Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami nafasi ya kuweza kuchangia hii hotuba ya Makadirio ya Bajeti kwa Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kabla sijaanza ili nisije nikasahau, naomba kwanza kuunga mkono hoja ya makadirio katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali kwa miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikiendelea hapa nchini. Miradi mingi kwa kweli ambayo hatukutegemea miaka ya nyuma, sasa inakwenda vizuri. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la kilimo. Tunaposema uchumi wa viwanda Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia ni kutilia kwanza mkazo kwenye suala la kilimo. Bila kilimo kwa kweli hata hayo meendeleo ya uchumi wa viwanda itakuwa ni ndoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Waheshimiwa Mawaziri katika sekta hii, lakini kilimo kina changamoto zake. Kwa mfano, ukiangalia sasa hivi kuna miradi hii ambayo iko chini ya Wizara, miradi kama ya greenhouse au vitalu nyumba. Tumefanya ziara tumeona baadhi ya hii miradi. Kwa kweli katika kilimo Wizara hii niwapongeze sana Waheshimiwa Waziri, wanafanya vizuri sana. Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri wenu, Mheshimiwa Ikupa na Mheshimiwa Mavunde, tumeona hiyo miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli miradi hii inakwenda vizuri na hasa ajira kwa vijana. Vijana wengi sana wameajiriwa katika miradi hii ya vitalu nyumba na wanafanya vizuri katika kujiingizia kipato. Tatizo linalojitokeza ni kwamba hii miradi hasa ya vitalu nyumba bado ni ghali. Mathalan, kama unataka upate kitalu nyumba cha mita 30 kwa nane unahitajika uwe na shilingi milioni 12 mpaka 15 kitalu nyumba kimoja. Sasa kwa mtu wa kawaida kuwa na uwezo huo ni vigumu. Naiomba Wizara katika eneo hili ione uwezekano wa kupunguza hi gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vingi kwa jinsi tulivyokuwa tunahoji vinatoka Kenya, vichache ndiyo vinatoka hapa Tanzania na hasa zile wavu zake kwa ajili ya kuezekea vitalu nyumba vinatoka nje kwa mujibu wa maelezo ya wataalam. Sasa naiomba Wizara, kama inawezekana, kukawepo na uwezekano wa kuweza kupata hizi malighafi hapa hapa Tanzania ili kila mmoja aweze kumudu kununua au kutengenezewa hivi vitalu nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta hiyo hiyo ya Kilimo naomba nisome eneo dogo kwenye ukurasa wa 27 kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Linasema: “upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 umeendelea kuimarika kutokana na hali nzuri ya mvua katika maeneo mengi ya nchi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashaka yangu hapa, data hizi sijui zimetoka wapi? Kwa hawa wataalam wetu, tumetembea kidogo Kamati ambayo mimi nipo ya Katiba na Sheria, maeneo mengi bado hali ya chakula siyo nzuri. Maeneo mengi ambayo tumetembea, mazao mengi yamekufa, hata hapa tu jirani Gairo mahindi mengi ukiangalia na mazao mengi yalifika maeneo yanataka kubeba, lakini sasa yanakufa na maeneo mengi. Sasa hii hali nzuri, sijui, labda kuna Mikoa ambayo mimi sijatembea inawezekana kuna hali nzuri ya mvua. Ila mimi sijaona sehemu nilizotembelea au tulizotembea nikaona kuna ongezeko au kuna mvua ambazo ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la ulinzi kwa wanawake na watoto ambapo katika kitabu hiki ni ukurasa wa 59. Kuna changamoto kubwa hapa. Juzi juzi tulikuwa Mkoa wa Mara, tuliufanya ziara ya kukagua miradi ya Makahama. Tulipomtembelea Mkuu wa Mkoa, Ndugu Malima alitupa report moja ambayo siyo nzuri kabisa kuhusiana na usalama wa wanawake na watoto. Kuna ongezeko kubwa sana la udhalilishwaji wa wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, pale Mara, tulikuta kesi ambayo kuna mtoto wa miaka kama minne alibakwa lakini siyo kubakwa tu, akaambukizwa na UKIMWI baada ya kwenda kupimwa. Mama wa mtoto yule baada ya kuona kesi haiko vizuri, akapewa shilingi milioni mbili akawa anakwenda kuomba kwamba kesi isiendelee kwa sababu mtoto wake tayari ameshaharibiwa na hakuna kitakachoweza kubadilika. Hii inaonyesha kabisa kwamba bado wananchi wengi na hasa akina mama hawajapata elimu ya kutosha kuona namna gani wanapaswa kulinda watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, udhalilishaji huo upo wa watoto lakini hatua zinachukuliwa. Sheria zetu bahati nzuri na wewe ni Mwanasheria; Sheria ya ubakaji haijakaa vizuri. Hii sheria kuna umuhimu wa kuipitia upya, kwa sababu ili idhihirike kwamba mtu alibaka, zile elements za kuhakikisha mtu atiwe hatiani kwa kubaka ni ndefu na siyo rahisi kuithibitisha. Nadhani hii haijakaa vizuri, inatakiwa ifanyiwe marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa Mahakama. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria. Tumekagua miradi mingi ya Mahakama, lakini kuna sehemu nyingi sana ambazo bado zinahitaji kuwepo na Mahakama. Sehemu nyingi Mahakama wanapanga, zile ambazo kunakuwa na mashauri mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tulikwenda Mkoa wa Arusha tukaenda mpaka kule Longido. Kuna sehemu tulifika yale maeneo ya mpakani pale, bado wanakodi kwenye sehemu za watu. Ile katika utoaji haki kunakuwa na tatizo kidogo, kwa sababu kama Hakimu au Mahakama zipo kwenye nyumba za watu, hata utaoji haki unakuwa hauko sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi hiyo ya Mahakama, kuna miradi mingi ambayo sasa inakamilika; na hili nimewahi kulizungumza. Shida inayokuja ni kwamba fedha zile za kuwalipa Wakandarasi sehemu nyingine bado hazijafika. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba Mahakama ambayo inasimamia haki pale itakapotokea kwamba pesa hazijapelekwa kwa wakati, Mahakama hiyo hiyo nayo itashitakiwa. Sasa hili jambo halijakaa sawa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hifadhi ya jamii. Mifuko yetu mingi imekuwa ikifanya vizuri, lakini kuna changamoto. Baadhi ya mifuko hii kuna kadi kwa mfano za NHIF hospitali nyingine zinakataa kupokea. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwakasaka.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)