Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara hii. Wamekuwa wasikivu sana na tunaona kazi zinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina wana msemo usemao, ‘ukitaka mafanikio ndani ya mwaka mmoja panda mahindi, ukitaka mafanikio baada ya miaka kumi mpaka ishirini panda miti, ukitaka mafanikio yatakayodumu kizazi na kizazi basi wekeza kwenye elimu’. Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi sana kutengeneza miundombinu ya elimu kwa kuhakikisha kila mtu mwenye uwezo wa kwenda darasa la kwanza anakwenda na afike mpaka form four na kujitahidi kuweka maboma, madarasa na madawati ili wanafunzi waende shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miundombinu mizuri inayoendelea kuwekwa na Serikali tuna changamoto kubwa moja ambayo kama nchi lazima tuwe na tafakari. Changamoto ni ubora wa elimu ambayo tunaitoa nchini. Ukiangalia kwa umakini matatizo yote ambayo yapo kwenye sekta ya elimu yameshindwa kujibu swali tunatoa elimu kwa ajili ya nini? Baada ya kutoa elimu matokeo ya ile elimu nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwetu sisi mafanikio ya elimu tunayahesabu kwa viwango vya madarasa yaani tulikuwa na wanafunzi 2,000 wenye uwezo wa kwenda darasa la kwanza wote wakaenda darasa la kwanza, wote wakamaliza darasa la saba, wote wakaenda form four, wote wakaenda chuo kikuu ndiyo kipimo chetu cha elimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa upande mmoja tunatatua tatizo moja tu we call it delaying techniques kumpa mtu matumaini kwamba kuna promise land inaweza ikaja huku mbele, kuna maana na asali iko huko mbele lakini in reality hicho kitu hakipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa elimu ulipaswa umuandae mwanafunzi katika level atakayoishia yoyote ile imwezeshe kuishi. Kama nguvu zake ni kuishia darasa saba akimaliza darasa la saba awe na uwezo wa kuishi. Kama ana nguvu za kufika form four, hawezi kwenda form five na form six, elimu aliyoipata imsaidie akifikia pale aweze kuishi hali kadhalika mpaka university. That’s why today unakuwa na engineer ambaye hawezi hata kutengeneza barabara na unakuwa na daktari ambaye badala ya kupasua mguu anapasua kichwa. Hii ni tafsiri kwamba elimu yetu haijamtengeneza vizuri wanasema umepata elimu lakini haujaelimika, tunatengeneza watu wenye elimu lakini hawajaelimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri kuna mambo mawili lazima uyaangalie ndiyo yatakayotusaidia. Jambo la kwanza ni Sera yetu ya Elimu. Sera yetu ya Elimu ya mwaka 2014 ina changamoto mpaka leo haitekelezeki kwa sababu yawezekana stadi haijafanyika vizuri au tu kuna mtu anaamua ku-roll a ball, sisi kwenye mpira tunasema unaamua tu kukokota mpira uwende basi ukifika golini likiwa goli sawa mipira ukipaishwa sawa, tuna changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine mnaitengeneza wenyewe kwa nyaraka na miongozo mnayoitoa. Kwa mfano, Waraka Na.5 wa mwaka 2011 unasema mwanafunzi katika mwaka atahudhuria vipindi siku 194 lakini kama kutakuwa na mtoro hatafukuzwa shule mpaka asihudhurie siku 90 mfululizo, unatengeneza nini hapa? Huu Waraka unatengeneza mazingira ya mwanafunzi kuwa mtoro kwa sababu hatahudhuria darasani siku 30 atakuja siku mbili, hatahudhuria tena 30 atakuja siku tatu ili tu zile siku 90 mfululizo ambazo kwa mujibu wa Waraka mlioutoa ndiyo unazipa mamlaka shule na vyombo vyake kumfukuza huyu shule matokeo yake tunatengeneza wazembe ndani ya shule. Niiombe sana Wizara iangalie Waraka Na.5 wa mwaka 2011 ambao unasema mwanafunzi atafukuzwa shule tu endapo hatahudhuria vipindi mfululizo kwa siku 90, hii si sawa iangaliwe tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, kipimo chetu cha ufaulu ili mtu atoke kidato cha pili kwenda kidato cha tatu anapaswa kuwa na D mbili au awe na A moja au na B moja au C moja. Taafsiri ya D mbili ya form two ni zero au ‘F’ ya form four. Maana yake from day one unaiandaa zero na kuipalilia iende. Kwa nini mtu huyu kiwango chake cha kuvuka darasa kiwe D mbili ambacho tunajua ni kiwango cha chini kabisa cha kufaulu, tutarajie mbele aje afanye mambo mazuri, kitu hicho hakiwezekani na tukienda hivi tutatengeneza kizazi cha zero cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaongelea sayansi na teknolojia (ICT). Mpaka leo ni ya ajabu nchi yetu haina combination ya kidato cha nne yenye somo la ICT. University tuna computer science, kidato cha tano na sita hakuna ICT. Niiombe Wizara, najua mmeshafanya kazi, mko katika hatua za mbali kwenye hili hakikisheni ICT iwepo kati ya combination za form five na form six. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kuna jambo ambalo sielewi Serikali mnalichukuliaje kati ya uhusiano wa Serikali kwenye upande wa elimu na private sector. Kwa sasa inavyoonekana uhusiano wa Serikali na private sector kwenye elimu siyo kama hawa equal partners wanaotoa huduma katika jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia historia private sector imetusaidia sana kutoa elimu sehemu Serikali haikuweza kutoa kwa miaka mingi. Nitoe tu mfano, kwa Mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma mpaka mwaka 1997 kulikuwa hakuna hata high school moja, waliokuwa wanataka kusoma high school za Serikali ilikuwa lazima watoke nje ya mikoa hii niliyoitaja na ikitokea hakuna nafasi basi waende wakasome private kidato cha tano na sita kipindi kile zilikuwa shule tatu tu Mbeya ama akasome Irambo, Sangu na Meta, hawa watu wamesaidia sana ku-cover gap ambayo Serikali haikuweza kufanya katika kipindi kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unakuta kama kuna aina ya upendeleo kwenye kutoa adhabu kati ya shule za Serikali na shule za private endapo zitakuwa zimekosea. Mwaka jana kulikuwa na uvujaji wa mitihani wote tulizisikia shule za Serikali kule Chemba mlisikia na shule nyingine, zile shule za private zote zimefungiwa, zile shule za Serikali hazijafungiwa.
Mheshimiwa Mwyekiti, sasa watu wanauliza, hivi kumbe ukiiba mtihani kwenye shule za Serikali adhabu yake ni ndogo tu mwalimu anaondoka, ukiiba mtihani kwenye shule ya private unafungiwa, matokeo yake private wataendelea kuwa makini …. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)