Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nianze kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuisimamia Serikali ndani ya Bunge lakini pia na nje ya Bunge kwa kazi mbalimbali anazofanya mikoa mbalimbali. Niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri katika Wizara hii, Mheshimiwa Jenista na Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazofanya lakini pia kwa hotuba ambayo imewasilishwa ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta yetu ya nishati ni nyeti na ndiyo maana kwenye mjadala wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wengi wamepata fursa ya kutoa uchauri, kuelezea wasiwasi wao na wengine pia wamepongeza. Kwa hiyo, kama Wizara tunashukuru kwa pongezi zote na tumepokea changamoto mbalimbali ambazo zimewasilishwa na tunaahidi tutaendelea kuzitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta yetu ya nishati ina mambo mengi; inasimamia suala zima la uzalishaji umeme, usafirishaji na usambazaji. Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia wamejielekeza pia kwenye jambo kubwa la muhimu la usambazaji wa umeme, hususani wamejielekeza kwenye mradi wa REA unaoendelea na wameonyesha changamoto ambazo zipo na wasiwasi pengine huu mradi unaweza usikamilike ndani ya wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwataarifu Waheshimiwa Wabunge, kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano, kupitia Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini, inatekeleza miradi mbalimbali ya umeme vijijini. Pamoja na changamoto ambazo zimejitokeza, nataka niwape matumaini kwa kweli huu mradi unaendelea. Tangu tarehe 1 Julai, 2016 mpaka tarehe 30 Machi, 2019 takribani Vijiji 1,969 vimeshapelekewa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichanganya na vijiji ambavyo vilikuwa vimepelekewa miundombinu ya umeme mpaka tarehe 30 Juni, 2016 kama 4,396, tunapozungumza sasa tuna vijiji takribani 6,365 vyenye umeme kati ya vijiji 12,268 na hii ni asilimia 52 ya vijiji vyote kwa mujibu wa takwimu ambayo tumepata kupitia TAMISEMI. Nini maana yake? Maana yake ni kwamba pamoja na changamoto zinazoendelea lakini kazi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge tunavyoupima Mradi wa REA Awamu ya Tatu, ni kweli mikataba ilianza 2017, sote tulishiriki hapa lakini tarehe kabisa ya kuanza kazi tunaipima pale wakandarasi walipofunguliwa Letter of Credit ambayo ni Julai, 2018. Kwetu sisi mradi una miezi 24 na utakamilika tarehe 30 Juni, 2020. Itakapofika tarehe 30 Juni, 2020 jumla ya vijiji 9,055 vitakuwa vyote vimepatiwa umeme na vitakavyosalia ni vijiji 3,213 ambavyo mpango wake na taratibu zake zimeanza katika Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikijibu maswali mengi na nashukuru pamoja na Waziri wangu mmekuwa mkitupa changamoto mbalimbali lakini kwetu sisi Wizara namna ambavyo tumeweka usimamizi ngazi ya Wizara, Kanda TANESCO na ndani ya REA na hivi karibuni tunaishukuru Seikali ilitupatia fedha tukaipa magari mikoa yote zaidi ya 26 kwa ajili ya usimamizi wa mradi huu na usimamizi ngazi ya wilaya na ma-technician.
