Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nianze nyuma niende mbele. Naomba nianze na hilo la Tume ya Uchaguzi kwa sababu limeongelewa sana.

Mheshimiwa Mewnyekiti, wewe ni Mwanasheria na Katiba ya mwaka 1977 na marekebisho yake yaliyofanywa mara kwa mara, wewe ulihusika. Tume ya Uchaguzi imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 74 1(a). Katiba imeelezea Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi anapatikanaje; japokuwa anachaguliwa na Rais, lakini (a) inasema, “Mwenyekiti ambaye atakuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani, au mtu mwenye sifa ya kuwa Wakili na amekuwa na sifa na hizo kwa muda usiopungua miaka 15.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipengele (b) kimetaja “Makamu Mwenyekiti,” naye, hivyo hivyo atakuwa Jaji wa Mahakamu Kuu na sifa ambazo zinafanana. Wajumbe wengine watachaguliwa kwa mujibu wa sheria ambazo zimetungwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 74(3) imetaja watu wafuatao ambao hawataweza kuwa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi; imetaja Waziri au Naibu Waziri, Mbunge, Diwani, kiongozi yeyote wa chama cha siasa. Sasa hawa wamewekwa kwa mujibu wa Katiba na wamewekwa na sifa. Hapa tumeona wapinzani wakiwasifia Majaji. Mfano, Jaji Rumanyika wamekuwa wakimsifia, sasa wangewekwa sifa sawa na walizochaguliwa Wakurugenzi hawa sio wangesema makada wa CCM au wanataka watumie mfumo gani kuwapata? Wangesema waje humu tuwapigie kura si bado tungewachagua hao hao wa CCM maana yake Wabunge wa CCM ni wengi.

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanataka wajumbe wa namna gani wachaguliwe kuwa…

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa

T A A R I F A

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayeendelea kuzungumza. Tunavyosema Tume Huru ya Uchaguzi, tuna maana tume ambayo baada ya kuchaguliwa hata angekuwa ni Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Zitto ndio Makamishna au ndio Mwenyekiti na sijui nani wa tume kwa muundo uliopo hiyo tume haiwezi kuwa huru kwa sababu hiyo ina watumishi wengine wa kuazima kwenye TAMISEMI ambao msingi wao wa uteuzi ni makada na ushahidi upo na hawawajibiki kwa tume, wanawajibika kwa wale waliowaajiri ambao ni makada vilevile. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga unasemaje kuhusiana na taarifa hiyo?

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa kwa sababu namuheshimu nitaendelea. Tume hiyo hiyo ambayo wanailaumu wanasema si huru, katika majimbo 262, mwaka 2015 CCM imechukua majimbo 188, CUF wamechukua majimbo 35, CHADEMA wamechukua majimbo 34, NCCR moja, ACT moja, Mheshimiwa Lowassa ambaye alikuwa mgombea wa UKAWA amepata kura milioni sita, Mheshimiwa Magufuli amepata kura milioni nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tume hiyo hiyo ambayo siyo huru kuna Wabunge kama Mheshimiwa Halima Mdee ni mara ya pili anaingia Bungeni, Mheshimiwa John Mnyika anaingia mara ya pili, Mheshimiwa Sugu anaingia mara ya pili, Mheshimiwa Zitto mara ya tatu tena kabadilisha na majimbo bado kashinda, Mheshimiwa Mbowe mara ya pili, Mheshimiwa Selasini mara…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo tume ya namna gani ambayo wao wanaitaka, hao watu wangeingiaje

MWENYEKITI: Taarifa

T A A R I F A

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa poyoyo kwamba mimi kuingia mara mbili mara ya kwanza walikufa watu wawili…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sugu, hebu futa hilo neno uliloanza kutumia

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuta poyoyo. Mimi kushinda mara ya pili, mara ya kwanza kuna watu walizikwa, vita brother, matairi yamechomwa, watu wamelazwa, watu wamepigwa risasi, watu wamekaa hospitali mwaka mzima, unaona wewe. Mara ya pili…

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Mlinga taarifa hiyo unasemaje?

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sishangai kuniita poyoyo kwa sababu umesikia mwenyekiti wake ametetea bangi kwa hiyo sio suala la kushangaa…

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye mada. Naomba nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa…

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilindie muda wangu.

