Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru sana kupata nafasi hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia uhai kufika hapa leo kuchangia bajeti hii ya Taifa. Pia nakushukuru na wewe kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze na pongezi na shukrani kwa Wizara ya Mambo ya Ndani. Shukrani zangu, mwaka 2018 nilikuja hapa nikasikitika kwamba kuna familia 120 ambazo zina wakazi au zina watu ambao wanafikia 480 walikuwa wakitumia choo kimoja. Hivi sasa Jeshi la Polisi kule Ziwani, Jimboni kwangu Jang’ombe tayari kuna choo kinajengwa na sasa hivi kipo katika hatua za mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali ni kwamba kuna choo pale cha zamani cha tokea Mkoloni mimi nimeanza kukikarabati pale, tumeshaingiza fedha kadhaa, lakini tumekwama katikati. Hata kama tukipata shilingi milioni mbili hivi au tatu, basi tunaweza tukatengeneza kile choo kikachangia pale kikaweza kuondoa matatizo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hili nalitupa kwake, nikipata fedha hizo kile choo kitamalizika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine, nizungumze kwa Wabunge wenzangu kwamba kuna msemo unasema, “asiyelijua chozi, amtazame aliaye.” Kuna msanii mmoja Marehemu John Komba alisema kwamba, “amani duniani imetoweka na pia Afrika imetoweka”; lakini kumbe Tanzania imejichimbia na kama hujui hayo, kaangalie Kongo. Kama hujui kufa, kaangalie Somalia.
Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu hii, ukiona vyaelea, basi ujue vimeundwa, amani iliyokuwepo ni kwa sababu ya mifumo ya kazi ya majeshi yetu ambayo yanafanya kazi ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuyapongeza majeshi yetu yote ambapo sasa hivi sisi tuko katika amani na usalama.
Kwa hiyo, kama kuna watu ambao waliwahi kubeza, wasifanye hicho kitu kwa sababu siyo kitu kizuri na wale ambao wanataka kutulizia ndege mbaya, washindwe na walegee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vote 28 - Jeshi la Polisi huwa mara nyingi linafanya kazi zake kwa kutegemea taarifa na mara nyingi mawasiliano ndiyo kitu muhimu kinachowezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi. Sasa nilivyoangalia randama na kitabu hiki cha bajeti, pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Waziri, nikagundua sub-vote 2036 ambayo iko katika mkoa wangu wa mjini kuna kifungu 22012 ambacho kinaelezea communication and information. Kifungu hiki kinahusiana na mambo ya mawasiliano ya simu pengine na mambo ya masunduku ya barua.
Mheshimiwa Spika, kwenye sub-vote hii ya Mjini Magharibi, kule hakuna hata senti tano: Je, kule Jeshi litafanya kazi vipi? Nikadhani labda zimewekwa Makao Makuu, nikaenda katika sub-vote 2005 ambayo ni Polisi Zanzibar. Kuangalia pale nikakuta zimewekwa shilingi 180,000/
= na hizi ni kwa ajili ya kulipia masunduku ya posta. Sasa nilikuwa najiuliza: Je, Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Mjini tunakoishi sisi pale, litafanya kazi zake vipi bila kuwa na vitu hivi vya mawasiliano? Watafanya kazi vipi?
Mheshimiwa Spika, nilipoangalia maeneo mengine kwenye mikoa mingine kama Kusini, Kaskazini, nimegundua kila sehemu kumewekwa shilingi 15,600,000/=, huku kwetu Mjini Magharibi, hakuna kitu. Nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, aniambie sisi tutafanya kazi vipi pale Mjini Magharibi? Aje anipe ufafanuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nililiomba katika bajeti iliyopita, nilisema kuna jengo la Kilimanjaro, Ziwani Polisi. Jengo lile liko katika hali mbaya na wakati wowote linaweza likaleta madhara kwa wakazi wa jengo lile. Familia zinazokaa pale zinaweza zikaadhirika. Serikali jambo hili hawajalichukua.
Mheshimiwa Spika, nimeenda kuangalia katika kifungu cha repairs and maintenance of buildings, nimetazama, hakuna fedha iliyotengwa pale kwa ajili ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Nimetazama katika kifungu hicho chicho kwa Polisi Zanzibar 2005, hakuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya jengo hili kulikarabati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimwulize Mheshimiwa Waziri: Je, pale Jeshi la Polisi amewahi kufika katika lile jengo akaona ile hali pale? Usipoziba ufa, utajenga ukuta. Kwa nini tusikarabati? Nimetazama katika fedha za ukarabati, kuna fedha zimewekwa chache sana lakini ziko katika mkoa mwingine. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia hiki kitu. Nasi tulikizungumza hiki, lakini sasa hakuna ambacho kimetengwa.
