Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ili niweze kutoa majibu ya hoja mbalimbali kutoka kwa Wabunge waliochangia kwa mdomo na maandishi katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na sheria nyingi kupitwa na wakati na kusababisha wananchi kutotendewa haki, je, ni utaratibu au mkakati gani umeweka ili kuhakikisha kuwa sheria zilizopitwa na wakati zinaandikwa kitaalam na kulingana na wakati? Hili ni swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Ritta Kabati. Jibu ni kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na sheria zinazokidhi mahitaji ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Hali hii imepelekea kuanzisha kwa Tume ya Kurekebisha Sheria mwaka 1980 kama chombo mahususi cha kupitia sheria zote ili ziweze kwenda na wakati katika kuandika na kuleta maendeleo na haki katika jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Kurekebisha Sheria katika muda wote imekuwa ikipitia sheria mara kwa mara na kutoa taarifa Serikalini juu ya maeneo ya sheria yanayohitaji maboresho. Serikali imekuwa ikitumia taarifa hizo katika kufuta sheria zilizopitwa na wakati, kurekebisha sheria zenye kasoro na kutunga sheria mpya katika maeneo mapya ambayo hayana sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine imetolewa na Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia. Anasema adhabu na faini mbalimbali zilizoko kwenye sheria zimepitwa na wakati kulingana na mazingira ya sasa. Anashauri Serikali ifanye upya mapitio ya vifungu vya faini na adhabu zinazotolewa. Majibu yanafanana na lile swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Ritta kwamba kuna jitihada za kila aina ili kuhakikisha kwamba sheria zilizopitwa na wakati pamoja na adhabu mbalimbali zinarekebishwa na Tume ya Sheria inafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni ya Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale. Anasema Tume ya Kurekebisha Sheria ifanye mapitio ya sheria mara kwa mara. Nalo hili majibu yanafanana na kama kutakuwa na ziada ya yale ambayo tumeshayatoa, tutaweza kuyajibu kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Pauline Gekul ameuliza kuhusu fidia ya wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mkoa na ya Wilaya ya Babati watalipwa lini? Jibu ni kwamba ni kweli Mahakama ilipatiwa eneo na Halmashauri ya Mji wa Babati kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama eneo ambalo lilikuwa bado halijatolewa fidia. Aidha, kati ya viwanja vinne vilivyotolewa viwanja vitatu vilishalipwa fidia. Mahakama inaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Mji kuhakiki kiasi halisi cha fidia inayodaiwa ili kuwalipa wananchi wanaohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Pauline Gekul pia amesema posho ya Wazee wa Baraza Mahakama ya Babati hawajalipwa miaka miwili iliyopita, je, wazee hawa wametapeliwa, ni lini watapewa lini fedha zao. Madeni ya Wazee wa Baraza wa Babati ni shilingi laki mia saba sitini elfu na deni hili ni sehemu ya madeni ya Wazee wa Baraza ambapo fedha imetengwa na malipo yatafanyika kabla ya Juni, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maswali yanayofanana ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mheshimiwa Joseph Haule, Mheshimiwa Ally Keisy, Mheshimiwa Pascal Haonga, Mheshimiwa Aida Khenani, Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mheshimiwa Hamoud Jumaa Kibaha na Mheshimiwa Susan Lyimo. Swali ni ni upungufu wa majengo ya Mahakama katika Jimbo la Tunduru, Mafia, Nkasi, Namtumbo na Liwale. Majibu ni haya yafuatayo, Mahakama ina upungufu mkubwa wa majengo ya Mahakama nchini katika ngazi zote. Mahakama inao mpango wa miaka mitano wa kujenga na kukarabati majengo katika ngazi zote. Mpango huu unaendelea kutekelezwa kama ilivyosemwa kwenye hotuba yangu aya ya 30 kwa kuanzia ujenzi katika makao makuu ya tarafa na baadaye kwenye kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maswali yaliyoulizwa na Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate na Mheshimiwa Joseph Haule na hili ni fupi tu linahusu upungufu wa vitendea kazi hasa magari na pikipiki. Jibu ni kwamba tunaendelea kununua vitendea kazi vya ofisi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha za Serikali na kutumia zile zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna swali limeulizwa na Mheshimiwa Hamoud Jumaa, Mbunge wa Kibaha ambalo ni kulalamikiwa kwa maamuzi