Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha sote salama. Mimi nitachangia mambo matatu. Kwanza, nitazungumzia kwa ufupi sana maandalizi ya Timu ya Taifa, TBC na FIFA, ZDFA na TFF na muda ukiruhusu nitazungumzia kwa ufupi sana suala la uhuru wa habari.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu wake na watendaji wote wa Wizara. Kwa namna ya pekee nimpongeze sana Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu, dada yangu Fisoo na niwapongeze pia wasanii wote wa Tanzania, wanafanya kazi nzuri na wanafanya kazi kubwa kwa sababu kazi ya usanii ni ngumu sana na inahitaji ubunifu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ni Shirika la Umma lakini bila kuwezeshwa kuwa ni mitambo ya kisasa usikivu wake hauko vizuri sana. Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, nashukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa siku za karibuni imeonesha kujali Shirika hili lakini yapo maeneo haisikiki vizuri. Hata kwako kule Kongwa yapo baadhi ya maeneo haisikiki vizuri, hata kule Chemba lakini pengine nadhani Serikali ikihakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinakwenda itasaidia zaidi TBC kusikika na kuonekana vizuri. Hata hapa Dodoma ule mtambo hauko vizuri, kwa hiyo, hata maeneo ya kwetu kule Chemba, Kondoa, Singida wakati mwingine ni tabu kusikika. Kwa hiyo, nadhani ni vizuri jambo hili Serikali ikalitilia mkazo na kuangalia pia maslahi ya wafanyakazi wa TBC, nadhani baada ya siku Shirika hili litasimama kwa miguu yake yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, naomba nizungumzie maandalizi ya Timu zetu za Taifa. Ni aibu sana na lazima tukubali kama Taifa kwamba huwezi kuandaa mashindano halafu ukashika nafasi ya mwisho. Huwa inatokea mara chache sana, hata Korea walipoandaa Kombe la Dunia waliishia robo fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kama kuna vitu ambavyo vilinishangaza ni kuona Kamati inasema vijana wale wakichukua ubingwa wanawapa magari na shilingi milioni 20. Ni sawasawa na mtoto wako wa miaka 8 ana birthday unamwambia nitakununulia gari. Kwa hiyo, kuna mahali tulipwaya kidogo na pia hatukuiandaa timu hii vizuri kwa sababu hata mashindano iliyokuwa inakwenda kwa trials ilikuwa ni bonanza. Wamekwenda Rwanda kwenye bonanza, wakaenda wapi sijui kule kwenye bonanza hatukuwaandaa vizuri. Kwa hiyo, nadhani ni vizuri sasa tuangalie in future tunawaandaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuwaangalie wachezaji hawa wanapatikana vipi kwa sababu nikiangalia ile timu ilikuwa ina wachezaji nane (8) wanatoka timu moja ya Alliance ambayo inashika karibu nafasi ya sita (6) kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kwa hiyo, kuna tatizo hilo, nafikiri tuangalie namna gani tunaweza kuwapata vizuri.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Timu yetu ya Taifa ya Taifa Stars inakwenda kwenye michezo ya AFCON Cairo na michezo hii imesogezwa mbele tu kupisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao unatarajiwa kuanza tarehe 5. Mwezi ukiisha maana yake ni kwamba tunaenda kwenye mashindano, lazima tujiandae vizuri sasa. Tusipojiandaa vizuri tunaweza kwenda kushika mkia kwenye lile kundi, Mungu pisha mbali lakini kwa kweli lazima tujiandae vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo limekuwa likijitokeza sana ndani ya Bunge mwaka nenda miaka rudi, tangu mimi nimeingia ndani ya Bunge hapa 2010 linazungumzwa nalo ni suala la Zanzibar kuwa mwanachama wa FIFA. Kwa mujibu wa United Nation Resolution No.25, Zanzibar is not a sovereign state. FIFA inatambua sovereign state except Wales, Scotland, England na Ireland ambazo ni founder wa FIFA.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Zipo nyingi.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nenda karejee kesi iliyoamuliwa katika Mahakama ya Rufaa ya Khamis Machano. Nadhani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikae na Serikali ya Zanzibar kwa sababu nayo hii isiwe kama kero ya Muungano, Tanzania Olympic (TOC) ina mwakilishi kutoka Zanzibar ambaye kwa sasa ndiye Rais wa TOC.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ipo haja kwenye nafasi za Makamu wa Rais wa TFF mmoja akatoka Zanzibar ili kuondoa hii hali ambayo kila siku inatokea humu lakini Zanzibar kuwa mwanachama wa FIFA ni jambo gumu. (Makofi)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, tarehe 16 Juni, 2011, Timu Maalum ya Zanzibar iliyokwenda FIFA iliandikiwa barua na aliyekuwa Katibu Mkuu wakati ule Bwana Volker kwamba Zanzibar is not a sovereign state, kwa hiyo haiwezi kuwa mwanachama wa FIFA, ni suala la busara tu.

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Ally Saleh.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumwarifu kwamba kwa mujibu wa FIFA mbali ya zile nchi wanachama za awali alizozitaja lakini pia kuna nchi ambazo sio sovereign state kama Macau, Hong Kong na nyingine pia ni wanachama wa FIFA kwa sababu nyinginezo. Uanachama wa FIFA hauko-based or sovereign state tu.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ally, namheshimu sana, tumefanya naye kazi BBC na alikuwa anakaa kwangu. (Kicheko)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, pia ni rafiki yangu, kuna tofauti kubwa sana unapoizungumzia Macau…

SPIKA: Mheshimiwa Ally Saleh unabisha hilo? (Kicheko)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, sijawahi kukaa kwake. (Kicheko)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, Hong Kong, Macau siyo permanent member wa FIFA, kwa hiyo, asipotoshe Bunge. Taarifa yako nimeipokea lakini siyo sahihi na kwa sababu ni rafiki tunaheshimiana hakuna sababu ya kugombana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani hilo jambo ipo haja kwa Serikali kutumia busara.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, hata Mheshimiwa Ally Saleh anafahamu hakuna nchi isiyokuwa na sheria. Huwezi kusimama tu unasema mimi kwa sababu ni mwandishi wa habari nitukane kwa sababu kuna uhuru wa habari, hakuna. Hata huko kwa wakubwa Mheshimiwa Ally Saleh wewe shahidi hakuna mtu anaweza kuandika tu akatukana Serikali au akatukana Kiongozi yeyote kwa sababu tu kuna uhuru wa vyombo vya habari, uhuru una mipaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani. Leo ni kweli yapo baadhi ya magazeti yanaandika vitu vya ajabu sana and the Government is quiet. Sasa upande wa pili kule wanasema hili Gazeti la Tanzanite… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kama ni msumeno ukate kotekote. Hilo gazeti unalosema la Tanzania Daima nalo ni moja kati ya magazeti ya ovyo sana katika nchi hii na ninashangaa linaachwa. La ovyo sana na mmiliki wake yuko humu humu ndani, rafiki yangu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Nani?

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, siwezi kumtaja, lakini yupo humu ndani na anasikia. kama hajasikia atapigiwa simu. Lazima tufike wakati kama Taifa, sheria za nchi ziheshimike. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili, Mheshimiwa Nkamia.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, jamaa alinikata pale.

SPIKA: Muda hauko upande wako.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)