Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Napenda sana kwa nafasi hii nami nichangie walau maeneo machache ambayo nadhani nitayasemea vizuri kwa ajili ya faida na manufaa ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba nami sitakuwa nyuma kuungana na wenzangu wote walioipongeza na kuishukuru Serikali kwa utendaji wake mkubwa ambao kwa kweli unaonekana kwa vitendo na si kwa maneno peke yake. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu namna ambavyo amekuwa akishiriki kwa asimilia kubwa kuhakikisha majukumu yote ya Wizara anayoisimamia yanatekelezeka kwa wakati na kwa namna ambavyo yamekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda njikite kwenye mambo ambayo nimepanga kuyazungumzia sana. Moja ni juu ya viwanja vya ndege. Ni ukweli usiofichika kwamba Taifa letu sasa hivi baada ya kuwa lina uwezo wa kumiliki ndege ilizonazo leo hakuna ukweli unaopingika kwamba ni lazima sasa tujikite kwenye kuimarisha viwanja vyetu vya ndege. Tumeanza ujenzi wa viwanja hivi kwa muda mrefu, vingine vilihitaji ukarabati mdogo, vingine vilihitaji ukarabati wa kati na vingine vilihitaji ujenzi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila wakati nimekuwa nikisema juu ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Uwanja huu kwa namna ulivyoanza na unavyopangiwa bajeti kila kukicha lakini bajeti hii isipokamilika kama ambavyo imekuwa, leo tuna zaidi ya miaka ya sita tunazungumzia uwanja wa ndege ambao unasafirisha abiria wengi kabisa kwenye nchi hii. Mwaka jana nilisema hapa na hata Mheshimiwa Waziri wa Utalii atakuwa ni shahidi yangu. Ushahidi huu unatoka na ubora na umuhimu wa Uwanja wa ndege wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rekodi tulizokuwa nazo mwaka jana kama tutaendelea hivi tutamaliza miaka hii uwanja huu hautafanikiwa. Tumeshajenga jengo la mizigo, jengo la kuendeshea ndege na tumeshapanua uwanja wa ndege, kila siku nasema huku ni sawa na kuvaa suti na kutembea na kandambili hutaonekana nadhifu kwa sababu ya namna ambavyo unaonekana. Kwa hiyo, nishauri sana Serikali kwa bajeti hii ambayo tumeitenga safari hii, Mheshimiwa Waziri Mkuu Uwanja wa Ndege wa Mwanza uwe ni sehemu ya kipaumbele tukiwa tumeelekeza katika kukuza utalii, lakini tukiwa tumeelekeza katika kuendelea kulipa hadhi Shirika letu la Ndege lakini ubora wa kiwanja chenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilitaka nizungumzie juu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Tulipoamua kuikabidhi Mamlaka ya Mapato Tanzania jukumu la ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo mbalimbali kutoka Halmashauri kuna mambo ambayo yatatupelekea miaka inayokuja tupoteze kabisa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka kwenye Jiji, pale katikati Mwanza Mjini, leo ushuru wa mabango baada ya kwenda TRA, naamini tukiwaweka hapa watupe record, record watakazotupa hazitalingana na kile ambacho kilikuwa kinafanywa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaweza kupigwa mkono gari mfano gari ya Pepsi, gari yenye trela ikipigwa mkono inachukuliwa futi inapimwa urefu na upana mtu anatozwa shilingi 500,000, shilingi 600,000 au shilingi 800,000 kwa gari moja, ana gari 300 huyu mtu, unategemea makampuni ya stahili hii yatafanya nini? Yalichoamua sasa hivi ni kufuta maandishi wanabakisha rangi nyekundu, Pepsi atafuta maandishi ya Pepsi atabakisha rangi ya blue na Konyagi watafuta konyagi watabakisha