Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kuwapongeza sana kaka yangu Mheshimiwa January, Waziri, pamoja na Naibu Waziri kaka yangu Mheshimiwa Sima kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mambo machache sana baada ya pongezi, kwenye hotuba hii na hoja hii iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo la kwanza ambalo limeonekana kwenye vitabu vyote vitatu, kitabu cha Upinzani, kitabu cha Kamati zote mbili za Kudumu za Bunge walipoongelea fedha ambazo zimetolewa, hasa fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi hutolewa kulingana na jinsi zinavyopatikana, kwa hiyo zikipatikana then mgao unafanyika nani apate nini kulingana na majukumu ya Ofisi husika na kama ilivyooneshwa kwenye vitabu hivi bajeti ilipitishwa na sisi hasa hii sehemu ya kujenga na kufanya ukarabati wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Luthuli, Tunguu na Wete-Pemba. Tumetoa kiwango hiki cha fedha shilingi milioni
538.4 ndizo ambazo zimetolewa kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi hii, lakini ninachoomba kusema hapa ni pale ambapo vitabu vyote vimesisitiza kwamba fedha hii iliyotolewa ni fedha ya nje hakuna fedha ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kwa kusema tunatoa fedha hizi kulingana na upatikanaji wa fedha husika. Katika hili mkononi mwangu nimebeba kitabu cha hotuba ya bajeti ya Serikali nzima aliyoisoma Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Ndugu zangu tunapojadili jambo hili tusioneshe kwamba kuna mtu ambaye hapewi kwa sababu ya aina fulani ya Wizara yake, hapana. Vyanzo vya mapato vya bajeti kuu wa Serikali vimetajwa kwenye kitabu hiki. Moja ya vyanzo vya mapato kama ilivyoelezwa, tuna mapato ya ndani na tuna mapato ya nje ambayo kwenye mapato ya nje tuna misaada na mikopo nafuu, tuna misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo, tuna misaada na mikopo nafuu ya kisekta kwa hiyo tunapoongelea jambo hili tuiongelee bajeti ya Serikali kama ilivyowasilishwa na vyanzo vyake vya mapato kuliko kusema fedha za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zinapopatikana kwenye kapu, Mfuko Mkuu wa Hazina zinapoingia fedha hizi zinagawiwa kutokana na mgao ambao kwahiyo haingii akilini tunaposema kwamba huyu apewe fedha za ndani wakati tayari ana fedha za nje na Wizara nyingine haina fedha za nje, kwa hiyo kwa kuwa tu tunataka na huyu aonekane ana fedha za ndani basi tulazimishe hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliombe Bunge lako Tukufu liweze kuzingatia yanayowasilishwa na tunayoyapitisha ndani ya Bunge lako Tukufu. Hiyo ilikuwa hoja ya kwanza ambayo nilikuwa napenda kusema kuhusu mapato ya Serikali na jinsi gani tunavyoyapeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependelea kulitolea maelezo hapa ni kuhusu Akaunti ya Fedha ya Pamoja. Nakumbuka vizuri sana mwaka jana tulitoa ahadi kama Serikali kwamba jambo hili linaendelea kufanyiwa kazi. Tunafahamu, Serikali ina ngazi zake za kufanya maamuzi, tayari watalaam wetu wameshamaliza kulifanyia kazi jambo hili na sasa tulipo kikao kilifanyika tarehe 9 Februari, 2019 chini ya Mwenyekiti wa Kamati hii ambaye ni Makamu wetu wa Rais anafanya kazi nzuri sana mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli nimpongeze sana Mama Samia amesimama imara kuhakikisha Muungano wetu unakuwa imara na unaendelea kudumu tofauti na inavyowekwa hapa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba Chama cha Mapinduzi, tukumbuke ni Chama cha Mapinduzi ndicho kilichoasisi Muungano huu. Ni viongozi wa vyama hivi viwili kwa dhamira njema ya pande zote mbili za Muungano. Ndiyo maana nataka kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Makamu wa Rais. Angekuwa na moyo kama wa hao wanaotaka kupotosha Watanzania kwenye Bunge lako Tukufu tusingetoka. Serikali ina dhamira njema ya kuhakikisha jambo hili tunafika muafaka ambapo tutakapoanza kuja kwenye migao halisi sasa ya fedha hizi pande zote mbili za Muungano ziwe zimeridhika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza kaka yangu Mheshimiwa Jaku anasema, Zanzibar wakati wanaungana walikuwa wachache, hivyo Watanzania Bara wakati tunaungana tulikuwa milioni 55? Kwa hiyo tuangalie hoja hizi, base yetu ni nini ya kuleta hoja hizi. Kwa hiyo tunaposema 4.5 ni ndogo umechukua kigezo gani kusema 4.5 ni ndogo inayopelekwa Zanzibar? Kwa hiyo tarehe 9 Februari, 2019, kikao kilichofanyika hapa Dodoma maamuzi yalifanyika. Kama tulivyokuwa tuna-report siku zote kwamba Serikali inayafanyia kazi pale ambapo hatujaelewana na sasa tumeelewana na unaandaliwa Waraka wa Baraza la Mawaziri ili kwenda kufanya maamuzi ya mwisho na jambo hili liweze kufika mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kombo amesema tutoe commitment, commitment ndiyo hiyo. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kikao hili ameshaelekeza na tayari waraka umeanza kuandaliwa, anataka commitment nyingine ipi Mheshimiwa Kombo? Kwa hiyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imedhamiria kuona Muungano huu unaendelea kuwa imara, Muungano huu unaendelea kuwa na faida na pande mbili zote za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limeongelewa ni kuhusu kodi mara mbili. Nimekuwa mimi na naomba niwe shahidi ndani ya Bunge lako Tukufu, nimekuwa nikisema siku zote hakuna kodi, hakuna bidhaa yoyote inayotozwa mara mbili. Kinachotokea nimesema hapa na jambo hili ni katika mambo ambayo yapo kwenye Waraka ulioandaliwa wa Baraza la Mawaziri kwamba valuation system zetu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara siyo moja. Watalaam wetu wamemaliza kuandaa taarifa yao ya kitaalam, wameshaileta tayari inaingia kwenye Waraka huu unaoshughulikia kero za Muungano ili sasa tuweze kulitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko kwenye dunia huru ambayo tunafanya boiashara. Haiwezekani jirani yako akaingiza bidhaa kutoka kwa jirani mwingine kwa bei ya chini halafu bidhaa hiyo useme uilete nyumbani kwako ili uweze kufanya biashara. Hiyo haitowezekana, ni ngumu sana, kama kweli sisi ni Taifa moja, ni lazima tuwe na valuation system moja yenye manufaa mapana kwa Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kulikumbusha Bunge lako Tukufu hakuna maendeleo bila kodi. Lazima kodi ilipwe na lazima ilipwe katika rate zilizokubalika. Tunachikifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania tuna-adopt international system…