Mheshimiwa Spika, zimetengwa pesa katika kifungu cha Polisi Zanzibar cha 2005 ambapo fedha zilizotengwa, zimetengwa katika kifungu cha 22019 ambayo ni kwa ajili ya ukarabati mdogo wa Vituo vya Polisi. Kwa hiyo, hakuna ukarabati unaolenga nyumba za Polisi. Mheshimiwa Waziri hili mimi ni ombi langu tokea nimeingia katika Bunge hili. Moja nimepata, lakini hili sijapata. Kwa hiyo, hili nalitupia kwa Mheshimiwa Waziri tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine kwenye bajeti ya maendeleo; sisi pale Zanzibar Polisi viwanja vya kujenga majengo vimo, lakini Mkoa wa Mjini hatujatengewa fedha. Nimetazama kwa Zanzibar nzima kwenye bajeti hii, ukienda katika bajeti ya maendeleo, utakuta kuna shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Mkokotoni Kaskazini Unguja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale Zanzibar ukija ni aibu. Nyumba ya IGP wamewekwa maofisa wane. Watu wanaohamishwa wakazungushwa vituo, huwa wanakuja pale Mkoa wa Mjini Magharibi na wanafikia Ziwani Polisi. Kwa hiyo, hali ya makazi mle haiko vizuri. Nilipotazama katika kifungu cha 6303 construction of offices and quarters cha Zanzibar, ndiyo nimegundua kwamba kuna hiyo shilingi milioni
500. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, ajaribu kuangalia hivi vitu kwamba vitafanyika vipi ili nasi mjini pale tuweze kupata majengo.
Mheshimiwa Spika, kingine, nakwenda katika vote ya vitambulisho, hapa kwenye vote ya vitambulisho nizungumzie kitambulisho kule kwetu tunachokiita kitambulisho cha Mzanzibar. Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar iliingia gharama na mpaka sasa hivi inaendelea kuingia gharama kutoa vile vitambulisho ili viweze kufanya kazi; na kweli vikatoka. Vilitoka mwanzo kabla ya Kitambulisho cha Taifa. Vitambulisho hivi vimetoka, sasa hivi eti hata benki unapokwenda wanakwambia lete namba yako ya leseni ya gari wanakidharau hiki kitambulisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, hapa sasa hivi kuna usajili wa simu kwamba mtu anaweza akasajiliwa hata na leseni ya gari au kadi ya kupigia kura, lakini kitambulisho kilichomtambulisha kwa taarifa zake zote kinakataliwa. Kwa nini kitambulisho hiki kisiende sambamba na kitambulisho hiki cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Kwa nini tunakidharau hiki kitambulisho wakati tayari Serikali moja imeshaingia gharama na bado Ofisi ya Vitambulisho ipo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikwenda benki moja nikasema kwamba kadi yangu ya Uraia ya Utanzania sijachukua, nikawatolea kadi ya Zanzibar wakasema, aah bora ulete leseni ya gari. Hivyo kweli kitambuilisho cha Mzanzibar Mkaazi kikadharaulike ikapate hadhi leseni ya gari katika kupita huduma!
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kupitia Idara hii ya Vitambulisho vya Taifa ajaribu kuliweka sawa au kutupa ufafanuzi, kwa nini watu wasiweze hata kusajili simu kwa kutumia Vitambulisho vya Uzanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa nami naweza nikajiandikisha kukamata shilingi, kwa sababu kule Ofisi ya Vitambulisho ipo na bado inafanya kazi na gharama kubwa zimetumika.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie katika masuala ya ufanisi kwenye Jeshi la Polisi hususan nazungumzia utendaji kazi katika mikoa yote. Natoa mfano tu, mikoa yote ina Askari tofauti. Mkoa wa kwangu mimi wa Mjini Magharibi, takribani sitaji namba, ukienda kwenye randama ipo, lakini ina Askari wengi zaidi ya mara nne au mara tano ukilinganisha na mikoa mingine.
Mheshimiwa Spika, ukiacha tofauti ya mshahara, ukienda kwenye kifungu cha fuel, ukienda kwenye kifungu cha utilities, military services, travel in country, communication and information, ukiangalia vifungu hivi vyote vimepewa idadi sawa. Amount ya fedha sawa. Hivi kweli hii bajeti ni realistic?
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mjini tumewazidi watu mara nne. Watu wanaoishi pale Mkoa wa Mjini ni wengi, Mkoa wa Mjini Magharibi ni sehemu kubwa, kuna population kubwa, matukio ni mengi. Kwa nini katika kulihudumia Jeshi la Polisi tupewe sawa na Mkoa ambao uko chini mara nne?
Mheshimiwa Spika, naomba ufafanuzi kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu pale tunapokaa wakati mwingine Askari hutumia pesa zao kupiga simu kwa ajili ya kazi, kwa ajili ya kujaza gari mafuta na kufuatilia matukio mengine. Kwa hiyo, aje anipe ufafanuzi, kwa nini viko hivi? Is it realistic?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)