Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote nitumie fursa hii kwanza kumpongeza sana Mwenyekiti wetu wa Chama cha Demokirasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lakini pia nimpongeze pia Waziri Kivuli aliyewasilisha taarifa hii vizuri na naomba tu kwamba taarifa hii kwa jinsi ambavyo imeandaliwa vizuri, Mawaziri waichukue itasaidia kujenga Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia sana kuhusiana na utawala bora, mambo yote yanayozungumzwa, maendeleo hakuna na mambo mengine, kama Taifa litakuwa halina utengamano, kutakuwa hakuna maendeleo na maendeleo hayatapatikana. Kwa sababu tunachokizungumza hapa sasa hivi, kila mmoja analia, leo tukiangalia bajeti za Mawaziri wote, karibu zote hakuna bajeti ambayo imefikia asilimia 70, karibu bajeti zote ziko asilimia 30, 40, na 47 mwisho. Kwa hiyo, tutazungumza sana hapa, kinachohitajika ni fedha, zikipatikana fedha miradi itakwenda kutekelezwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kwa nini miradi hii haiwezi kutekelezwa vizuri na kwa nini fedha haziwezi kupatikana? Sababu ni kwamba tumesahau jambo moja. Katika Taifa hili utawala bora limekuwa ni jambo ambalo ni tatizo kubwa sana na lazima tuliangalie kwa umakini mkubwa sana. Tumefika humu ndani ya Bunge tunafanya siasa, tumefika ndani ya Bunge badala ya kujenga hoja za msingi za kutatua tatizo, ni kwa nini hatupati fedha ni kwa nini hatusongi mbele, tunaendelea kufanya siasa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wananchi waliotutuma, hawajatutuma kuja kufanya siasa za namna hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema, unapozungumzia utawala bora, una mapana yake, ukizungumzia utawala bora tafsri yake ni kwamba unazungumzia mambo mengi sana ambayo yanahusiana na maisha ya kawaida ya wananchi. Hata hivyo, unategemeaje maendeleo, kama wananchi wanabaguana, unategemeaje maendeleo kama kuna baadhi ya kikundi kinaonekana ni bora kuliko watu wengine, hayo maendeleo yatatoka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, Mheshimiwa Rais sasa hivi anakozunguka kote huko, ameanza kuwanyooshea vidole Waheshimiwa Mawaziri, anasema hamfanyi kazi vizuri, ameongea na Wizara ya Fedha amesema wamekosea, kwa nini wanaendelea kupandisha kodi, anawaambia TRA kwa nini wanafanya hivi, haya yote tumeshayashauri sana, lakini wakatupuuza wakasema sisi hatufai, tunafanya mambo ya hovyo na sisi ni watu ambao hatuwezi kulijenga Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukweli tu, hata angezunguka huko, anachokizunguimza Mheshimiwa Rais ni kitu kidogo sana, lakini kitu kikubwa ambacho lazima tukiangalie, ni kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa pamoja. Kama Taifa halijakuwa