Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nami nichangie hoja hii ya hotuba ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia. Nami nitachangia mambo mawili tu. La kwanza, nitatoa shukurani kwa ajili ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, lakini nitachangia sana kwenye sera ambayo itakuwa na vijpengele viwili; kipengele cha Elimu ya Fundi kama ilivyo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini pia kipengele cha lugha ya kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi kubwa kwa Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa fedha nyingi ambazo amezitenga kwa ajili ya Wizara hii. Fedha nyingi ambazo zimefika ni pamoja na elimu bure na ujenzi wa shule, ujenzi wa madarasa na kwangu katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini Uyui, tumepata fedha za kutosha karibu shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi ya shule za high school na shule za msingi na shule za sekondari. Kwa hilo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote katika Wizara hii Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye sera. Nianze kwa ufafanuzi wa maneno ambayo yamekuwa hayaeleweki; na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna baadhi ya ufundi hakuutaja kabisa; na ndiyo ilivyo katika Wizara ya Sayansi na Teknolojia. Kwa hiyo, nianze na Technical Colleges (Vyuo vya Ufundi). Hivi vinazalisha mafundi wanaitwa technicians au kwa Kiswahili ni Fundi Sadifu; na hili Mheshimiwa Waziri hakulitaja kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna vituo vya ufundi vinaitwa VETA kwa Kiingereza. Hivi vinazalisha Artsans ambao ni Fundi Mchundo. Sasa taaluma nzima ya fundi inafanya kazi hivi: Juu tuna engineer, wanatafuata technician halafu Artsans. Ni kama vile madaktari, ukiwatoa ma-nurse pale hawafanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka wataalam wa elimu wamweleweshe vizuri Waziri wangu. Waziri ametoka kwenye ule mfumo wa kuanzia form one, form five, form six, university. Na sisi tumetokea shule za ufundi miaka minne ya ufundi uliochagua kama ni umeme au Civil Engineering halafu unaenda Technical College miaka mitatu unachukuwa FTC, unatoka kwenda kufanya kazi, unarudi unachukua Diploma in Engineering (DE) miaka mitatu, unakuwa na miaka kumi katika ufundi ambao umeusomea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, field hii ikifa tutafanya jambo ambalo haliwezekani. Wahandisi hawawezi kufanya kazi na Artsans. Kwa hiyo, kunakuwa na engineer huku kichwani, kiwiliwili hakuna, kuna miguu (Artsan) kule chini. Kwa hili lazima lisahihishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba nzima Mheshimiwa Waziri ameongelea mambo ya vyuo. Neno “vyuo” akiwa na maana ya vituo vya VETA. Tunajenga vyuo vingi; hatujengi vyuo vingi, tunajenga vituo vya VETA. Vyuo vya ufundi ni Dar Tech. ilivyokuwa nao wakapelekwa watu pale wakajaribu kuifanya iwe University College au University. Ikaacha mfumo mzima wa ufundi ikaenda kwenye mambo ya academicians. Halafu kimebakia chuo kimoja Arusha Technical College, maana yake hata Mbeya mmebadilisha, siyo college ya ufundi, imekuwa University. Matokeo yake tunakuwa na white collars hatuna Blue collars katika engineering na jambo hilo haliwezi kufanikiwa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba, kwangu nina shule 22 za secondary school na nina shule za msingi 222, hatuna chuo cha VETA. Vyuo vya Ufundi nafikiri nisimseme sana Mheshimiwa Waziri wangu, amenielewa; ni kwamba hakuna vyuo vya ufundi vinavyozalisha technicians wanaoitwa Fundi Sadifu. Fundi Sadifu ni tofauti na Fundi Mchundo. Serikali inajenga Vyuo vya Ufundi Mchundo ambapo katika elimu tunakokwenda huko kwenye Sera ya Uchumi na Viwanda hawatatusaidia Artsans, tunahitaji Fundi Sadifu (Technicians) hili lisahihishwe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaotuna wengi hapa, humu tuna mafundi; mimi ni fundi tena mkongwe. Wamo mafundi wengine kumi humu ndani tumetokea Ifunda au Moshi Technical, au Tanga Technical au Mtwara Technical College, tukasoma FTC halafu tena tukarudi, tukachukuwa Diploma…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Nataka nimpe taarifa muongeaji.
