Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu. Kwa upande wangu, mara nyingi nasema Wizara hii ya Utamaduni ni Wizara mama ya Wizara zote ambazo zipo kwa sababu ndiyo Wizara ambayo inajenga misingi ya utaifa wetu ikiwemo uzalendo, maadili, udugu, mshikamano na ujamaa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kweli niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote akiwepo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya ili kuweza kufikia malengo ya maendeleo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujikita sehemu kubwa moja ambayo kwa kweli bila kukumbushana maendeleo yote tunayoyapanga, bajeti yote tunayoipitisha katika Taifa letu haitaweza kufikiwa kama Watanzania leo hatutakuwa kitu kimoja na wazalendo katika nchi yetu. Tumeona mifano mingi ambayo inaendelea katika Taifa letu ambayo kwa kweli uzalendo wetu tusipoendelea kujikumbusha nchi hii itagawanyika katika misingi ya ukabila, udini, vyama vingi na kadhalika na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi dunia tunaona imeingia katika crisis ya uchumi, kwa hiyo, kila mtu anatafuta namna ya kumtawala mwingine ili aweze kupata masoko na kujua rasilimali zitatoka wapi. Watanzania tusipokuwa na mshikamano katika uzalendo na utaifa wetu kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kwa kazi anazozifanya hatutaweza kufikia maendeleo hata tungekuwa na Wizara ngapi au bajeti kubwa kiasi gani. Kwa sababu uzalendo ndiyo ambao unasema Taifa kwanza halafu mimi baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niombe kwamba fedha zote walizoomba Wizara hii wapewe lakini pia hata zile zilizobaki za 2017/2018 wapewe katika misingi niliyoisema ya umuhimu wa Wizara hii. Kwa nini nasema hivi? Kwa mfano, katika katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 18, item ya 31 na ukurasa 24, item ya 42 amezungumzia suala la uzalendo. Sasa uzalendo maana kama nilivyosema nchi kwanza mengine baadaye, tumeona sasa hivi nchi inaweza ikawa na amani na utulivu lakini bila uzalendo maana yake rasilimali za nchi hazitatumika kwa tija ya Taifa zitatumika kwa mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nisisitize kwamba katika nchi yetu kuna vipengele vya uzalendo. Vijana wengi sasa hivi wamechukua madaraka lakini wamezaliwa katika kipindi cha mageuzi, miaka ya 80 kuja mbele wakakutana na sera za ubinafsishaji, vyama vingi, haki za binadamu, kwa hiyo, kama alitoka kwenye familia ya ufisadi na uhujumu anachokijua ni hiko. Kwa hiyo, Wizara hii ina jukumu kubwa kushughulikia suala hili. Mlizindua Kampeni ya Uzalendo nafikiri 2017, nilikuwa nategemea katika ripoti yenu hiki kipengele jinsi ya kuwalea hawa vijana kuanzia mtu anapozaliwa, uzalendo ndugu zangu unazaliwa, unakua na unaweza ukafa. Kwa hiyo, lazima tulinde misingi ya uzalendo ambayo waasisi wetu walituwekea. (Makofi)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Tisekwa kuna taarifa, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa Daktari kwa kile anachokichangia na mimi namuunga mkono. Hata hivyo, nataka kumwambia uzalendo unaanzia kwenye nyumba hii hii ambayo ndiyo tunatunga sheria. Kwa hiyo, nakubaliana naye kwamba uzalendo unaanzia humu ndani ndiyo utafika nje. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru anatambua kwamba wote tunatakiwa tuwe wazalendo kuanzia kwenye nyumba hii. Pale tunapotunga sheria wote tukae ndani ya nyumba hii tutunge sheria, tunapopitisha bajeti wote tukae tupitishe bajeti kwa umoja wetu kwamba ndani ya nyumba hii hoja ndiyo zishike mshiko na siyo vitendo vya kususa na kadhalika. Kwa hiyo, nashukuru kwa kulitambua hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme kwamba kuna Tunu zetu za Taifa ambazo zimejenga uzalendo nchi hii. Kwa mfano, Uhuru, Muungano na Mwenge wa Uhuru. Hivi vitu lazima watoto wetu wanapozaliwa, kama nilivyosema uzalendo toka mtu anapozaliwa kwa sababu unazaliwa na unakua, hizi tunu tunatakiwa tuzienzi lakini leo hii Uhuru, Muungano na Mwenge wa nchi hii unaonekana kama wa chama fulani. Kuna wenzetu bado wanadai Uhuru, kuna watu ambao wanataka Muungano uvunjike, kuna watu ambao wanataka Mwenge wa Uhuru usitishwe lakini hivi vitu vimebeba philosophy kubwa ya mshikamano, udugu, utaifa wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nashauri Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri nyingine Mwenge wa Uhuru uheshimiwe kitaifa, bajeti yake iende kwenye Taifa isiwe sasa kuomba kama ilivyo sasa kwa sababu tunapoomba watu wanafikiri labda hii ni ya kichama lakini ndani ya Mwenge wa Uhuru ndiyo tunasema imulike, ilete amani, upendo na umoja. Kwa hiyo, naomba Kampeni hii ya Uzalendo mwende kule chini kuanzia chekechea mpaka vyuo vikuu tujenge taifa la uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema hayo kwa mfano sasa hivi, Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kuna miradi hii mikubwa, mimi nimesomea maendeleo, kuna stimulus za maendeleo ambazo ni usafiri wa uhakika lakini pia energy (umeme) wa uhakika. Nachukulia mfano hii Stigler’s Gorge, kwanza neno Stigler lenyewe limetoka wapi, huyu ni mkoloni, upembuzi yakinifu wa hii Stigle’rs Gorge ilifanywa toka wakati wa ukoloni na walikubali. Je, hili bwawa kwa mfano lingejengwa wakati wa ukoloni haya masuala ya mazingira wangeyazungumza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika Awamu hii ya Tano hii Stigler’s hakuianza yeye ni strategic plan ya miaka toka ya ukoloni, ndugu zangu tuwe wazalendo. Ulaya na Amerika wameharibu mazingira kiasi gani? Leo umeme tunalipa senti 12 wenzetu wanalipa senti 0.0 something, hivi hatuoni? Kwa hiyo, suala la uzalendo ni muhimu sana kulijenga katika nchi yetu, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa maendeleo ya nchi yetu, tusipokuwa wazalendo tutakuwa wabinafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimejikita kwenye sekta ya uzalendo na utaifa. Uzalendo hauwezi ukaja kwa kuzungumza lakini nachotaka kuzungumza pia rushwa, ufisadi, uonevu, dhuluma, hivi vyote vinamong’onyoa msingi wa uzalendo. Kwa hiyo, wenzetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Daktari, muda wako umekwisha.

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, oooh, naunga mkono hoja. (Makofi)