ya mashauri yanayohusu migogoro ya wakulima na wafanyakazi Kibaha Vijijini. Jibu ni kwamba mfumo wa utoaji haki wa masuala ya ardhi umegawanyika katika maeneo matatu, Mabaraza ya Kata ambayo yako chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mabaraza ya Wilaya, Ardhi na Nyumba ambayo yako chini ya Wizara ya Ardhi; na Mahakama Kuu ambayo inapokea rufaa kutoka kwenye mabaraza mengine. Kazi ya Wizara yangu ni kuratibu shughuli za upatikanaji haki ikishirikiana na Mahakama na Wizara ya Ardhi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa weledi. Pale ambapo wadai hawaridhiki na uamuzi washauriwe/washawishiwe kufuata utaratibu wa rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lucia Mlowe, alizungumzia kuhusu Mahakama kutotenda haki na kufuata maelekezo ya Serikali. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uhuru wa Mahakama katika usikilizaji na utaoji wa maamuzi mbalimbali. Aidha, mfumo wa rufaa unamtaka mtu ambaye hajaridhishwa na maamuzi ya Mahakama ya chini kukata rufaa katika Mahakama ya juu. Hivyo, kama kuna mtu yeyote ambaye hajaridhika na maamuzi yoyote ya Mahakama afuate utaratibu wa kukata rufaa kwenda Mahakama ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Joseph Leonard Haule Mikumi anauliza kuhusu mishahara midogo kwa Watumishi na mikataba mibovu tunayoingia inapelekea Taifa kuingia kwenye hasara kubwa na kupelekea umaskini kwa uzembe wa kutopitia mikataba vizuri. Hili ni swali ambalo litafuata baada ya kujibu hili. Kwa sasa Serikali chini ya Bodi ya Mishahara na Maslahi ya Watumishi wanaendelea kufanyia kazi suala hili ili kurekebisha hali iliyopo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna swali linalohusu Mahakimu kupewa ulinzi. Serikali inathamini kazi ya Mahakimu wa ngazi zote za Mahakama. Hata hivyo, kwa sasa tumewahimiza Mahakimu kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Aidha, tunawashauri wananchi kushirikiana na Mahakimu ili kuondoa dosari zozote zinazoweza kuhatarisha usalama wao. Hatujapata matishio makubwa ya kuweza kuweka walinzi kwa Mahakimu wote zaidi ya 1,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie swali hili la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, CHADEMA ambapo anasema mikataba mibovu tunayoingia inapelekea Taifa kuingia kwenye hasara kubwa na kupelekea umaskini kwa uzembe wa kutopitia mikataba hii vizuri. Jibu ni kwamba uwezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa kupitia mikataba umeimarika baada ya kuanzishwa Idara Maalum inayopitia mikataba na kutoa ushauri. Pili, marekebisho ya Sheria ya Manunuzi, Kanuni ya 59 ya Kanuni za Manunuzi ya mwaka 2013 na marekebisho yake ya 2016 ambayo imeongezewa wigo hadi shilingi bilioni moja na zaidi hali iliyopelekea kupungua kwa idadi ya mikataba sambasamba na kuimarika kwa mapato. Tatu, raslimali watu inaendelea kuongezwa na kusababisha Wakili wa Serikali kupata muda wa kutosha kupitia mikataba mbalimbali kwa kina tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, hivyo uwezekano wa kuwa na mikataba mibovu kwa sasa umepungua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka anasema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina wanasheria waliobobea kwenye fani ya sheria na wanaojua jamii ya Watanzania, ni kwa nini Miswada mingi inayoletwa Bungeni kwa ajili ya kutungiwa sheria na Bunge huletwa ikiwa na mapungufu mengi ya kisheria na mengine kukosa kabisa uhalisia kiasi cha kudhani watu wanaoandaa Miswada hiyo si watu wanaotoka katika jamii yetu? Jambo hili hufanya Miswada inayoletwa Serikalini kufanyiwa marekebisho na Bunge wakati mwingine kwa asilimia 80. Hii inachangia kulifanya Bunge kutunga sheria inayodumu kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ni kwamba Miswada inayowasilishwa Bungeni na Serikali ni mapendekezo na maoni ya Serikali kuhusu kutungwa kwa sharia. Miswada hii kama ilivyopendekezwa inawasilishwa ili Bunge litekeleze jukumu lake la kufanyia uchambuzi, kujadili na hatimaye kupitisha. Mchakato wa kutunga sheria au kuchambua Miswada unajumuisha maoni ya wadau wengi ambayo yanazingatiwa katika maboresho ya Miswada hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yamekuwa mengi na mengi ya hayo yatajibiwa kwa maandishi na kutumwa kwa Waheshimiwa wanaohusika. Nakuomba nitumie nafasi na muda uliobakia kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuniwezesha leo asubuhi