MHE. ALLY S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa WABUNGE FULANI: Kaa chini wewe, kaa chini wewe. MWENYEKITI: Ukiona nimenyamaza nimeikataa, endelea Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimeitwa poyoyo japokuwa imefutwa, lakini sishangai kwa sababu umesikia Mwenyekiti wake ametetea bangi kwa hiyo sishangai wafuasi wake kutetea mambo ya kijinga.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga naomba ukae. Sasa naku-address wewe Mheshimiwa Mlinga. Nakuomba sana ile kauli ya kumuhusisha kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwamba ameruhusu bangi, naomba uifute tu hiyo, uendelee kuchangia, futa kauli hiyo.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nafuta hiyo kauli na naendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Manaibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa TAMISEMI…

MWENYEKITI: Nimekataa taarifa please.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Jafo ameitendea haki Wizara hii. Wizara hii ni kubwa sana na ina bajeti kubwa mno lakini ameitendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Ulanga naomba nitoe shukrani kwa mwaka wa fedha uliopita tumepata shilingi milioni 117 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekondari ya Celina Kombani tumepata milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wa kituo cha afya cha Lupilo, tumepata milioni 214 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma, tumepata ujenzi wa shule na madarasa zaidi ya milioni 400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata pikipiki 19 na gari moja ya ukaguzi wa elimu, kwa kweli kazi inafanyika. Hata hivyo, nina jambo moja la uboreshaji wa kitengo cha ukaguzi. Wizara hii ni kubwa na bajeti yake ni kubwa ambayo inatolewa lakini bado kuna upungufu kwenye ufuatiliaji wa matumizi ya hizi pesa. Kuna kitengo cha financial tracking cha TAMISEMI, lakini hiko kitengo kinapata bajeti ndogo mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anakagua kwa mfano Ulanga, tunakaguliwa kila mwaka lakini CAG wanavyokagua wanafanya random sampling yaani kama miradi 10 wanakagua miradi mitatu na wanatoa maksi kwa miradi yote kumi. Binafsi kitengo cha financial tracking kilivyokuja Ulanga kilikuta madudu sio ya kurudi nyuma. Kwa mfano tulipanga matumizi ya milioni 75 kwa ajili ya posho ya mkurugenzi ya safari lakini mkurugenzi alitumia posho shilingi milioni 192 lakini financial tracking ndio waliogundua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa Ulanga walichukua zaidi ya milioni 760 hawakuzipeleka benki na walizitumia binafsi. Ilifika kipindi watumishi wanaokusanya pesa wanaziweka kwenye akaunti zao binafsi, lakini Kitengo cha Financial Tracking ndio kilichogundua haya. Sasa mambo ambayo yalifanyika Ulanga yana-reflect halmashauri nyingine yanavyofanyika. Kwa hiyo nashauri Kitengo cha Financial Tracking cha TAMISEMI kiwezwe ili kiweze kufanya kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwa Walimu. Nimekuwa msemaji sana wa Walimu. Walimu bado wananyanyaswa mno, upandishaji wa madaraja umekuwa wa shida, wanapata manyanyaso makubwa kutoka kwa Maafisa Utumishi kwani wamekuwa wazembe katika kufuatilia taarifa za Walimu kwa ajili ya kupandishwa madaraja. Matibabu yamekuwa shida, nilishuhudia kesi moja Mwalimu amesimamishwa kazi kwa kuambiwa mtoro kwa sababu aliandikiwa ED na kituo cha afya cha private, lakini wanasema eti vituo vya afya vya private haviko kwenye standing order mbona sisi Wabunge tunatibiwa Apollo, Apollo iko kwenye standing order. Kwa mfano Dar es Salaam kuna Hospitali ya Hindu Mandal na Mwananyamala, sitojitendea haki kama nitaenda Mwananyamala nitaacha kwenda Hindu Mandal. Mbona NHIF wame-credit hivi vituo vya private, kwa hiyo Walimu wote hawa wananyanyaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye posho za Madiwani. Ukimuuliza Waziri swali hapa Bungeni atakwambia Madiwani walipwe posho kulingana na uwezo wa halmashauri lakini kila kukicha TAMISEMI wanatoa waraka...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlinga kwa mchango wako.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)