pamoja, tusitegemee maendeleo katika Taifa hili, tusitegemee wawekezaji katika Taifa hili, kama hatutakuwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa ni jambo kubwa sana, demokrasia ni jambo kubwa katika maisha ya binadamu, demokrasia ni maendeleo, lakini leo demokrasia katika Taifa hili, kila wanachofanya CCM huku na Serikali yao wanafanya kwa ajili ya uchaguzi ujao, ndicho wanachokifanya, hawafanyi kwa sababu ya maendeleo na ahadi walizotoa kwenye Ilani yao ya Uchaguzi. Wanafanya mambo yote kwa sababu ya siasa ya kesho ili waweze kufanya vizuri katika uchaguzi unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wanazidi kulia na sasa hivi utawashangaa sana Watanzania, kwa nini Watanzania hawasemi, Walimu wamekaa kimya, hawajapandishiwa mishahara muda mrefu, lakini wamekaa kimya wanawatazama tu. Ukienda kwa wakulima, wamekaa kimya, mazao yao hayanunuliki, soko limeshuka wamekaa kimya wanawaangalia tu. Kwa sababu wakizungumza wanawakamata wanawaweka ndani, wameamua kuwanyamazisha na wao wamekaa kimya, wanataka waone wanaelekea wapi. Wafanyabiashara wamekaa kimya, wananyanyaswa wafanyabiashara katika nchi hii, wamekaa kimya, hawazunguzi kabisa. Leo wanasiasa wameamua kutunyamazisha pia tukae kimya, waendeshe nchi hii kwa hivi wanavyotaka wao, lakini nataka niwaambie, tunakutana kwenye bajeti kila mwaka, tunaangalia utekelezaji wao kwenye bajeti, kila siku, kila Wizara tunakuta wametekeleza chini ya asilimia 50, chini ya asilimia 40, wanatekeleza bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo Mawaziri waweke commitment hapa, ndani ya Bunge, mbele ya Rais, wamwambie Mheshimiwa Rais, tunataka tutekeleze bajeti inayokuja kwa asilimia 80. Mbona Halmashauri zetu wamezipa masharti, kwamba kila Halmashauri ihakikishe kwamba inatekeleza kwa asilimia 80, lakini kwa nini Mawaziri hawataki kujiwekea malengo hayo ya kutekeleza kwa asilimia 80. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tunaendelea kuwashangaa, wameendelea kujichanganya, wameanza kuchekana wenyewe. Leo mnasema Serikali ya Awamu ya Tano, ina maana Serikali ya Awamu ya Nne, ilikuwa ni Serikali ya CHADEMA? Haikuwa Serikali ya CCM? Kwa nini wasizungumze mipango yao ya miaka inayokuja, lakini wanaanza kuzomeana wenyewe, wanasema Awamu ya Tano imekuwa nzuri kuliko Awamu ya Nne. Awamu ya Nne imefanya kazi kubwa, hivi nyie Awamu ya Tano wangejenga chuo cha Dodoma hiki hapa, tungelala na kunywa maji kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hawawezi kuangalia, kwa nini hawawezi kuweka mipango ya muda mrefu. Serikali ni ya kwao, chama ni cha kwao, muda wote wamepewa madaraka ya kuongoza Taifa hili, leo wameanza kuzoemeana, Awamu ya Nne imefanya vibaya, lakini nataka nikwambie…

