Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii. Moyo usio na shukrani hukausha mema mengi. Napenda kuwapongeza Mawaziri; Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Mkuchika na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na Wakuu wa Taasisi wanazoziongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jambo hili kwanza napongeza kwa sababu nimepata vituo viwili vya afya; na cha kwanza kiko hapa cha Kahangara kwenye mfano wa hotuba hii. Bado nina vituo vya afya vitatu; Kituo cha Afya cha Kabila pamoja na Kituo cha Afya cha Kisesa na Nyanguge. Vituo hivi ni muhimu sana, Serikali ione namna ya kuweza kunisaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Mbatia anachangia hapa, ndiyo maana nimeanza na moyo usio na shukrani; Mheshimiwa Mbatia ameishukuru Serikali hii. Kama wapinzani wa nchi hii wangekuwa kama Mheshimiwa Mbatia, upinzani ungeweza kusaidia nchi. Kwa sababu michango aliyoitoa ni kwa maslahi ya Taifa hili. Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inaendelea kuboresha huduma. Kwenye hospitali, ninajua mnaendelea kujenga hospitali mpya, lakini hata hospitali yangu ya Magu, Mheshimiwa Jafo ni shahidi amefika mara mbili, inahitaji ukarabati. Kwa sababu tumezungumza naye ninaamini jambo hili atalichukua kwa uzito wa pekee kwa sababu yeye ni shahidi amefika OPD, inaweza kuanguka wakati wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye barabara. Magu tuna kilometa za barabara 1,600. Kwenye bajeti hii tumepangiwa shilingi milioni 900, hazitoshi hata kidogo. Naiomba Serikali, kwa sababu TARURA inapokea asilimia 30 na TANROADS inapokea asilimia 70, wangalie namna ya kubadilisha sheria ili mradi TARURA ipate asilimia 50 na TANROADS ipate asilimia 50 ili barabara zetu za wilayani kule ziweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza sana Chief wa TARURA ni msikivu. Ukimpigia simu wakati wowote anapokea, naye anazunguka kwenye barabara zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna daraja pale Mahaha, Itubukiro kwako kule, tunaunganishwa na daraja, halipo. Ili kuunganisha mawasiliano ya kiuchumi ni vizuri waangalie TARURA namna yoyote ambayo wanaweza kutusaidia madaraja ili tuweze kuunganisha hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna barabara ya Magu – Isolo, kuanzia Kabila – Isolo na Isawida kule kutokea Itilima, pale tunatenganishwa na daraja. Magu tumelima mpaka kwenye mpaka wa Itilima na Itilima imelima mpaka kwenye mpaka wa Magu; TARURA ninakuomba utupatie daraja na tulikuja ofisini kwako na Mheshimiwa Njalu kuomba pale utupe daraja ili tuweze kuunganisha mawasiliano ya wilaya hizo mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Magu tumejenga maboma vijiji 21 ambayo yako tayari, zinahitajika fedha za kuweza kukamilisha na hili ni la ki-Ilani. Tulisema Ilani ya Chama cha Mapinduzi kila kijiji kiwe na zahanati, wananchi wameitikia, wamejenga, wanahitaji kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii kama ambavyo inafanya kazi, iangalie namna ya kutoa fedha kwa ajili ya maboma ya nchi hii ikiwemo Wilaya ya Magu ili tuweze kuwapa nguvu wananchi kwa kazi ambazo wamezifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkanganyiko wa waraka. Waraka uliokuja unasisitiza nyaraka zilizopita, lakini Wakurugenzi wameshindwa kutafsiri waraka huu. Wamefuta per diem wamekwenda kusisitiza kwenye sitting pekee. Madiwani hawa ni viongozi, ndio wanaofanya kazi, ndio Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata, ni vizuri tukawaona. Kwa sababu hawa huwa tunachagua nao siku moja, ni vizuri tukawapa maslahi yao ya kweli. Kuna Diwani anatoka kilometa 40, kuna Diwani anatoka kilometa 20; wao wameangalia tu pale mwisho kwamba kama kuna uwezekano wa kutolala wasilipwe per diem. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni Mbunge. Mbunge na Diwani kila kunapokucha asubuhi watu wanajaa ukiwa Jimboni au kwenye Kata yako. Ndiyo maana ikawekwa per diem ili Diwani atoke kwenye familia yake aende akalale Makao Makuu ili concentrate vikao vya Halmashauri. Kwa hiyo, perdiem hii wanapaswa walipwe Waheshimiwa Madiwani hawa. Madiwani hawa hakuna sherehe inayompita, hakuna kilio kinachompita na hakuna mgonjwa anayempita. Mimi nilikuwa Diwani na sasa ni Diwani kwa mujibu wa sheria kwa sababu ya Ubunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana TAMISEMI, Mheshimiwa Kandege uko hapo. Kandege andika hili, Kandege andika hili, mtafasiri waraka huu, ili Madiwani waweze kulipwa per diem yao. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga naona umepandisha? Mwite tu Mheshimiwa Kandege.
MHE. MUNGE FULANI: Aongezwe dakika huyu.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kwa mamlaka uliyokuwanayo.
MWENYEKITI: Tumia basi lugha ya Kibunge, mwite Waziri Mheshimiwa Kandege.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Kandege. Mheshimiwa Kandege. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Tena, rudia!
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Kandege, sikiliza hili na aandika ili mtafsiri waraka huu Madiwani waweze kulipwa perdiem. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sauti yangu ni ya msisitizo, nasisitiza tu, siyo kwamba, labda nafoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye Service Levy. Hii Service Levy wakati inatungwa Sheria ya Serikali za Mitaa ilikuwa inalenga viwanda. Kwa mfano, kama kiwanda cha Tanga Cement kimezalisha simenti na inauzwa hapa Dodoma, Halmashauri ya Dodoma ina-claim madai yake ya Service Levy Tanga. Leo Tanga Cement kama hapa Dodoma ina tawi, inatozwa hapa, akinunua Dodoma hapa kupeleka Mvumi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kiswaga.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naunga mkono hoja. Kumbe dakika 15 ni muhimu sana.