MWENYEKITI: Unataka umpe taarifa eeh! Mheshimiwa Maige, mnakutana mafundi mchundo.
T A A R I F A
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ameitaja Arusha Technical. Hiyo Arusha Technical College sasa hivi kuna kozi ya kusuka nywele. Kwa hiyo, tunakwenda kuharibu utamaduni ule wa ufundi. Kuna kozi za kusuka nywele, kuna shule upishi. Wakati mimi nipo pale Arusha Techn. Zile kozi hazikuwepo. Sasa hivi tunaanza kuwachanganya, hatuwezi kupata mafundi kwenye style hiyo. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Almasi.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni sawa kabisa, nakubali, huyo ni Fundi Sadifu mwenzangu (technician).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niendelee kwenye suala la lugha ya kufundishia. Nimesema naongelea mambo mawili tu; kwa ufundi nafikiri niishia hapo, lakini nijikite hasa katika suala la lugha ya kufundishia. Suala hili limo katika Sera ya Elimu na limeelezwa vizuri sana katika sura ya tatu ambayo inahusu mambo ya maazimio na malengo na lugha ya kufundishia. Ninayo Sera ya Elimu hapa ya mwaka 2014 ukurasa wa 38 inasema: “lengo ni kutumia lugha ya Kiswahili katika kufundishia.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maelezo, lakini muda sina, ila wenye sera hii wakasome sura tatu ukurasa wa 37 mpaka 38. Sasa naomba ni nukuu: “lengo la kutumia lugha ya Kiswahili katika kufundishia.” Tamko, nasoma kipengele cha 3, 2 na 19. “Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumiwa kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo na Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija Kitaifa na Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo tafiti zaidi ya 30 kwa muda wa miaka 45, zote zinasema: “mtoto yeyote ataelewa masomo vizuri kama atafundishwa kwa lugha ya kwanza au ya pili ya mtoto huyo.” Tafiti zote zimesema Kiswahili ndiyo lugha ya kwanza au ya pili kwa Watanzania wote. Kwa hiyo Kiswahili ndiyo lugha pekee inayofaa kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo, kipo kipengele kidogo cha mistari mitatu kimechomekwa hapa, naomba nikisome. Ni kipengele cha 3.2.20: “Serikali itaendelea na utaratibu wa kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiingereza katika kufundishia na kujifunzia, tena katika ngazi zote za elimu na Mafunzo.” Hivi vipengele viwili vinagongana na matokeo yake, imeacha nchi nzima isieleweke tunatumia lugha gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo, napenda kusema yafuatayo: kwa kuwa tafiti zimeonyesha kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya kwanza na inazungumzwa na Watanzania wote ikitumika kufundishia, kujifunzia elimu na maarifa mafunzo, yataeleweka zaidi kwa walengwa; kwa kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na Tunu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo haya ya kwenda kutumia Kiswahili; na tatu, kwa kuwa tafiti zaidi ya 30 zilizofanyika katika miaka zaidi ya 40 zimeonyesha kuwa Kiswahili ndiyo lugha inayofaa kwa Tanzania kufundishia na kujifunzia; na kwa kuwa nia ya mabadiliko ya lugha ya kufundishia na kujifunzia ni pamoja na kuimarisha mbinu za kufundishia Kiingereza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie; na kwakuwa muda sasa wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake kubwa za kukithamini na kukikuza Kiswahili. Hivyo, kitumike Serikalini, Bungeni na kuwa lugha ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo nchini. Serikali ilete Bungeni hoja…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maige.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)