Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyopo mezani kwetu hapo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka 15, nchi yetu imekuwa katika harakati kubwa ya kupanua upatikanaji wa elimu na juhudi kubwa zimefanywa ili elimu imfikie kila mtoto wa Tanzania. Napenda sana niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi na hasa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa wanayofanya hasa kwa kukubali baada ya kupanua elimu hii, kuitoa bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Waziri wa Elimu aliwasilisha bajeti ya Wizara ya Elimu na kwa muda tuliopo sasa katika kupanua elimu, bajeti ile imeitendea haki Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa hiyo, napenda sana nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa kazi nzuri ambayo inaonekana kufanywa. Kwa upande wetu kwa wakati huu kazi kubwa ni kuboresha elimu, kuishauri Serikali pale ambapo inaweza kufanya vizuri zaidi katika kutekeleza suala hili la kuboresha elimu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuboresha elimu, jambo la kwanza lazima uwe na walimu. Niendelee kusema kwamba tunaendelea kuiomba Serikali ihakikishe kwamba inapeleka walimu wengi wa kutosha hasa katika shule za msingi. Wiki iliyopita, sisi katika Wilaya ya Mwanga tumepewa walimu wachache; tuliomba walimu 386, tumepewa walimu 30 hivi na tunategemea kupewa wengine mwezi wa Sita. Kwa hiyo, mwezi wa Sita utakapofika tungependa tuone significant kabisa walimu wa kutosha kabisa ili waweze kufundisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kuhusiana na bajeti hii kwamba ili elimu ya Tanzania iboreke, ni muhimu Serikali ichukue hatua ya kuboresha Idara ya Ukaguzi. Wafanyakazi wa Idara ya Ukaguzi wengi wanaomba kuondoka kwa sababu mishahara, madaraja na marupurupu yao na nafasi ya kazi wanayokuwa nayo siyo nzuri kama wale ambao wanaofanya kwenye kufundisha na kusimamia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la kwanza ambalo napenda kupendekeza, Wizara iangalie Idara ya Ukaguzi wa Shule na imlinganishe Mkaguzi Mkuu wa Shule na Kamishna wa Elimu. Kule kwenye mikoa, Mkaguzi Mkuu wa Kanda awe sawa sawa na wale Manaibu RAS wa kule kwenye mikoa na wale wafanyakazi ambao wanafanya kwenye Idara hii waweze kupewa vyeo sawa sawa na Maofisa wa Elimu wanaoshiriki katika kuendesha elimu katika Wilaya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni muhimu sana idara hii ipatiwe vifaa; magari na vifaa vya ukaguzi ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuwafikia walimu na kwamba ripoti ya ukaguzi wa shule na ukaguzi wa kila mwalimu katika kufundisha unaongezea katika sifa za mwalimu kupandishwa madaraja na kupandishwa vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunapotaka kuboresha elimu ni muhimu sana tulenge tunafanya nini? Katika miaka ya kwanza miwili ya shuleni, ni vizuri sana tuache kuwafundisha kila kitu watoto wa Darasa la Kwanza na la Pili. Tulenge kuwafundisha vitu vitatu peke yake kwa miaka ile ya kwanza mitatu ya shule; Darasa la Awali, Darasa la Kwanza na Darasa la Pili tuwafundishe zile K tatu; Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na namna ya kutumia namba katika maisha. Tuache kuwafundisha masomo yote, tuwafundishe hivyo vitu vitatu tu ili wakitoka hapo wamevishika na wanaweza kujifunza mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi hii ya elimu ya msingi na hata sekondari, ni muhimu sana tuboreshe hii mitaala na tutunge sasa vitabu ambavyo vina tija, vinaweza kuwafundisha watoto wetu wakajifunza, wakaelewa kinachofundishwa. Tusiongee juu ya joto la mwili wakati tunaongea juu ya homa, tuongee juu ya Malaria; tutibu Malaria tusitibu joto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, ni muhimu sana tutunge vitabu vizuri na katika kila somo kuwe na wataalam waliobobea katika somo hilo ambao wanatoka kwenye taasisi za nchini humu, taasisi za Serikali kama Vyuo Vikuu, taasisi zisizo za Serikali, Vyuo vya Ualimu na hata Shule zetu za Sekondari na Msingi. Tutoe wataalam wa masomo hayo ambao wataandaa mitaala, vitabu vya kutumia na wale ambao watafanya review, wataviangalia kama vinafikia standard inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika ngazi hiyo ni kwamba katika sekondari, shule zetu nyingi hazina maabara. Tumeacha kazi ya kutengeneza na kujenga maabara, tumewaachia wanavijiji. Wanavijiji hawajui sayansi na hawana uwezo wa kujenga maabara, lakini tumewaachia. Hii ni kwa sababu katika hatua ya upanuzi tulifika mahali hela zimetuishia, lakini kwa sasa hatuna sababu yoyote ya kuwaaachia wanavijiji watujengee maabara ya sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninapendekeza kabisa Wizara ya Elimu itenge fedha kwa makusudi kabisa, ijenge na kumalizia maabara zote ambazo zipo huko kwenye Shule zetu za Kata. Hili litatusaidia, tukisema tunataka kuongeza wanasayansi, tuanze kuwafundisha wanasayansi. Hivi sasa haiwezekani. Tunavyo vifaa vya maabara lakini vimewekwa stoo na vikiwa stoo haviwezi kufundisha watoto. Kwa hiyo, ninashauri sana tujenge maabara na tufanye hili jambo liwe la makusudi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, niliwahi kupendekeza hapa kwamba ni muhimu sana tuwapatie watoto wote mikopo ya kusomea katika Vyuo Vikuu. Katika hotuba ambayo imesomwa jana tumeletewa na Waziri, juhudi kubwa sana imefanywa kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo lakini mimi nadhani hakuna sababu yoyote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Profesa. Mheshimiwa Dkt. Tisekwa halafu jiandae Mheshimiwa Mama Salma.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)