Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wote wa Wizara hii kwa kufanya kazi yao ya udhibiti wa uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa dhati na weledi pamoja na kutopelekewa fedha kama zilivyopitishwa na kuidhinishwa na Bunge kutoka Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu eneo kubwa limeathiriwa na uharibifu wa mazingira na tabianchi na kupelekea vipindi vyetu vya masika (mvua) kubadilika na mvua kuwa ndogo na mazao ya mahindi, mpunga na kadhalika kukosa maji (mvua) na kufanya uzalishaji kuwa mdogo. Mfano mwaka huu mazao yamekubwa na ukame, hivyo nashauri Serikali ijipange namna ya kukabiliana na ukosefu wa chakula nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kila Halmashauri kubaini miinuko (milima) iliyokuwa kipara yaani hakuna miti kuweka mkakati wa kupanda miti na kuweka kanuni za kulinda miinuko hiyo. Pia, kwa vile athari ni kubwa kwa nchi, ni vema bajeti ya Wizara hii katika Fungu 31 na 26, zikatolewa kwa asilimia zaidi ya 85 kwani hali ya mazingira yetu ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yasipoboreshwa kwa uharaka zaidi, lengo la maendeleo ya uchumi wa viwanda halitakuwa lenye mafanikio na endelevu kwa vizazi vijavyo. Tufanye jitihada za kufufua na kuboresha mazingira ili tupate mvua za kutosha na kupunguza athari za upepo (kuezuliwa na kubomoa majengo) ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri tupate Maafisa wa Mazingira wa kutosha ili watoe elimu na iwe elimu endelevu kwa wananchi wetu na tuwe na ushindani kwenye Halmashauri zetu. Wataalam hawa wasiwe na urasimu mkubwa wa kufikisha mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Mazingira kutokana na waliyoyaona katika utekelezaji wao wa majukumu ili kusaidia kutatua changamoto za mazingira katika maeneo yao. Tuwe na kanuni na miongozo ya kurejesha hali ya mazingira yetu kwa haraka tusiwe na urasimu? Chelewa chelewa tutakuta mazingira yameharibika kwa kiasi kikubwa na kuwa jangwa na gharama ya kuyarejesha itatushinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali tushughulikie haraka suala hili, hali ni mbaya sana. Naomba tuone umuhimu wa kuongeza bajeti yetu ndani. Pia tuweke mikakati maalum ya kupanda miti rafiki ya kulinda mazingira na vyanzo vya mito, maziwa na bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Rukwa nalo limejazwa na udongo unaoteremka kwenye milima na kushuka kwenye Bonde la Rukwa hadi kuingia Ziwa Rukwa. Hivyo nalo liko mbioni kina chake kutoweka. Naomba nalo lipewe kipaumbele ili kulinusuru na hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, suala la mazingira tuliangalie upya na kuliwekea mikakati kwani tunahitaji mazingira kwa ajili ya urithi wa vijana wetu. Naunga mkono hoja.