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tume-adopt international system ambayo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jaku kaa chini please.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tume-adopt international system, tuna international database sasa huwezi ukajifungia chumbani ukasema mimi siangalii kinachotokea duniani, mimi nataka nilinde watu wangu, unalinda watu wako ukiwa na nini mkononi? Kwa hiyo ni lazima tukubaliane na dunia inakwenda vipi, global business inakwenda vipi ili kwa pamoja tuweze kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mgao wa Mashirika ya Umma; nilijulishe Bunge lako Tukufu kama ambavyo wamesema Waheshimiwa Wabunge hapa, Benki Kuu tunapeleka na tayari tarehe Mosi Februari, 2019 tumepeleka zaidi ya shilingi bilioni 15 ambazo ulikuwa ni mgao kutoka gawiwo la Benki Kuu. Kwa Mashirika mengine yaliyosalia tunaendelea kuyafanyia kazi na ni moja ya mambo yanayoshughulikiwa kwenye kero za Muungano ili kwa pamoja Mashirika haya yaweze nayo gawiwo waliloanza kutoa, kwanza lazima, tukumbuke Mashirika haya yalikuwa hayafanyi vizuri, Serikali imefanya jitihada kubwa Mashirika haya yameanza kufanya vizuri kwa sasa tunalishughulikia ili kama linavyoingia gawiwo la Benki Kuu, moja kwa moja…

MWENYEKITI: Nakuongezea dakika moja malizia.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa hiyo tunakwenda kumalizia na mashirika mengine likiingia tu gawiwo lile kwenye Mashirika haya iende moja kwa moja asilimia 4.5 kwenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki yetu TPB; hii huwa tunagawana kulingana na hisa ulizonazo kwenye Benki hii. Kwa hiyo hili halina changamoto yoyote, limekuwa likitendeka miaka yote ya Muungano na tangu TPB Bank ilipoanza kutengeneza faida.

Mheshimiwa Mwenyekjiti, baada ya kusema haya, nirejee kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri Wizara hii na naunga mkono hoja. (Makofi)