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakajoka subiri kuna taarifa.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: We dogo vipi wewe!

T A A R I F A

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa rafiki yangu, muda mrefu wa speech yake aliyokuwa anazungumza hapa au maelezo yake, mengi yanazungumzia kukosoa. Nilitegemea angalau katika muda ambao anazungumza angeweka maombi mawili matatu au ushauri katika maombi ya jimboni kwake, angalau maji, barabara, lakini yote anayozungumza ni siasa ambayo haina
faida kwenye jimbo lake na yeye ni mwakilishi ambaye anatoka kwenye jimbo ambalo… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mwakajoka taarifa hiyo. (Kicheko)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu bwana mdogo siwezi kupokea taarifa yake naona ana matatizo huyu bwana mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukwambia, ndiyo maana nimetangulia kusema, leo kila mmoja anazungumza hapa, Waziri wa Fedha alikuja hapa akasema, hakuna fedha. Sasa unaposema kwamba hakuna fedha halafu unataka mimi nianze kusema eti nasifia, nasifia kitu gani wakati hakuna kazi iliyofanyika, hakuna kazi iliyofanyika nasifia kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo kubwa nililolizungumza tunahitaji utawala bora katika Taifa hili. Utawala bora ukiwepo, wawekezaji tunaowataka, wanaweza kuja kuwekeza katika Taifa hili na wakalipa kodi na nchi ikapata fedha.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Frank subiri.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, linda muda watu wanana…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji, anaposema Waziri wa Fedha akisimama anasema hakuna fedha, lakini amesikia, vituo vya afya zaidi ya 352 vimejengwa ndani ya mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshatoa zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshatoa bilioni 1.5 kwa hospitali za halmashauri 67. Anatakiwa aseme mambo ambayo yana ukweli ambayo wananchi wanayaona kwa macho yao, kwamba fedha ipo na Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika majimbo yote likiwemo na jimbo lake yeye mwenyewe. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Frank, taarifa hiyo.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri kama Waziri wa Fedha, kwa sababu ndiye anayewaambia Mawaziri wengine kwamba hamtatekeleza kwa asilimia mnazozihitaji kwa sababu fedha hakuna amekusanya chini ya kiwango na anayekusanya fedha ni yeye. Cha kushangaza, namshangaa, lakini pia kama mama, tukiangalia takwimu za mwaka jana za vifo vya wanawake na watoto, kati ya vizazi laki moja katika nchi hii, watu wanaopoteza maisha ni vizazi elfu sitini na tano, kwa hiyo, elfu 44 wanakuwa wazima. Sasa huwezi kuniambia kwamba, eti umejenga vituo, unajenga vituo madawa hakuna, unajenga vituo vifaa hakuna, ee, una maana gani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukijaribu kuangalia kwenye shule zetu za msingi, watoto wanakaa zaidi ya 250 kwenye shule za msingi. Hizo ndizo takwimu ambazo tunazo, lakini leo anatuambia kwamba, eti anasema kwamba fedha zinatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumza ni kwamba, lazima tutengeneze utawala bora na nawaambia ndugu zangu, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Mawaziri pamoja na Mheshimiwa Rais, asikie, wananchi wamekaa kimya, hawajakaa kimya eti kwa sababu wameridhika na utawala huu, wamekaa kimya na wanapata taarifa kwamba mnategemea kwenye uchaguzi ujao mtapeleka polisi wengi, mtapeleka majeshi mengi, lakini wamesema hawatagombana na jeshi la polisi, watakwenda sasa kujuana na ndugu zao ambao watasababisha wapigwe. Sawa jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niwaambie, lazima tuelewane, wanataka kuleta machafuko katika Taifa hili kwa sababu ya uroho wa madaraka. Haiwezekani wamekubali demokrasia, leo wanataka wabaki peke yao, wakati wananchi hawakubaliani na ninyi, wanahitaji upinzani ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa namsikia Mheshimiwa Jenista Mhagama, anasema watu ambao wamechangia kuhusiana na Katiba Mpya, anasema ni watu wawili, watatu……

MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Frank taarifa.

T A A R I F A

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana mzungumzaji kaka yangu Mwakajoka, lakini nataka nimpe taarifa, si kweli kwamba wananchi hawaipendi au hawakipendi Chama cha Mapinduzi, ni kwamba wananchi wetu huko tunakotoka wameridhika, wanakipenda Chama cha Mapinduzi na mwaka 2020, hali itakuwa mbaya sana kipande cha kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo taarifa yangu.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Frank.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza huyo bwana Akwirina anamlilia sana. Kwa sababu ndiye aliyesababisha Mkurugenzi wake akazuia viapo vya…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Frank elekeza hoja yako kwenye kuchangia.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea….

MWENYEKITI: Taarifa nyingine, Mheshimiwa Frank kaa, taarifa ya mwisho hiyo.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Mheshimiwa Frank taarifa kwamba, anayoyasema ni ya kweli, kwamba bila jeshi la polisi CCM haitafika madarakani na uthibitisho upo, Mheshimiwa Frank kwa mfano Kata ya Turwa Tarime, tuliwashinda CCM kwa kura zaidi ya 76 lakini walitupiga mabomu wakachukua wakajitangaza. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Frank.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea na mimi kwenye kata ya Ndarambo kule kwetu Momba, Mkurugenzi alikuja na polisi zaidi ya 100 ndani ya chumba na akanyang’anya matokeo na akaondoka nayo, kwa hiyo, hili lipo. Kama kweli Mtulia anasema kwamba eti CCM inapendwa na wananchi, wekeni mpira chini…

MWENYEKITI: Ahsante, nilikuongeza dakika moja. (Makofi)