Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami niendelee kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu. Pia niendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunijalia afya njema ili niweze kutoa michango yangu katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoanza kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora, naomba kuanza kwa kusema kuwa mwanazuoni mmoja ametafsiri viongozi wa kisiasa kuwa ni muhimu sana katika mamlaka za Serikali na hufanya maamuzi sahihi yanayoweza kuleta manufaa zaidi katika ustawi wa Taifa na watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kuanza kwa kusema hivyo nikiamini kwamba sisi kama Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukiwa kama viongozi wa kisiasa tunalo jukumu la kuhakikisha kuwa tunaishauri Serikali, tunaisimamia vyema ili kuhakikisha ustawi wa Taifa letu pamoja na wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa sababu yeye ameonyesha mfano wa yale ambayo nimeyatangulia kuongea, akiisimamia nchi yetu ya Tanzania kuhakikisha kwamba Watanzania wanaongozwa vizuri katika sehemu ya Utawala Bora lakini pia Watanzania wanaweza kupata ustawi na maendeleo katika nchi ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI nikianza na suala la ujenzi wa vituo vya afya, pamoja na hospitali. Serikali imejitahidi sana kujenga na kukarabati vituo vya afya na hospitali, hiyo yote ni katika kuhakikisha inaboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Mkoa wa Mwanza tumefaidika katika ukarabati na ujenzi wa vituo vya afya kama ambavyo imekuwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini, Mkoa wa Mwanza tumepata takribani shilingi bilioni 10.3 ambayo imetusaidia kurekebisha vituo vya afya katika maeneo mbalimbali Mkoani Mwanza vikiwemo Wilaya ya Ukerewe, Wilaya ya Kwimba, Wilaya ya Magu, Wilaya ya Misungwi na Wilaya nyingine zote Mkoa wa Mwanza zimeweza kufaidika kwa kupata vituo vya afya na hospitali za wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizo za Serikali, zipo changamoto mbalimbali ambazo zinatokea katika jamii yetu. Maeneo kama ya visiwani, bado hawajaweza kupata huduma za afya kwa sababu wanatembea umbali mrefu na ukiangalia Mkoa wa Mwanza ni Mkoa umezungukwa na visiwa vingi. Kwa maana hiyo, wananchi wanapata changamoto ya usafiri kuweza kufikia huduma za afya kwa ukaribu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ukiangalia Wilaya ya Ukerewe na Wilaya ya Ilemela, kuna Visiwa vya Irugwa Kisiwa cha Bezi. Wananchi ambao wanahishi katika visiwa hivyo ambavyo nimevitaja bado wanapata changamoto ya kufikia huduma huduma za afya. Ombi langu kwa Serikali, naiomba Serikali katika bajeti yake hii waweze kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza kujenga vituo vya afya katika maeneo hayo ya visiwani ili wananchi waweze kuzifikia huduma za afya kwa ukaribu na hatimaye kuweza kuokoa maisha ya wananchi, hususani tukiwalenga kundi maalum ambalo ni akina mama na watoto ili kuweza kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Mwanza pia tunayo Hospitali ya Ukerewe ya Wilaya ambayo ipo pale Nansio. Hospitali hii ya Wilaya ya Ukerewe inawahudumia wananchi wengi sana kutoka maeneo ya visiwani kule Ukerewe. Sasa kuwapunguzia wananchi kutoka Ukerewe kwenda kupata tiba au kwenda kupata huduma za kiafya za kibigwa, ninaishauri Serikali kuweza kukarabati Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe ambayo ipo pale Nansio. Hii itawasaidia wananchi wanaotaka huduma maeneo yale kwani hawapati huduma za kibigwa za kiafya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, naiomba Serikali iweze kutenga fedha katika kipindi hiki cha bajeti ili kuhakikisha kwamba hospitali hii ya Wilaya ya Ukerewe ambayo inahudumia wananchi wengi iweze kutoa huduma za Kibigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuchangia katika suala la elimu. Pamoja na juhudi za Serikali kujenga madarasa na shule za mabweni katika maeneo mbalimbali, bado tunazo changamoto kwa watoto wetu wa kike ambao wanatembea mwendo mrefu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wa kike anapotembea mwendo mrefu, njiani anakutana na vikwazo mbalimbali. Atakutana na madereva wa bodaboda watamshawishi kupanda usafiri ili aweze kufika haraka shuleni. Atakutana na watu tumezoea kuwaita mashunga dadys, wataweza kumrubuni mtoto wa kike na kukatisha masomo yake hatimaye aweze kupata ujauzito ama la aolewe akiwa bado ni mdogo na hatimaye kukatisha ndoto zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali kufanyika, lakini bado tunayo changamoto ambapo sehemu mbalimbali ambazo ziko mbali na maeneo ya shule za msingi, zinazo-feed shule zetu za Kata za Serikali kwa wanafunzi kutembea mwendo mrefu. Tunaishauri Serikali iweze kujenga shule za mabweni katika shule zetu za kata ili iweze kuwasaidia watoto wa kike wasiweze kutembea mwendo mrefu kwenda kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mkoa wa Mwanza, sisi tunazo baadhi ya shule hapa ambazo nitazitaja ili Serikali iweze kuzisaidia. Kwa sababu nimeona katika ukurasa wa 124 katika kitabu hiki cha Wizara ya TAMISEMI wamesema kwamba watajenga shule za mabweni kwa kupitia EP4R. Kwa hiyo, naomba katika mpango huo shule hizi ikipendeza ziweze kuingia katika mpango huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ya Bwisia ambayo iko Wilayani Ukerewe, Shule ya Sekondari Bujiku Sakila ambayo ipo Kwimba, Shule ya Sekondari Kabila ambayo ipo Wilayani Magu na Shule ya Sekondari Nyamadoke ambayo ipo Buchosa. Sehemu hizi zote ambazo nimejaribu kuziainisha, wanafunzi wanatembea zaidi ya kilomita tano kwenda kutafuta elimu. Hivyo, naamini kabisa kwa kufanya hivyo, wanafunzi wa kike wataweza kufaidika na hatimaye kufikia ndoto zao kama sisi wengine tulivyoweza kuzifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuongelea suala la asilimia kumi ambalo linatakiwa kutenga na Halmashauri zetu kwa mujibu wa sheria ambayo tulipitisha wenyewe hapa Bungeni kuhusiana na wanawake ambao wanapata asilimia nne, vijana ambao wanapata asilimia nne na asilimia mbili inatakiwa kutolewa kwa watu wenye ulemavu. Kwa bahati mbaya sana baadhi ya Halmashauri zetu hazitimizi sharti hili la kutenga hii asilimia kumi. Nafahamu kabisa kwamba Halmashauri mbalimbali zinapata changamoto ya mapato kuwa ni madogo lakini kwa sababu hiki kitu kimewekwa kisheria, ninaamini wanatakiwa kuzitenga fedha hizi. Kwa bahati mbaya fedha hizi hazitengwi, matokeo yake, hata viongozi wakubwa wanapokuja kutembelea katika Majimbo yetu, taarifa ambazo wanazopatiwa siyo za ukweli. Kwa mfano, wanaambiwa Halmashauri imetoa shilingi milioni 500, unajiuliza swali, hivi katika Halmashauri kwa mfano ya Jiji, hiyo ndiyo fedha pekee iliyopatikana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali kuhakikisha wanafuatilia Halmashauri ambazo hazitengi fedha hizo za asilimia kumi ili waweze kuzitenga na kuweza kuwasaidia wananchi.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako mzuri.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)