Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Dr. Adelardus Lubango Kilangi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika kuhitimisha hoja iliyopo mezani. Nami nitajitahidi kupitia masuala kadhaa na hasa nitajikita kwa yale yaliyoibuliwa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, imezungumzwa juu ya sheria zinazodaiwa zinakiuka katiba, mifano imetolewa; Cybercrimes Act, Media Services Act, Accesses to Information Act na nyinginezo na kwamba hizi zinaingilia uhuru wa kujieleza na uhuru wa kupata habari na haki nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema tu ni kwamba masuala ya haki na uhuru yana mipaka na hii imeelezwa vizuri sana katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 30. Hata tukienda katika zile sheria za Kimataifa, kama ile International Covenants on Civil and Political Rights, tunaona Ibara ya 19 inazungumzia juu ya uwepo wa mipaka katika haki mbalimbali zilizoelezwa katika sheria hiyo. Kwa hiyo, ninachotaka kusema hapa tu ni kwamba, sheria hizi zinakuwepo, haki na uhuru vipo katika katiba lakini haki na uhuru huo una mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, linamhusu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwamba anayo mamlaka ya kutoa maelekezo ya kufanya upelelezi anapoona jambo fulani limetokea na kwamba analaumiwa hapa kwamba hajachukua hatua yoyote kwenye matukio kadhaa yaliyotokea, kwamba hakutoa maelekezo kwamba upelelezi ufanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba Mkurugenzi huyu wa Mashtaka, huwa anatoa maelekezo pafanyike upelelezi kama anaona upelelezi huo haujafanywa na chombo chochote kinachopaswa kufanya uchunguzi. Kama kuna vyombo kadhaa; kimoja au viwili au vitatu vinavyofanya uchunguzi katika jambo hilo, hana haja ya kutoa maelekezo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu lilikuwa linahusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika majukumu yake ya kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu masuala ya mikataba na kwamba pengine ofisi hii haijafanya vema katika jukumu hilo. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kweli imekuwa na changamoto za hapa na pale, lakini kwa sasa hivi maboresho makubwa yamefanyika katika ofisi ile hasa katika eneo hili la uchunguzi wa mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulilizungumza hili hata mwaka jana kwamba tumeweka hata masuala ya ubobezi katika uangalizi wa mikataba. Kwa hiyo, sasa hivi wanasheria wetu wako specialized. Kama ni mikataba ya mambo ya ujenzi, kama ni mikataba ya rasilimali, kama ni mikataba ya financing, kama ni mikataba ya manunuzi na kadhalika sasa tumeweka specializations katika ofisi ile na nafikiri ofisi inafanyakazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imeanzishwa idara maalum ambayo inahusika na kutoa ushauri pia. Kwa hiyo, kama kuna upungufu wa capacity kule kwenye idara inayohusika na mikataba hii idara nyingine inayohusika na ushauri kwa ujumla inasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne lililoelezwa katika taarifa hiyo ni kushindwa kutoa ushauri sahihi kwenye kesi mbalimbali na hasa zilizofunguliwa nje ya nchi na hadi kupelekea Serikali kupata hasara kubwa na mifano hapa imetolewa Kesi ya Konoike, kesi ya Sterling iliyokuwa inahusiana na zile ndege zetu, kesi iliyofunguliwa na ACACIAs, kesi iliyofunguliwa na Symbion, Eco energy pengine na nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kutoa taarifa kwa zile kesi mbili za kwanza, kesi ya Konoike na kesi ya Sterling, actually mashauri haya yameshamalizika, kwa sababu pia palikuwa na mazungumzo kati ya hawa wadai pamoja na Serikali. Niseme tu hapa kwamba hata fedha zilizolipwa katika mashauri haya ni ndogo sana sana sana kuliko zile ambazo zinaelezwa au zilioneshwa katika zile hukumu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika kesi ya Konoike inasemwa ilikuwa ni shilingi bilioni 80, lakini iliyolipwa ni kidogo kabisa. Kwenye kesi ya Sterling nayo ilisemwa ni zaidi ya shilingi bilioni 80 lakini iliyolipwa ni chini ya hata ya theluthi moja ya kiasi hicho kinachotajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi zile nyingine za ACACIAs, Symbion, EKOenergy zinaendelea, kwa hiyo, hatuwezi kuzizungumzia sana. Hata hivyo, hawa wahusika waliotushitaki katika kesi hizo, wao wenyewe ndio wamekuwa wa kwanza kuomba pawe na mazungumzo kati yao na Serikali. Serikali imepokea wito huo na kwa hiyo, mazungumzo yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lilikuwa ni kuhusu mkataba wa Afrika kuhusu mambo ya demokrasia, chaguzi na utawala, yaani African Charter on Democracy Elections and Governance na kwamba Tanzania haijatia saini mkataba huo; na kwamba Mataifa 35 yameshatia saini mkataba huo na kufanya sheria ya nchi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hapa kwenye hii idadi siyo sahihi. Mataifa ambayo yametia saini na kuufanya huo mkataba