Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, nasimama hapa kuiunga mkono Serikali, kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote walioko katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yako mengi na muda ni mchache katika hotuba hii. Mimi nitajielekeza katika sekta ya michezo lakini pia sanaa. Mwaka huu umekuwa ni wa Taifa la Tanzania kwa mafanikio katika sekta ya michezo na hasa soka pamoja na tasnia ya sanaa. Wote tumeshuhudia tokea mwaka jana wakati ambapo Bunge lako Tukufu lilivyokwenda kushiriki Mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kule Bujumbura, Burundi, wachezaji wako wa timu ya Bunge Sports Club wakijumuisha michezo mbalimbali walishiriki kwa ufanisi mkubwa sana. Tumepata medali nyingi za kumwaga za Dhahabu, Fedha na nyingine ambazo zilikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kusema tu ni kwamba yote hii imetokana na maandalizi mazuri. Kwa nafasi ya Bunge Sports Club tunampongeza sana Mheshimiwa Naibu Spika, wewe Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati na Wabunge wote kwa ujumla kwa namna ambavyo mmekuwa mkiunga mkono sekta hii na sisi ndiyo wasimamizi wa sheria zinazohusisha mambo ya michezo, sanaa na mambo mengine. Kwa hivi tumetembea katika maneno yetu na tumeonyesha kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na tunampongeza sana Mheshimiwa Spika. Ndiyo maana hata leo asubuhi wakati anasimamia session ya maswali na majibu ametoa taarifa kwa Watanzania kupitia Bunge hili Tukufu kwamba tarehe 26 Aprili, tutakuwa na mechi ya kirafiki kati ya Bunge Sports Club kwa football na netball pamoja na Baraza la Wawakilishi, ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ushiriki wetu si wa kupoteza muda kwa sababu tunatumia fedha za Serikali lakini pia zinatupa fursa sisi kama Taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujua na kufanya itifaki ama kufanya utafiti kwa yale ambayo yanatuhusu kwa manufaa ya Taifa letu. Kupitia hili dirisha la ushiriki wetu naamini kwamba Serikali kimkakati inaweza kujua kinachotokea kwenye nyumba za jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitazungumza kwa maneno mengi lakini nayafahamu Watanzania na hasa wanaoshiriki katika mambo yao kusimamia maeneo haya wanajua namaanisha nini. Ukijua kwa jirani kunatokea nini ni rahisi sana kujipanga na kujua kesho kutakuwaje kwa manufaa ya Taifa letu, kwa hivi tuendelee kuuunga mkono ushiriki wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili naipongeza sana Timu ya Taifa, mmefanya kazi kubwa Mheshimiwa Waziri Mwakyembe, Daktari na Mwalimu wetu pamoja na wenzako mmefanya jambo kubwa. Ni miaka 39 imepita tangu tushiriki Mashindano ya Fainali za AFCON mwaka huu tunakwenda kushiriki. Ni jambo jema sana, hatujafikia hapa kwa bahati mbaya ni kwa sababu ya maandalizi. Tumeona ushiriki wa Serikali na hata Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa hamasa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake, wananchi kwa ujumla na sisi kama Bunge tukiwa sehemu ya wahamasishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda fainali lakini fainali hizi zimechagizwa sana na ushindi wa Simba uliopatikana katika ushiriki wa Klabu Bingwa ya Afrika. Wote tunafahamu kwamba Simba imefikia kuingia hatua ya robo fainali, kuanzia ushiriki wa Mashindano haya Klabu Bingwa Afrika kwa ligi ya mwaka 2021 Tanzania kwa hatua iliyofikiwa na Simba Sports Club tunakwenda kuingiza timu nne; Kombe la Shirikisho zitakwenda timu mbili na Kombe la Klabu Bingwa zitakwenda timu mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Ushabiki pembeni ukweli ni kwamba kama Taifa tunatembea vizuri. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe na safu yako. Kwa ushiriki wa Simba tumepata pointi 15 kujumlisha na tatu ambazo Yanga aliziweka katika ushiriki wake wa miaka mitano, tumepata kile kigezo ambacho kinatuwezesha kuingia kwenye timu 12 na sasa tunapata ruksa ya kushirikisha timu nne katika mashindano haya makubwa, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kupata fursa hiyo tunakwenda kutangaza Taifa letu. Wachezaji wetu wanajitangaza, Mbwana Samata Samata alikuwa mchezaji wa Timu ya Taifa kabla hajakwenda TP Mazembe pale na sasa hivi anacheza katika ligi ya nchi ambayo kwa vigezo vya ubora wa soka duniani, Ubelgiji ndiyo timu ya kwanza kwa ubora wa viwango vya FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna mchezaji anatoka Tanzania Mbwana Samata aliyewahi kukipiga katika Soka la Simba Sport Club na baadaye akaenda kule TP Mazembe, huyu ni mchezaji anayecheza ligi katika nchi ambayo kwa viwango ni FIFA namba moja duniani. Si jambo dogo