambo lolote kwenye nchi hii ni Mheshimiwa Rais, ndiye aliyefanya uamuzi. Unaweza ukapiga kelele na kelele yako isisikilizwe kama hatuna kiongozi mwenye huruma. Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni kiongozi mwenye huruma anayehurumia wananchi wake. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ambayo yanafanywa na Serikali. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kumuweka Waziri anayeshughulikia Uwekezaji kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, yako manung’uniko mengi ya wawekezaji hasa mtu anapotaka kuwekeza kiwanda, iko mifumo mbalimbali ambayo sisi Wabunge ama nchi tumeiweka mwekezaji apitie hatua hizo ili akafikie uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu angalia mifumo yote ambayo haileti tija, inamkwamisha mwekezaji ulete mapendekezo hapa tuweze kuweka utaratibu mzuri ambao utawasababisha wawekezaji wawekeze kwa urahisi zaidi la sivyo tutakuwa tunasema kwamba wawekezaji wanakwenda kuwekeza nchi nyingine. Tunayo mifano mingi hatuna sababu ya kutaja majina yao lakini watu wamekuja kutafuta uwekezaji hapa nchini lakini kwa bureaucracy za taasisi hizo wamekwenda kuwekeza nchi nyingine, Watanzania tunakosa ajira, fedha na kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tuiangalie NEMC kwani haina watumishi wa kutosha kufika kila eneo ambalo mwekezaji anaomba kuwekeza kiwanda chake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Asante sana Mheshimiwa Kiswaga.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nilistahili nipate dakika 15 nilikuwa na mengi ya kuchangia lakini basi. Ahsante sana. (Makofi)