Naomba niwatoe hofu hivi karibu tumetoa maelekezo kila wiki kuwasha vijiji vitatu na kila wakati tunapata taarifa. Tumetoa maelekezo ya kuwa kila wilaya kuwa na magenge zaidi ya matano. Kwa hiyo, naomba mtuamini kwamba sisi tunachopambana ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba vijiji vyote nchi nzima ifikapo 2021 vipatiwe umeme. Kwa hiyo, mtuamini kwamba uwezo tunao, nia tunayo na nguvu tunayo ya kulisimamia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoendelea pia tutaliomba Bunge lako Tukufu litaidhinisha mradi, tunaanza densification Awamu ya Pili. Pamoja na kwamba hivi nilivyovitaja ni vijiji lakini ni wazi kwamba miradi kama hii mikubwa kwa Serikali inayofanya miradi mikubwa mingi; ujenzi wa Bwawa la Stiegler’s na ujenzi wa miundombinu mbalimbali lazima kuwe na wigo. Kwa hiyo, baada ya kuona hivyo Serikali imetafakari tunakuja na mradi mwingine wa Ujazilizi Awamu wa Pili ambao utagusa vitongoji. Kwa hiyo, ikifika kwenye kijiji kama umefika kwenye vitongoji vitatu au vinne vimesalia vitongoji ujazilizi unakuja na zaidi ya shilingi bilioni 290 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo pamoja na miradi ya peri- urban kwa Majiji makubwa zaidi ya shilingi bilioni 86 za kuanzia zimetengwa na Serikali yetu ya Awamu ya tano kupitia Wizara ya Nishati na taasisi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imefanya uamuzi wa kisera, kupitia agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, baada ya kutafakari upelekaji wa miradi ya nishati vijijini na hoja ya kwamba ikipeleka TANESCO au na wadau wengine kuwe na bei tofauti au ikipelekwa na REA inakuwa na bei tofauti. Serikali imefanya maamuzi kuanzia sasa hivi miradi yote hiyo itapelekewa umeme wananchi wataunganishwa kwa bei ya Sh.27,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme wazi kabisa, Serikali itandelea kupambana na wale Vishoka ambao wanawaongezea wananchi bei lakini bei ya kuunganishia umeme ni Sh.27,000. Hii italeta matumaini hata kwa wananchi tunaowaambia wasubiri kwamba TANESCO watapeleka umeme vijijini kwa kupitia Sh.27,000, REA Sh.27,000 na sekta binafsi nayo Sh.27,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limezungumzwa ni suala la uzalishaji wa umeme. Serikali yetu imefanya mapinduzi kupitia Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, imekuwa na maono ya kuzalisha umeme mwingi ambao utashusha gharama ya umeme. Umeme mwingi utakaozalishwa ni kupitia vyanzo vya maji. Tunao mradi wa Stiegler’s Gorge MW 2,115 tumeshamkabidhi mkandarasi site anaendelea vizuri; Mradi wa Rusumo MW 80 anaendelea vizuri; tumeanza mchakato wa Mradi wa Rumakali MW 358; na Mradi wa Ruhuji MW 222 unaendelea. Kwa hiyo, nataka niseme dhima au mpango huu wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha ifikapo 2025 tunazalisha MW10,000 kwa ajili ya kuhimili uchumi wa viwanda unaojengwa kwa kasi kubwa katika awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme dhima hii au mpango huu wa Serikali Awamu ya Tano ni kuhakikisha ifikapo 2025 tunazalisha Megawati 10,000 kwa ajili ya kuhimili uchumi wa viwanda unaojengwa kwa kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine limezungumzwa hapa kwamba Serikali imeacha kutumia gesi, siyo kweli. Serikali inaendelea kutumia gesi kwenye masuala mbalimbali. Gesi katika kuzalisha umeme; na kwa sasa tuna mradi Kinyerezi I Extension Megawati 185; tumemaliza Kinyerezi II megawati 240; kuna mpango wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme Megawati 300 Mtwara pamoja na njia za kuzalisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukisema eti Serikali imehama kwenye uchumi wa gesi siyo sahihi na hata sasa tunasambaza gesi kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya Jimbo la Mheshimiwa kaka yangu Ulega hapa Mkuranga. Tunaongeza viwanda vitano kuvisambazia gesi ili kupunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mmesikia kiongozi wa Ujerumani ameipongeza Serikali na ameahidi kuleta kiwanda kikubwa cha mbolea na tumeshafikia makubaliano ya bei ya gesi kwenye viwanda vyote vya mbolea. Kwa hiyo, utaona gesi bado ina mchango mkubwa katika uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwamba hivi karibuni pia Mheshimiwa Rais ametuzindulia mradi wetu wa kusafirisha umeme wa Kilovoti 220, Makambako, Songea. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake kwa kazi nzuri anayoifanya na kwenye sekta yetu hatuna shida, hatuna tatizo la pesa. Tumekuwa tukiidhinishiwa na Wizara ya Fedha, nawashukuru sana. Hata ninaposema sasa, zaidi ya asilimia 16 tumeshapata pesa zake. Tunawaahidi tu utumishi uliotukuka na usimamizi wa miradi hii. (Makofi/ Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi/Vigelegele)