Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii adhimu ya kuchangia katika Bunge hili. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imegusa katika Kiswahili na ili tuweze kuenzi Kiswahili hiki, nakumbushia, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wajaribu kutazama michezo ambayo inakuza Kiswahili chetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna tabia ya michezo kutafsiriwa, sisi tuna mila zetu na tuna Kiswahili chetu, mchezo kama unatafsiriwa Kiswahili bora ukaonyeshwe huko nchi nyingine ili Kiswahili kienee. Siyo mchezo unatafsriwa Kiswahili hapa kwetu, haiwezi kuchangia kitu. Hilo moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, alisimama hapa mtu mmoja akazungumza Mheshimiwa Khatib, Mheshimiwa Khatib, najua amezungumza hivyo ili anichafulie katika uteuzi katika chama changu. Kwa sababu najua yeye hana wasiwasi kwenye uteuzi, kwa sababu Mheshimiwa Khatibu ni pete na Maalim ni chanda. Kwa hiyo, najua tu kwamba yeye atachaguliwa na hilo jambo linajulikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anasema mimi naimba taarab, ni sawa, na starehe kwa mwenye kuimba, taarab inazungumzia sana mapenzi na mapenzi mara nyingi yanakuwa ni baina ya jinsia mbili, mwanamke na mwanamume, mwenzangu yeye hana hilo, hata mke hana! Sasa siwezi kujua kwamba yeye ana kitu gani maana… (Kicheko)[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ali King, hayo ya kutokuwa na mke mwachie yeye mwenyewe kama anayo. Kwa hiyo, hebu endelea na mchango wako, ondoa hayo maneno ya yeye kutokuwa na mke. (Makelele)
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, na yule aliyesimama namjua vizuri tu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ali King, kuna taarifa, Mheshimiwa Juma!
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Ally King ya kistaarabu tu Mheshimiwa ana mke na ana watoto sita, mke wake yuko Tanga, familia yake iko Tanga, kwa hiyo, suala la kwamba Mheshimiwa Khatibu hana mke hili Mheshimiwa Ally King siyo la kweli kabisa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa AlI King, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hii taarifa, ni sawasawa na mchicha wenye miiba lakini huliwa! (Kicheko/Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ali King hebu ondoa hayo maneno yako ya mwisho hapo. (Kicheko)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, naondoa haya maneno.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye michango ya Bunge hili kama watu watakumbuka hoja ya umeme kwenye VAT, hilo lilizungumzwa, kazungumza Mheshimiwa Saada Mkuya nimezungumza mimi, kule hakujakuwepo mtu hata mchango wake. Hoja ya VAT ya bidhaa zinazokwenda Zanzibar, zinazotengenezwa Zanzibar kuja bara, hakuna mbunge aliyeweza kulizungumza hilo nililolizungumza mimi. Sasa hii kupiga makelele, kujikamua na kujidhihirisha ile tabia yake ambayo anayo, hicho siyo kitu ambacho labda kila mmoja anaweza akafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nimshauri tu Mheshimiwa Khatibu, sie tushamjua na vijana huko nje wanapata taabu sana, waosha magari, tunajua! (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba ajaribu kueleza vitu ambavyo viko kweli. Kwenye masuala ya Muungano sisi Wabunge wa CCM ndiyo tuliozungumzia sana, nami nina hoja nyingi sana ambazo nikiziweka hapa mezani, watu watajua nini nimechangia katika Bunge hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Khatib mimi namwambia hiki kitu aache, mimi muimbaji taarab sawa, lakini yeye asitumie mic nyingine atumie mic ileile ambayo mimi naimbia taarab. Sasa hii mimi napenda kumwambia kitu hiki. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninachopenda kuchangia katika Bunge hili, tuanze kuandaa vijana vizuri kwa michezo! Michezo, tukiandaa vijana vizuri, timu zetu zitaenda mbele! Watanzania tutakuwa tuna furaha, tusiwe na programmes hizi za zimamoto. Juzi tulifurahi kidogo tatizo tulifungwa na hata siku ile ambayo Simba amefungwa nne, Yanga walifurahi lakini Simba tulinuna, lakini sasa tukiwa na timu zilizoandaliwa itakuwa ni vizuri, kwa nini tusiwe na academy. Academies zipo lakini za watu binafsi!
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko taasisi zinao uwezo wa kuhamasishwa hata hizi nyingine, zikaandaa hizo programmes kwa sababu sasa hivi michezo ni uwekezaji, leo tukiwa tuna wanamichezo 20 wanacheza ligi za nje, watachangia katika mapato ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa mia, Wizara ya Michezo izingatie haya ambayo nimeyazungumza. (Makofi)