rangi za njano. Matokeo yake ni nini? Mwaka ujao hatutapata hata shilingi 100 ya fedha kidogo ambayo tungeweza kuipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe warudi nyuma ambavyo Halmashauri zilikuwa zinafanya. Mfano upo, Mheshimiwa Rais alipoelekeza kukusanya kodi ya majengo kwa kiwango cha shilingi 10,000 na shilingi 50,000 kwenye nyumba zenye sakafu moja na kuendelea imeleta mafanikio makubwa sana. Kwa nini hawataki kujifunza kufanya kidogo ili upate kingi? Sasa ni sehemu ambayo inatupa tabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu suala la vitambulisho na namshukuru Mheshimiwa Rais amelisema juzi. Yuko mwendesha bodaboda ambaye tayari ameshatambuliwa na Serikali, ndiyo maana leo analipa bima Sh.76,800, leseni ya pikipiki shilingi 56,000, kodi ya Halmashauri ambayo wanagawa 50% na SUMATRA shilingi 22,000, tunapomwambia leo alipe Sh.20,000 tunamkosea na tunamkosea Mheshimiwa Rais kwa sababu siyo sawa. Ni lazima tuwaache hawa watu walipo na tuangalie namna ya kuwapunguzia mzigo na siyo kuendelea kuongeza mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza juu ya uboreshaji wa bandari. Sisi sote hapa tunafahamiana na sote hapa tunafanya biashara kwa namna moja au nyingine. Bandari ya Da es Salaam pamoja upanuzi mkubwa tunaoufanya leo hatuwezi kufanikiwa kwa sababu ya namna mbovu inavyoshughulikia ukusanyaji mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo haya tusipoyasimamia, mtu ana bonded warehouse, huyu ni mtu anauza brands ikifika wakati brands zimeisha huyu mtu anaonekana lazima alipe kodi wakati ambao sote tunafahamu namna anavyokwenda. Lazima tukubali tunapoboresha hizi bandari leo tunataka ku-archive nini? Kazi ya mtu wa TPA ni nini? Kazi ya mtu wa Mapato ni ipi? Ni lazima tukubaliane haya mambo yaende kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimependa sana nizungumze juu ya habari ya Mifuko yetu hii ya Hifadhi ya Jamii. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wakurugenzi waliopata nafasi hizi, Mkurugenzi wa PSSSF, Ndugu yangu Kashimba na Ndugu yangu Erio wa NSSF. Tunaamini baada ya migogoro mingi na wanafanya kazi kubwa sana, huu ni wakati wao sasa wa kuhakikisha ule umuhimu wa Serikali kuyaunganisha unaonekana kwa kutoa huduma bora. Kwa uwezo na sifa zao na kuwa kwenye sekta hii kwa muda mrefu sina shaka watafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mwisho, Limezungumzwa humu, na mimi naomba hili niliseme kwa masikitiko makubwa sana. Wizara hii jukumu lake na Wizara kupitia sekta hii ya Mambo ya Ndani kupitia sekta ya Uhamiaji, kuna mdau mmoja amekuwa anasemwa sana humu ndani na kila akitaka kusemwa sisi tunaguswa. Bahati nzuri Mheshimiwa kila akitaka kuongea anasema najua wako watu humu wataumia.

Mimi ni mmoja watu wanaoumia, naomba nikiri hivyo. Kwa sababu mtu huyu ni mwekezaji, haijalishi ameishi hapa miaka mingapi. Kutaka kupata leo uraia siyo jukumu la Wizara kusema apewe au asipewe. Jukumu la Wizara ni kuhakikisha haki na utaratibu na sheria zimefuatwa. Leo mtu akitaka kuomba uraia kutumia utaratibu anaambiwa amehonga pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nilitegemea sana Mheshimiwa Waziri aombe hapa kama kuna ushahidi unatumika kama huyu mtu ni mhalifu kwanini asishughulikiwe?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Ahsante sana Mheshimiwa Mabula. Mheshimiwa Mabula, muda wetu ndiyo huo.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)