Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa kupata nafasi nami nichangie katika hotuba hii ya Waziri Mkuu. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri baada ya kupata ajali. Nawashukuru Wabunge wote ambao walikuja hospitali na ambao walinifariji kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, namshukuru Mwenyekiti wangu kwa misukosuko aliyoipata, lakini ukiona giza linazidi ujue alfajiri inakaribia. Jambo la tatu, napenda niunge mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia katika mambo machache. Jambo la kwanza nitakalochangia ni mapato ya Serikali na sekta binafsi. Hii ni sekta muhimu sana kwa Taifa letu kwa sababu ni sekta ambayo inakusanya mapato ya Taifa. Sekta hii imekuwa ni kama adhabu kwa wananchi na sekta binafsi, kwa sababu katika sekta hii kuna milolongo mingi ya kodi. Kwa mfano, unapoanzisha biashara ama kampuni, kuna milolongo mingi ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, utatakiwa kusajili biashara yako ama kampuni, inahitaji hela; pili, utatakiwa kodi ya mapato ya TRA, ni hela; kulipa kodi la zuio, ni hela; kulipa kodi ya ujuzi, ni hela; na hali kadhalika. Hivi kwa mlolongo huu wa kodi, sekta binafsi ndiyo maana zinafunga kampuni zao na wafanyabiashara wanafunga biashara zao. Kwa nini tusiweke kodi ambazo ni chache na kodi ambayo itakuwa ni rafiki kwa wananchi na sekta binafsi kuliko kuweka mlolongo huu ambao unasababisha biashara kufungwa na sekta binafsi kukimbia katika nchi yetu? Hatuoni kwamba hii ni hasara katika nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoweka kodi ndogo ni kwamba wananchi wote watalipa kodi na Serikali itapata mapato ya kutosha, lakini tunapoweka utitiri huu wa kodi, inasababisha wale ambao tunasema wajiajiri washindwe kujiajiri; na wale ambao wataajiriwa na sekta binafsi, sekta binafsi zisiweze kuajiri kwa sababu hali ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee suala lingine la demokrasia nchini. Hali ya demokrasia nchini ni mbaya sana. Naomba tujitathmini. Serikali ya CCM ijitathmini, ni demokrasia gani ambayo inaonesha? Ni demokrasia gani ambayo wenzetu wanaotuangalia sisi tunawaonesha? Ni kwamba sasa hivi Serikali ya CCM inazuia vyama vya siasa kufanya kazi za siasa wakati Chama cha Siasa kazi yake ni kufanya siasa. Sasa unapoizuia unataka wafanye kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ina-base upande mmoja. Tunaona kwamba vyama vya Upinzani wanazuiwa kufanya mikutano, wanazuiwa kufanya kazi yao ya siasa. Tukiangalia Chama Tawala, kinafanya mikutano, kinafanya siasa, kinazunguka nchi nzima bila kubughudiwa, lakini leo vyama vya Upinzani ukitaka kufanya siasa, unaambiwa kuna intelijensia, sijui kuna namna gani, huo ni uoga. Hivyo ndivyo mnakufa kidogo kidogo kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kama hiki kikiendelea, mhakikishe 2020 hapa hamtashika dola, kwa sababu wananchi sio wajinga, wanaona yote mnayoyafanya.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Mlinga.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe Taarifa mzungumzaji kuwa kufanya siasa siyo kufanya mikutano ya hadhara tu, kufanya siasa hata anayofanya Mheshimiwa Lipumba kuwaondoa wasaliti ndani ya CUF, hiyo ni siasa tosha. (Kicheko)

MWENYEKITI: Unasemaje na Taarifa hiyo Mheshimiwa?

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siwezi kupokea taarifa hiyo, kwa sababu ninavyojua chama cha siasa, ni kufanya siasa. Leo CCM wanafanya maandamano, lakini wakifanya Chama cha Upinzani inakuwa ni zogo, Polisi, ni kwamba ninyi mnajidai kutokana na kwamba mnalindwa na dola, lakini iko siku hiyo dola itavua jukumu la kuwalinda ninyi ambao mnawateka wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkiendelea hivyo, niwahakikishie 2020 mtalala kifo cha mende. (Makofi/ Kicheko)

MBUNGE FULANI: Waambie!

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee kuchangia. Nataka nichangie katika maandalizi ya uchaguzi na Tume Huru. Tume Huru ni kilio cha siku nyingi katika nchi hii. Serikali ya CCM inajificha katika kivuli ambacho sijui nikiite kivuli gani kwa sababu hawataki kuleta Tume huru ya uchaguzi kwa sababu wanaona ikiletwa Tume huru ya uchaguzi ndiyo kifo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika Tume hii hasa muundo, Maafisa wote wa Tume ni makada wa CCM, Wakurugenzi wote ni makada wa CCM walioshindwa uchaguzi. Hivi hapa kweli pafanyike uchaguzi upinzani, hata siku moja. Huko ni kujitekenya huku mkijichekesha wenyewe. (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Tume ya Uchaguzi ni huru sana na ndiyo maana huyu Mbunge anayezungumza ni Mbunge wa Viti Maalum baada ya Tume kutangaza Wabunge wa CHADEMA wengi wakapata Viti Maalum. Pia mimi nilitangazwa na Tume hii nikiwa CHADEMA na nimetangazwa tena nikiwa CCM, maana haipendelei kabisa. Hii Tume ni huru, waendelee kuchapa kazi, wanatenda haki na hiyo ndiyo taarifa. (Makofi/ Kicheko)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa…

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo kwa sababu alitoka huku akaenda huko, wakiweko huko wanakuwa kama wamerogwa fulani wanaropokwa ropokwa tu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama CCM inajiamini, ithubutu leo hii kuleta Tume Huru ya Uchaguzi. Kama CCM inajiamini, ithubutu leo hii kuleta Katiba mpya ya wananchi inayopendekezwa. Nawapa changamoto hiyo, mkiweza, nitajua mnajiamini, lakini mnashindwa kujiamini kutokana na kwamba mkileta Tume Huru ya Uchaguzi au Katiba ya wananchi inayopendekezwa kwa dola mtasahau.

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu…

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu kanuni ya ngapi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Kanuni ya ngapi, nakuuliza?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia Kanuni ya 64(1) (a). Mheshimiwa Mbunge anayechangia hatatumia ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli. Mimi sijalogwa. Kwa hiyo, naomba athibitishe au afute hiyo kauli. Kikanuni, naomba athibitishe au afute hiyo kauli, mimi sijalogwa. Nathibitisha niko timamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba afute hiyo kauli au alithibitishie Bunge kwa mujibu wa kanuni hii.

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee kuchangia. Wakati watu wanadai Tume Huru ya Uchaguzi ziliundwa Tume zaidi ya tatu; iliundwa Tume ya Jaji Nyalali, Kamati ya Jaji Robert, baadaye ikaja Rasimu ya pili ya Katiba mpya na wananchi wote walitoa maoni yao kwamba wanataka Tume Huru ya Uchaguzi. Ni kwamba Tume iliyopo hapa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar siyo huru.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)