Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hizi mbili; Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais wetu ametukopesha Watanzania imani, ametukopesha Watanzania mapenzi, ametukopesha Watanzania utu wema, ametukopesha Watanzania kazi, ametutendea haki. Tunaahidi 2020 kulipa alichotukopesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanamna pia ya pekee nichukue fursa hii nimshukuru Rais wangu wa Zanzibar,mwongeaji aliyepita kabla ya huyu aliyekaa alizungumzia Zanzibar naakasema kwamba hali ya kisiasa haiko vizuri. Niseme katika ukumbi huu kwamba Zanzibar hali ya kisiasa iko vizuri, Rais wa Zanzibar anaisimamia siasa ya Zanzibar vizuri hatuna mashaka usiku na mchana tunatembea bila wasiwasi na siasa inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Mawaziri wa Wizara zote mbili nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Jafo, kazi kubwa anayoifanya pamoja na wasaidizi wake, lakini pia nimpongeze Waziri wa Utawala Bora kazi kubwa wanazozifanya Mwenyezi Mungu atawalipa, maana tukisema tu kwa mdomo haitoshi lakini tuseme kwa vitendo tunaiona kazi kubwa wanayoifanya, tunasimama kutimiza wajibu na kuona maeneo gani ambayo wanahitajika kuongeza nguvu ili tuweze kwenda vizuri kwa pamoja.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama leosuala kubwa ninalotaka kulizungumza ni suala la Mfuko wa Wanawake,Vijana na Watu Wenye Mahitaji Maalum. Nimwambie kaka yangu, Mheshimiwa Jafo pamoja na kazi kubwa na majukumu aliyokuwanayo na wasaidizi wake,aweke mkazo kwenye suala la Mfuko wa Vijana, Wanawake na Watu Wenye Mahitaji Maalum. Sehemu hii tunahitaji mkazo wa kipekee, suala kubwa ndani ya Taifa letu, janga kubwa tulililokuwa nalo ni suala la ajira kwa vijana. Kwa maneno ya vijana wanakwambia hatuna njia ya kutokea isipokuwa kwenye Mfuko huu. Kaka yangu, Mheshimiwa Jafo mengi anayoyafanya tunampongeza na mazuri, mazuri na yakupigiwa mfano. Tunamwomba kaka, kwa vijana wanawake na watu wenye mahitaji maalum aweke mkakati mahususi wa kuusimamia Mfuko huu ambao utakwenda kuwakomboa wanawake na vijana. Mfuko huu upo na unafanya kazi, lakini unasuasua, haupo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ndani ya Kamati ya LAAC miaka mitano Mwenyezi Mungu aliyonipa kibali cha kuingia Bungeni kupitia nafasi za vijana, nilikaa ndani ya Kamati ya LAAC, Mfuko huu haufiki kwa vijana kama ipasavyo, haufiki kwa wanawake kama ipasavyo na kwa sasa tumeongeza kufika kwa watu wenye mahitaji maalumu. Mpaka sasa ninavyoongea namshukuru Mheshimiwa Spika kwa kunirudisha tena kwenye Kamati ya LAAC, kwahiyo napata kujua tathmini mambo yanakwendaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jafo halmashauri zinaendelea vizuri,hatusemi kwa asilimia mia moja, lakini zinaendelea vizuri, jitihada zake zinafanya kazi, aweke mkazo kwenye Mfuko huu ili vijana wapate kutoka, akiwapa fursa vijana kutoka kupitia Mfuko huu, namwambia kaka, Mheshimiwa Jafo hatuna wasiwasi na yeye, Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti,Mfuko huu waVijana, Wanawake na Watu Wenye Mahitaji Maalum ndiyo kwenye kilio, labda kaka, Mheshimiwa Jafo ifike wakati nikutolee mfano, kuna halmashauri ya mwisho wakati tupo kwenye Kamati, tulikwenda Halmashauri ya Kahama kama sikosei. Halmashauri ya Kahama wana mradi unahitwa unaitwa Mradi wa Dodoma. Kaka, Mheshimiwa Jafo mradi ule umetoa ajira kupitia huo huo Mfuko, ajira elfu moja mia tano na sabini na tisa, lakini hapo hapo wamepatiwa viwanja wanawake, vijana na watu wenye ulemavu watu738.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama nimwombe jambo moja tu kaka, Mheshimiwa Jafo, aendeakakague kama itamridhisha, kama ule mradi umefanywa upo sana salama ashawishi na halmashauri nyingine ziige. Ni mfano wa kuigwa, leo kijana wa Tanzania aliyekuwa akiuza karanga, aliyekuwa akipanga mananasi matatu, manne, Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu anapata hati miliki ya kiwanja bure.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kamakaka, Mheshimiwa Jafo utamridhisha,atauhisi uko salama, hautakuwa na matatizo mbele ya safari akauangalie,ashawishi na halmashauri nyingine. Naamini kama utakuwa mradi mzuri, basi halmashauri nyingi zikitaka, vijana watapata mabadiliko kwa sababu leo kijana ana hati miliki kwamba ana sehemu anapamiliki, anaenda kukopa wakati wowote, saa yoyote, benki yoyote, kwa sababu hati miliki ya kumiliki anayo.
