Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza kabisa, niweze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kuipongeza kwanza hotuba ya Waziri Mkuu, imesheheni mambo mazuri. Serikali yetu imefanya kazi vizuri, labda tu kabla sijaingia kwenye kuchangia, wachangiaji wawili waliotangulia, wamesema maneno mengi lakini hakuna hata neno moja la maana kwa sababu hotuba ya Waziri Mkuu imeonyesha mafanikio ya nchi hii. Cha ajabu wao kazi yao ni kuponda kila jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukawa una macho lakini huoni, unaweza ukawa una masikio lakini husikii. Cha ajabu ni kwamba hawa watani zetu wa jadi walisema mzigo mzito mpe Mnyamwezi na Mnyamwezi ameubeba mzigo huo na amefanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameifanya. Nadhani pia wanazidi kumkufuru Mungu kwa sababu hakuna mwanadamu aliyekamilika, lazima mwanadamu awe na upungufu. Kilichotakiwa ni kueleza mafanikio ya Serikali, lakini pia kuishauri maeneo ambayo yana upungufu kidogo. Kwa hiyo, ndugu zetu hao kazi yao ni kulalamika na wanasema 2020 tutakuwa na jeshi gani la kuweza kumudu uchaguzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawahakikishieni kwamba uchaguzi wa 2020 asilimia kubwa ni CCM. Wananchi wanashuhudia Serikali ya CCM ni kazi ipi ambayo inafanywa nitazungumza kazi nzuri ambazo zimefanywa kwa kipindi cha miaka minne. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeweza kuanzisha elimu ya msingi bila malipo hadi sekondari. Hayo ni mafanikio mazuri na wananchi ni mashuhuda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu kidogo katika elimu ya bure. Tunaishauri Serikali ijaribu kuiangalia huo upungufu kwa sababu wimbi la wanafunzi kuandikishwa na kuingia mashuleni limekuwa kubwa. Pamekuwa na upungufu kidogo wa madarasa, madawati, Walimu na vyoo. Huu ndiyo ushauri tunatakiwa tuishauri Serikali ijaribu kuangalia na kuboresha maeneo kama hayo. Siyo kukaa mnalalamika kwamba Serikali haijafanya lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajaribu kuzungumzia kwenye upande wa afya. Serikali imeweza kupunguza gharama za wagonjwa kuwapeleka nje, imeweza kuboresha Hospitali zake za Rufaa, tumeweza kujenga shule, kujenga Hospitali nyingi za Wilaya na Vituo vya Afya. Leo hii tumeweza ku-save pesa nyingi za kuwapeleka wagonjwa wetu nje. Hiyo ni kazi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujaribu tu kuangalia upungufu kidogo uliopo. Mfano, katika Wilaya yangu ya Nyang’hwale, vifaa vipo lakini tumepungukiwa kama vile x-ray. Hatuna x-ray. Naiomba Serikali iweze basi kutuletea x-ray katika Kituo chetu cha Afya pale Kaluma. Huu ni upungufu lakini kazi kubwa imefanywa, dawa zipo za kutosha, majengo mazuri yapo na madaktari wapo pamoja na kwamba hawatoshelezi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijaribu kuzungumzia upande wa madini. Upande wa madini naipongeza Serikali imeweza kuweka utaratibu mzuri kuwasaidia wachimbaji kuondoa kero zao. Bado naiomba Serikali, kuna upotevu mkubwa sana ambao unapoteza mapato ya Serikali kwa kuchelewa kuwapa maeneo ya wachimbaji wetu kutoa leseni na kuweza kuwatambua. Kwa sababu wachimbaji walioko wengi sana katika Wilaya ya Nyang’hwale hawajarasimishwa na hawana leseni. Kwa hiyo, upotevu ni mkubwa na Serikali wala haiwatambui. Naiomba Serikali sasa iweze kuwatambua hao wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni ili waweze kutambulika na waweze kuikusanyia Serikali mapato mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyang’wale, Serikali imefanya kazi nzuri sana, lakini kuna upungufu kidogo. Tuna mradi wetu mkubwa wa maji ambapo mradi ule umetengewa takribani shilingi bilioni 15.5, lakini mradi huo leo una zaidi ya miaka minne haujakamilika. Wakandarasi wako kazini wanailalamikia Serikali yao kwamba inawacheleweshea malipo. Nataka nijue, ni kweli Serikali inachelewesha malipo ama Makandarasi ni matapeli? Naomba nipate majibu wakati Waziri atakapokuja kufanya majumuisho hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mapambano dhidi ya Ukimwi, nilikuwa nataka nitoe ushauri. Serikali inatoa fedha nyingi sana kupambana na suala hili la Ukimwi. Suala hili tujaribu kuliangalia. Nataka nitoe ushauri, nitakuja kuchangia zaidi kule mbele. Kuna masuala ambayo yanasababisha kuongezeka. Pamoja na kwamba tunapambana, lakini bado kuna maeneo ambayo yanatakiwa yafanyiwe kazi. Mfano, kuna magulio maeneo mbalimbali hapa nchini. Magulio haya yanaanza saa 10.00 jioni na yanakwenda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wetu ndiyo huo.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.