kuwasilisha Mpango wa Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2019/2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa namna ya pekee namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha Waheshimiwa Wabunge kushiriki na kuchangia hotuba ya Wizara yangu. Kwa namna ya pekee pia nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mwenyekiti kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hotuba yangu na kwa umahiri wako katika uendeshaji wa vikao vya leo katika Bunge hili na kwa kusimamia mjadala huu kitaalamu na vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Profesa Adelardus Lubango Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano ambao ananipa katika utekelezaji wa majukumu yangu na kipekee kwa kuungana nami katika kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala wa hotuba yangu. Nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Profesa Kabudi ambaye alikuwa Waziri kabla yangu kwa mchango wake mkubwa sana katika masuala mbalimbali ambayo yaliguswa na hotuba yangu na ameonesha ujuzi, utaalamu na ufanisi wake na nadhani mchango wake ni mkubwa na utakumbukwa sana katika kikao cha Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa maoni na ushauri ambao wanaipatia Wizara na taasisi zake katika kutekeleza majukumu yetu vizuri. Napenda nikuhakikishie wewe binafsi, Kamati yako na Waheshimiwa Wabunge wote kuwa tumepokea kwa unyenyekevu na shukrani maoni, hoja na ushauri mliotupa wakati wa mjadala wa bajeti yetu. Kwa niaba ya Wizara, tunaahidi kufanyia kazi masuala yote yaliyojitokeza katika mjadala huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani kwa wadau wa maendeleo waliochangia utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu. Wizara yangu inatambua na kuthamini mahusiano hayo. Wadau hao ni Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women), Jumuiya ya Ulaya (EU)…
WABUNGE FULANI: Mabeberu.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DfID), Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) na Shirika la Misaada ya Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID). (Makofi)
WABUNGE FULANI: Mabeberu.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Wengine ni Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kushughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu, Mfuko wa Kimataifa wa Kuhudumia Wanyamapori, Shirika la Maendeleo la Ujerumani, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shirika la Udhibiti wa Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori na Misitu, Bloomberg DHI na Shirika la Maendeleo la Italia (AICS). (Makofi)
WABUNGE FULANI: Mabeberu.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala wa hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu na katika mjadala wa hotuba ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Waheshimiwa Wabunge walitoa hoja mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine ziligusa Wizara yangu na sekta ya sheria kwa ujumla. Tumezipokea hoja zote zilizotolewa na tunaahidi kuzifanyia kazi na kuleta mrejesho hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuongea na wale waliochangia kwa maandishi na kuchambua Bajeti yetu kwa kina. Michango yenu ni nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji kazi wa Wizara na taasisi zake ili Sekta ya Sheria ikidhi matarajio ya Watanzania na iwe na mchango chanya katika maendeleo yao ya jamii, kisiasa na kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Wabunge waliochangia hotuba yetu, Wabunge 17 wamechangia kwa maandishi na Wabunge nane (8) wamechangia kwa kuzungumza. Kati ya wale waliozungumza mchana huu walitoa hoja nzuri na kubwa tutayajibu kwa maandishi ili tuwe na ufasaha zaidi katika kujibu maswali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa uniruhusu nianze kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa. Nadhani hapa maandishi yamekorofisha.
MWENYEKITI: Eeeh, umalizie. Malizia kwa kutoa hoja tu. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema naomba rasilimaliwatu tuiboreshe, lakini ninawashukuru wafanyakazi walionisaidia kujibu maswali haya kwa muda mfupi ambayo mmeyauliza na nina hakika majibu ambayo mtayapata kwa maandishi yatakuwa ni sahihi zaidi kuliko ambayo mmeyapata hapa kutoka kwangu. Ahsanteni sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, toa hoja.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.