Sasa nimshauri na kumwomba Mheshimiwa Jafo kwamba, akiangalia na ukimridhisha, kama itawezekana mfumo unaotolewa fedha kwa vijana kupitia halmashauri, kwa sasa fedha hazina marejesho, vijana wakipewa fedha hawarejeshi, lakini kama tutatumia mfumo huo kwamba amepatiwa viwanja bure,wameenda kukopa huko mwenyewe, wataelekezwa utaratibu mzuri wa kukopa, watasimamiwa na mabenki basi mambo yataendelea kwenda vizuri.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimwambie kaka, Mheshimiwa Jafo kwamba tuwapongeze pamoja na Utawala Bora, zamani ukienda halmashauri, wafanyakazi wa halmashauri, Mkurugenzi kaenda leo wanasema kesho ataondoka, lakini sasa hivi mambo hayako hivyo, kila mfanyakazi aliyekuwepo kwenye halmashauri akiiona Kamati ya LAAC anatamani kuulizwa ajibu nini kinaonesha kwamba wafanyakazi wameelimika, wamefundishwa vya kutosha, utawala bora unaonekana. Niwaombe kwamba waendelee kusimamia bila wasiwasi…
T A A R I F A
MWENYEKITI: Taarifa Mwakanyoka.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji, amekuwa ana tamka mara kwa mara kaka Jafo kwa mujibu wa kanuni, ni kwamba lazima aheshimu sana nafasi yake awataje kwa vyeo vyao kama ni Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aseme ili na watu wamwelewe na hansard ziweze kusoma vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tauhida.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti,naipokea taarifa yake. Asiwe muungwana kwa hapa, awe muungwana na kwa mengine wanayoyaona Rais yetu anayoyafanya na Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri ni Mawaziri, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naomba waendelee kuwasimamia wafanyakazi. Kulikuwa na tatizo sugu la mfanyakazi anaharibu halmashauri moja, ugonjwa wake unahamishiwa halmashauri ya pili, kaka Jafo…
WABUNGE FULANI: Aaa,aaa. (Makofi/Kicheko)
MHE. TAUHIDA CASSSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Waziri sijaona kipindi hiki hilo tatizo, hilo tatizo limepungua kwa asilimia kubwa. Niseme kwamba kulikuwa na matatizo ya ma-engineer kutokujua wajibu wao, lakini sasa mambo yamebadilika hayajaondoka, hayajamalizika, lakini yamepungua. Kwahiyo, Mheshimiwa Waziri kwa maeneo wanayofanya vizuri lazima tumpongeze, lakini asiache kuendelea kusimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo pia la kukaimu, Mheshimiwa Waziri ajitahidi kwenye hili. Mtendaji waHalmashauri unapomwambia kakaimu hawajibiki ipasavyo, kwanza anawajibika kwa hofu, jambo la pili anachofanya ni kufanya kazi kwa kutokujiamini. Kwahiyo, Mheshimiwa Waziri kamahili eneo utalisimamia kumaliza suala la watu wanaokaimu, litatusaidia na tutaendelea kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine linalosumbua ni suala la Wanasheria waliokuwepo ndani ya Halmashauri. Nafikiri ni muda mzuri wa kukaa na Wanasheria waliokuwemo ndani ya halmashauri na wanaotaka kuwapeleka, kwa sababu baadhi ya halmashauri bado hazina Wanasheria, mambo mengi ambayo yanaharibika ndani ya halmashauri chanzo kinachosababisha na kinachochangia pia ni kutokuwa na Wanasheria wazuri. Wapeleke Wanasheria wazuri ambao wataweza kuisaidia halmashauri hususan kwenye suala la kuingia mikataba, halmashauri zimekuwa zikilega lega au zikiharibika kwenye suala hili au haliko vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kama maeneo haya atayakazia vizuri na kuyasimamia vizuri, nafikiri kwamba kero na matatizo ya ndani ya halmashauri yatakwisha.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tauhida.
MHE. TAUHIDA CASSSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwaasilimia mia moja.(Makofi)