Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uzima na kuweza kuchangia leo hii katika hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara hii kwa jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika katika kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika katika nchi yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola na Naibu wake kwa kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazofanywa na Wizara hii lakini bado kuna changamoto katika mipaka yetu. Mimi natokea Mkoa wa Kigoma, huu ni mkoa ambao tunapakana na nchi nne za Congo, Burundi, Zambia na Rwanda ambapo mwingiliano na wenzetu hawa ni mkubwa.
Mheshimiwa Spika, mipaka yetu haina ulinzi wa kutosha kwani wakimbizi hawa wamekuwa wakifanya matukio ya kihalifu. Tumeona matukio ya ujambazi yakishamiri kila kukicha kwa kutumia silaha za moto, wananchi wamekuwa na hofu hawana amani na maisha yao. Hivyo niiombe sana Serikali tupate askari wa kutosha katika Wilaya zote za Kasulu, Kibondo, Buhigwa, Kigoma na Mkoa wetu kwa ujumla watu wake waishi kwa amani pasipo hofu ya ujambazi huu.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie tena suala la hawa ndugu zetu askari. Hawa ni ndugu zetu lakini ni watu muhimu sana kwani hawalali wakilinda usalama wa raia na mali zao, lakini pia amani ya nchi yetu. Niombe sana Wizara iwaangalie hawa askari wetu kwa jicho la pili kwani wanaishi katika mazingira magumu sana, hawana makazi bora na imara, wengi wanaishi mpaka kwenye nyumba za mabati, hii si sawa. Naomba sana Wizara iwathamini wapate nyumba za kutosha bora na imara, hii itawasaidia hata kuongeza bidii katika kazi. Pia watu hawa wamekuwa wakifanya kazi muda mrefu bila kupandishwa vyeo, niombe sana tuwalipe fadhila wapande vyeo kwani wanafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Spika, niguse suala la Vitambulisho vya Taifa. Kiukweli bado wananchi wengi sana hawajapata hivi vitambulisho, leo watu milioni 16 ndiyo ambao wamepata vitambulisho hivi wakati Tanzania ina watu zaidi ya milioni 50. Niombe sana Serikali iongeze kasi kuhakikisha wananchi wote wanapata vitambulisho na tumeona Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano wanasema kuanzia mwezi ujao watu watasajili line kwa kutumia Vitambulisho hivi vya Taifa. Niseme hili zoezi lisitishwe kwanza mpaka pale wananchi wote watakapopata hivi vitambulisho kama kweli tuna nia ya kuwasaidia hawa wananchi.
Mheshimiwa Spika, nigusie suala la ujenzi wa vituo vya polisi. Kiukweli hali ni mbaya sana yaani kuna vijiji ukifika unaweza lia kwa huruma, kwani majengo yao yapo katika hali mbaya sana. Unajiuliza hii ofisi kweli ndiyo wanafanyia kazi hawa askari wetu wanaolala usiku kucha wakilinda mipaka, usalama wa raia na mali, ofisi inataka kuanguka, hakuna hata vitendea kazi, kiukweli hii siyo sawa.
Mheshimiwa Spika, leo katika Kijiji cha Mwindiga ninapotoka kituo cha polisi kina hali mbaya sana, kituo kidogo lakini hakuna hata vitendea kazi, hawana magari. Naomba sana Wizara mkarabati vituo vya polisi lakini magari ya kutosha yapelekwe katika maeneo mengi kwani hali ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, kwa leo niishie hapa, nashukuru kwa kuweza kupata muda wa kuchangia leo kwa maandishi.