kuwa sehemu ya sheria za nchi zao, yaani ratification hayajazidi 11 hadi sasa hivi. Napenda tu kusema kwa haraka haraka kwamba kuna mambo kadhaa ambayo bado yanajadiliwa na yanaonekana bado ni kikwazo kwa nchi nyingi kuweza kutia saini mkataba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawili makubwa, kuna suala la unconstitutional change of government halijatafsiriwa vizuri na kuelezwa vizuri; na masuala yanayohusu uangalizi wa uchaguzi (election monitoring). Sasa nchi nyingi bado zina mashaka, nini hasa majukumu ya waangalizi wa uchaguzi na kadhalika. Kwa hiyo, siyo Tanzania peke yake na kila mara tunashauriwa kwamba nchi ichukue tahadhari ya kutosha kabla ya kuingia tu kwenye mkataba wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililoibuliwa katika taarifa hiyo ni suala la Katiba na linaingiza masuala ya Muungano. Taarifa hii kwa namna moja au nyingine inaijadili au inaizungumza Katiba ya Zanzibar na inahoji katika maeneo fulani fulani kwamba kwa nini katiba ya Zanzibar kwa mfano inamsimamo huu, haimtambui Rais kuwa ndiyo Mkuu wa nchi yote kwa Jamhuri ya Muungano, pamoja na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili niliweke vizuri kabisa. Bunge hili lina mamlaka na uwezo wa kuzungumzia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba ya Zanzibar ni ya Zanzibar na hata anayeweza kuizungumzia kwa kweli kwa mamlaka kama ninavyoweza kuizungumzia hapa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ndio anayeweza kuizungumzia authoritatively Katiba ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata likitokea shauri lolote linalogusa Katiba ya Zanzibar, shauri hilo haliwezi likafika katika Mahakama ya Rufaa ambayo ni Mahakama ya Muungano, shauri hilo litakomea katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na huo ndio utaratibu na misingi ya Kikatiba tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo ya Muungano, tunazungumza kwamba tuna changamoto. haya yote yaliyoelezwa katika ile taarifa ni changamoto za Muungano. Mpaka sasa hakuna jambo la kikatiba ambalo limebishaniwa rasmi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ipo Ibara katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vema tuwe tunaisoma kila wakati, inayosema: “kama kutakuwa na jambo linalobishaniwa kati ya Serikali hizi mbili, itaundwa Mahakama Maalum ya Katiba.” Kwa kumbukumbu zilizopo Mahakama hii haijawahi kuundwa kwa sababu hakujatokea jambo linalobishaniwa; na kwa hiyo, yaliyopo haya yote ni changamoto za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezungumzwa pia juu ya mashauri mbalimbali yaliyoko nje ya nchi, nadhani huu ni mchango wa Mheshimiwa Zitto, akazungumza juu ya kuangalia publiic intrest katika mashauri hayo na akatolea mfano wa kesi ya Standard Charterd Hong Kong; na akaeleza kuna kitu kinaitwa indemnity ambayo iliwekwa na wahahusika wa ile kampuni ya IPTL na kwamba kwa nini wasitolewe mahabusu kwa sababu waliweka ile indemnity? Sasa hapa nahitaji kueleza kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezungumzwa pia juu ya mashauri mbalimbali yaliyoko nje ya nchi, nadhani huu ni mchango wa Mheshimiwa Zitto. Amezungumza juu ya kuangalia public intrest katika mashauri hayo na akatolea mfano wa kesi ya Standard Charterd Hong Kong na akaeleza kuna kitu kinaitwa indemnity ambayo iliwekwa na wahusika wa ile kampuni ya IPTL na kwamba kwa nini wasitolewe mahabusu kwa sababu waliweka ile indemnity.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa nahitaji kueleza kidogo. Ni kweli kabisa kwamba wale watu waliopo mahabusu kuhusiana na Escrow Account katika ile kampuni ya IPTL waliweka indemnity. Hata hivyo, indemnity ile ilikuwa ni kuipa kinga Serikali iwapo litatokea shauri lolote na kutakuwa na hasara fulani au malipo fulani yanayotakiwa kufanyika, indemnity hiyo ita-cover ama hasara hiyo au malipo hayo au mahitaji yoyote yale. Kwa hiyo kimsingi indemnity inagusa masuala ya madai, ni mashauri ya madai, inagusa kwenye madai, kwamba unanipa kinga ikija kutokea shauri lolote linaibuka hapa wewe utanilipa gharama pengine za kesi, wewe utanilipa gharama pengine za kesi, wewe utalipa gharama fulani, wewe utalipa chochote nitakachotakiwa nilipe, ikiwa ni pamoja na yale ambayo mahakama mbalimbali za kimataifa zimeamuru Standard Chartered Hong Kong walipwe kimsingi wanatakiwa kulipwa kutoka kwenye indemnity hii lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Muda wetu...

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja;

MWENYEKITI: Haya, endelea.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, dakika moja tu nimalizie hapo, kwa sababu ni suala la muhimu kidogo. Indemnity hii haigusi masuala ya jinai, sasa wahusika hawa aliowataja Mheshimiwa Zitto wana kesi, wapo ndani au mahabusu kwa sababu ya kesi za jinai. Nadhani kuna mashtaka kadhaa yanayowahusu kwenye jinai hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. (Makofi)