Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kuongelea kuhusu viwanja vya michezo. Kulingana na changamoto za viwanja vingi nchini kuwa chakavu, jambo hili linatakiwa kupewa kipaumbele na Wizara ili kuweza kukuza michezo katika ngazi mbalimbali nchini na pia italeta chachu kwa vijana wenye vipaji mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kuhusu kuboresha usikivu. Kwa sasa kuna shida kubwa ya usikivu wa chaneli zetu, hasa kwenye maeneo ya mipakani. Naomba maboresho yafanyike ili kuwasaidia wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kupata habari za taifa lao badala ya kupata habari za nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, tatu ni usalama wa waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari. Kwa sasa kumekuwa na vitisho na watu kupotea, je, Wizara ina mkakati gani wa kuwalinda kwani kuwepo kwa waandishi wa habari ni muhimu sana katika taifa lolote lile.

Mheshimiwa Spika, nne, vazi la taifa. Mpaka sasa vazi la taifa halijajulikana na imekuwa ni malalamiko ya muda mrefu kwa wananchi katika ngazi mbalimbali nchini kuhusu vazi hili. Je, Wizara mpaka sasa imefikia hatua gani kuhusu vazi la taifa?

Mheshimiwa Spika, tano, chuo kikuu kwa ajili ya walimu wa michezo. Nashauri kijengwe chuo kikuu cha walimu wa michezo ili kuweza kukuza michezo nchini kwani kwa sasa kuna uhaba wa walimu bora wa michezo. Hii pia itasaidia kuinua michezo nchini.

Mheshimiwa Spika, sita, wanamichezo wanaofanya vizuri ndani na nje ya nchi. Kumekuwa na malalamiko kwa kiasi wanachopewa baada ya ushindi kwamba wanapewa kiasi kidogo sana ambacho hakiendani na kiasi walichopata, jambo ambalo linapunguza morali kwa wanamichezo wetu.

Mheshimiwa Spika, saba, nashauri Wizara iweke utaratibu mzuri wa kuibua vipaji mbalimbali kuanzia huko wilayani na mikoani ndani ya nchi yetu. Ni imani yangu kuwa wilayani na mikoani kuna vipaji vingi.

Mheshimiwa Spika, nane, kufungia magazeti. Suala hili limekuwa likileta sura mbaya kwa mataifa mengine yanayotuzunguka. Suala la kufungia magazeti linaathiri wamiliki, waajiriwa pamoja na wananchi wanaopata habari ambayo ni haki yao.