Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikaki za Mitaa). Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai na mwenye afya njema katika siku ya leo niweze kushiriki kuchangia katika hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nami naungana na Watanzania kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi anazozifanya, Watanzania wanaziona. Vilevile nampongeza Mheshimiwa Jafo kwa kazi kubwa anayofanya, kijana huyu ni hodari, lazima tuseme ukweli, anafanya kazi vizuri sana. Niwapongeze Naibu wake; Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Waitara, wanafanya kazi vizuri. Nimpongeze Katibu Mkuu, Eng. Nyamhanga na watumishi wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuanza, naomba nizungumzie barabara za vijijini. Barabara za vijijini ndiyo msingi wa maendeleo katika nchi yetu, kwa sababu huko ndiko kunatoka chakula, kuna wananchi wanyonge na huko ndiko wananchi wanauza mazao kwa bei mbaya kutokana na hali ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliunda hapa chombo cha TARURA kwa matumaini mema tu kwamba kitaweza kutusaidia. Mimi nikiri kabisa kwamba chombo hiki ni kizuri na Watendaji wana uwezo wa kusimamia fedha vizuri kwa ajili ya kujenga barabara, shida iliyopo wanapewa pesa kidogo mno. Sasa matumaini ya Watanzania na sisi Wabunge tunashindwa kuelewa ni kwa namna gani hizi barabara zitajengwa kama tulivyokusudia. Tunaomba kwa kweli chombo hiki kiongezewe pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi katika Jimbo langu nina barabara sugu sana, lakini ninachokiona hata mgawanyo wa pesa hizo ndogo hauendi sawa, ni kama kuna upendeleo wa namna fulani. Nakuomba kabisa uagalie ukurasa wa 196, angalia mgao wa fedha katika Halmashauri ya Sumbawanga DC vilevile uende ukurasa wa 200 - 201 uone jinsi Halmashauri ya Sumbawanga DC ilivyopata pesa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hapo twende kwa Mkoa mzima wa Rukwa, umepewa shilingi bilioni nne, mkoa wenye uzalishaji mkubwa na wenye barabara sugu na mvua nyingi ambazo zinaharibu barabara kila siku kupewa kiasi hiki siyo sawa. Kwa kweli naona jambo hili sio jema, mtafakari upya na maeneo niliyokwambia yafuatilie utaona kama ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie barabara sugu ambazo ziko katika maeneo yetu ambazo tulizipitisha kwamba walau zikitengenezwa hizi, zinaweza zikasaidia kiasi fulani. Barabara ya Kahengesa - Kitete pamoja daraja; barabara ya Kahengesa – Itela – Ntumbi – Ilembo; na barabara ya Mawenzuzi – Msia. Barabara hii Serikali iliwahi kutupa pesa shilingi milioni 400 lakini imeitelekeza maana yake zile pesa thamani yake itapotea kwa sababu hakuna nyongeza iliyoongezeka ili barabara iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ni barabara ya Mtowisa - Ng’ongo. Barabara hii ni ahadi ya Makamu wa Rais, hebu tumheshimu Makamu wa Rais, kwa huruma ya akina mama akasema hii barabara lazima itengenezwe kwa changarawe. Nashangaa mpaka sasa hivi sioni ahadi ile kama inatekelezeka na miaka inaendelea kuisha. Ni lazima tumheshimu mama huyu kwa kazi anazozifanya, walau tumpe upendeleo wa barabara hii iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara Mihangalua - Chombe na Chombe – Kahoze. Hizi barabara nazozungumzia ni barabara sugu. Barabara zipo nyingi lakini hizi tulizitenga kwamba ni sugu, zikitengenezwa zinaweza zikapunguza kiasi fulani maumivu kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni katika ukurasa wa 5 ambapo Mheshimiwa Waziri umeelezea namna Serikali ilivyojipanga katika kujenga majengo ya utawala. Nimeangalia nikaona Sumbawanga DC ambayo ina jengo la utawala ilianza kujenga mwaka 2011 mpaka sasa hivi halijaisha, Serikali ilitupa shilingi bilioni 1.6 na mkataba wa jengo hili ni shilingi bilioni 2 na mwaka huu tuliomba shilingi milioni 700 lakini hatujapangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo limechukuwa miaka mwishowe litachakaa, watumishi watakosa pa kufanyia kazi, kumbukumbu zitahifadhiwa wapi? Naomba Mheshimiwa Jafo ulione hili, jengo ni la muda mrefu, ni ghorofa moja, miaka imekuwa mingi na linachakaa na tuliomba pesa tunashangaa hamjatupangia. Tunaomba Mheshimiwa Jafo uliangalie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la wakandarasi upande wa maji hawalipwi kwa wakati. Kama tatizo ni pesa kwa sababu tatizo la maji ni kwa nchi nzima, tulijadili kwa pamoja tutafute ufumbuzi kuliko wakandarasi wanafanya kazi muda mrefu wanadai pesa hawapati sasa tunaanza kushangaa tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ahadi ya Serikali inavyosema miradi ya maji itajengeka, sijaona itajengeka kwa namna gani, kwangu mpaka sasa hivi nina wakandarasi zaidi ya wanne wanadai pesa hawajalipwa. Kwa mfano, mkandarasi wa mradi wa pale Ikosyi, alipeleka vifaa ameanza kujenga, mwishowe ameamua kuviondoa kwa sababu hajalipwa na amedai kwa muda mrefu na nimefuatilia mara kadhaa nashangaa Serikali haijamlipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda kuzungumzia upande wa afya. Kwanza kabisa, niishukuru Serikali mmetupa shilingi 1,500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, hongereni sana. Halafu mmetupa shilingi 400,000,000 kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya na kwenye bajeti hii mmetupa shilingi 200,000,000 kwa ajili ya kupanua Kituo cha Afya pale Mpuli, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kuongezea Mheshimiwa Waziri uliangalie Jimbo lilivyo na jiografia yake. Nashukuru kwa hiki mlichotupatia lakini hebu jaribuni kutanuka zaidi. Mimi Jimbo langu ni kubwa na jiografia ni mbaya, majimbo mengine yamepata vituo vya afya vinne, vitatu sasa najiuliza, jimbo langu ambalo ni kubwa na Mheshimiwa Jafo umefika umeliona mpaka ukatuonea huruma, hebu jaribu huruma hiyo upeleke kwenye vitendo. Tunaamini kwa sababu utakuwa umesikia na ni kijana msikivu endelea kulingalia uweze kutuongezea kituo kingine cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie tatizo la gari. Jimbo langu halina gari la wagonjwa na mazingira unayajua, nimeomba gari hili karibu miaka mitatu, unaenda mwaka wa nne, naahidiwa sijapewa. Naomba na lenyewe hilo Mheshimiwa Jafo uweze kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni maombi ya fedha za kumalizia maboma yetu. Tuna zahanati 20 ambazo zimejengwa na wananchi kutoka usawa wa lenta na wengine wameweka na mabati, tunaomba tupewe fedha za kumalizia hizo zahanati vinginevyo wananchi watakata tamaa. Tunavyo vituo vya afya kama vitano ambavyo wananchi wameshajenga majengo ya utawala wakaezeka tunasubiri kupewa fedha tuweze kumalizia ili yaweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile upande wa watumishi, tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Halmashauri ya Sumbawanga DC ina upungufu wa watumishi 667. Ukiangalia mgao unaotolewa unakuta sisi tumepata kidogo hata wale ambao wana nafuu wanapata watumishi zaidi. Sijajua ni vigezo gani vinatumika katika kugawa watumishi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jamani mtuangalie maana Sumbawanga DC tuko vijijini, mara nyingi tukisema Sumbawanga DC mkija mnafikiri ni pale mjini, hapana, kuna mazingira magumu sana, Mheshimiwa Jafo umetembea umeyaona, hata Waziri Mkuu alipita akashangaa kwamba katika nchi hii kuna mazingira ya namna hii. Sasa kama hata viongozi mmeyaona si mtupendelee basi hata wa kutupa wa fedha. Kama mmekataa kugawa Halmashauri na Jimbo basi tupeni fedha za kukidhi mahitaji na shida za wananchi. Sasa kama kotekote mnatunyima wananchi watatufikiriaje? Tunaomba sana jambo hili muweze kuliangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu, tuna maboma mengi. Kwenye Halmashauri yangu tuna maboma 259 ya madarasa na nyumba za Walimu tunaomba na hilo mfikirie. Tunashukuru mmetupa shilingi milioni 75, lakini ukilinganisha na maboma yale, kwa kweli hakuna uwiano, hazitoshi. Tunaomba na lenyewe hilo muweze kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni upande wa posho za Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Madiwani. Lazima tufike mahali tulitazame jambo hili. Hata miradi mikubwa tunayopeleka, ni wale ndio wanaosimamia, wanashinda kutoka asubuhi mpaka jioni bila posho. Hebu fikiria kama ungekuwa ni wewe, ungeweza kufanya kazi hiyo. Tujaribu jamani kutafuta namna yoyote ya kuwafuta jasho hawa watu, angalau kama hatuwezi kuwapa mishahara, basi tuweke hata posho, baada ya uongozi wake apate hata kiasi fulani cha kumfuta jasho, hata kama hapati mshahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanafanya kazi kubwa sana. Kama hatuwapi posho ya kutosha hawa Madiwani basi tuwatengee posho hata mara moja baada ya miaka mitano mtu aweze kupata posho ya kufuta jasho lake kuliko kuacha kama jinsi ilivyo. Hawa watu wanafanya kazi kubwa mno. Nasi tunashuhudia tukienda tunashinda nao, unaweza ukachoka, wenyewe wanaendelea. Hebu jamani mjaribu kuangalia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napenda kuishukuru Serikali, tulikuwa na kilio cha muda mrefu cha daraja la mto Momba. Nashukuru daraja hili linaelekea kukamilika, Serikali imetupa shilingi bilioni 17,700,000,000/=, daraja hili linaelekea mwisho, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tusiishie hapo, lengo la daraja ile ni kuunganisha mikoa mitatu. Kwa hiyo, tunaomba sasa Serikali ifikirie namna ya kuanza kujenga barabara ile kwa kiwango cha lami. Mkifanya hivyo, mtakuwa mmetutendea haki wananchi wa maeneo yale na ni maeneo kwa kweli yenye uzalishaji, hakuna zao linalokataa katika maeneo yale, lina rutuba nyingi sana. Mazao mengi mnayoyaona hata kule Mpanda, yanatoka Sumbawanga Vijijini; hata huko Mbeya Tunduma yanatoka Sumbawanga Vijijini. Kwa hiyo, ndiyo maeneo yenye uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali iweze kuangalia jambo hilo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. IGNAS A. MALOCHA Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)