na ni mfungaji bora anaongoza ana magoli 21 kwenye ligi, wapo akina Msuva na wapo wengi wanakuja. Kwa hiyo, ushiriki wa timu zetu nne utakwenda kuleta faida kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nataka kusema tunakwenda kwa sababu Serikali, wadau na sekta binafsi zinashiriki. Jambo langu ambalo nataka kulipendekeza kwa Serikali na hasa kupitia kwa Waziri mhusika hapa ni kwamba tuimarishe sana Sports Academy. Watu wote hatuwezi kuwa Wabunge, ma-engineer, walimu au kusoma mpaka vyuo vikuu, hizi ni fursa kwa manufaa ya Watanzania. Tujenge Sports Academy nyingi na ikiwezekana tujenge Sports Academy Kikanda na pale Sengerema tuna uwanja mkubwa sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu nilishamuomba na nishaiomba Serikali, tutakapofikia hatua hiyo kama Serikali itaridhia utaratibu huo, niiombe sana Serikali ije pale Sengerema ijenge Sports Academy kwa maana ya Kanda ya Ziwa, tutapeleka zingine Kanda mbalimbali lengo lake ni kujenga fursa kwa ajili ya kuendeleza michezo na ni jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naishauri Serikali, sasa tunahitaji kufungamanisha sekta ya michezo na hamasa tunayoiona pamoja na uchumi wake. Dunia nzima imeshuhudia na sisi wote ni mashahidi kwamba mataifa makubwa kiuchumi duniani yanawekeza pia katika michezo. Miaka 30 iliyopita Marekani ambalo ni taifa kubwa kiuchumi duniani lilikuwa halijajielekeza sana katika michezo lakini kuanzia mwaka 1994 waliibuka sasa na kuanza kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia hasa soka na hata michezo mingine. Nachotaka kusema sisi tufungamanishe uchumi wetu, kama tunasema uchumi wetu sasa unakua kwa kasi na tuko katika miongoni mwa nchi tano Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ni lazima i-reflect katika kuendeleza sekta za michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia uchumi mkubwa hapa Afrika, South Africa, Nigeria, Egypt, wote wanafanya vizuri katika michezo. Kwa hiyo, tusibaki nyuma katika hilo na sisi ni ma-giant watarajiwa katika uchumi wa Afrika, tutumie nafsi hii ku-link uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watu wengi maarufu (celebrities), leo ukingia madukani pale New York City, utakuta majina ya Watanzania wamejifungamanisha kupitia shughuli za kibiashara na makampuni makubwa ya design. Wapo akina Flaviana Matata, Happiness Magesa (MiIlen), wapo Watanzania wengi. Leo tunao akina Diamond, Rayvan, Ally Kiba, hawa tunahitaji kuwafungamanisha wakashirikiana na sekta ya utalii naamini kwamba tunaweza kuendeleza vizuri sana sekta ya utalii na kufungua fursa kwa Watanzania wengi na hatimaye tukafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye mafanikio hapakosi challenges na nafahamu katika hili yako mambo ambayo tunaweza kufanya vizuri kwa sababu ya hamasa tu. Nataka nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mhamasishaji na Msemaji Mkuu wa Simba Sports Club, mtani wetu, Ndugu Haji Sunday Manara, amekuwa ni kigezo ni kielelezo mpaka FIFA wamemtambua. Juzi nimeona hata Instagram amefikisha followers zaidi ya milioni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Simba Sports kwa miaka imekuwa ndiyo timu pekee ambayo inaujaza Uwanja wa Taifa kwa kuingiza zaidi ya watu 60,000 kwa kiingilio. Maana yake ni nini? Tunahitaji kuhamasishana kama Taifa tusimame pamoja. Nafahamu wako wasemaji wa vilabu vikubwa hapa Tanzania, wao wanacheza kwenye Blog tu, lakini huwezi kuwasikia lakini michezo hii inahitaji kusema na kusikika. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Msemaji wa Bunge Sports. (Kicheko)

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachoomba Watanzania tusimame kwa ujumla wetu, tuhamasishe michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mahali fulani kwamba baadhi ya mambo yaliyosababisha makusanyo yakawa machache katika Wizara hii ni pamoja na kuonyeshwa michezo hii live kwenye television na kwenye App. Nasema kama Simba waliweza kuujaza uwanja na hii michezo inaonyeshwa kwenye television kwa nini tusihamasishane kama Taifa, tutumie hiyo fursa watu kuonyeshwa hii michezo live isiwe kigezo cha kupunguza mapato yetu kwa sababu tunao sisi kama Taifa kupitia Simba Sports Club. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Watanzania tutumie huu uzoefu ambao tumeupata kutoka kwa Msemaji wa Simba Sports Club, Ndugu Haji Sunday Manara tuupeleke sasa katika level ya kitaifa zaidi. Naamini kwa kufanya vile Taifa litaendelea kunufaika na fursa zinazojitokeza katika michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimalizie jambo moja, tuna Television ya Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)