Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba Serikali anayoiongoza inatimiza na kutekeleza ahadi ambazo imeziweka kwa wananchi hususan kwenye sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri, kumpongeza Naibu Waziri, pamoja na Makatibu wake, Manaibu Katibu Mkuu lakini kwa namna ya kipekee nimpongeze sana Dkt Pilap ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hii. Kwa jumla watu hawa wanafanyakazi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Elimu kwenye upande wa kuimarisha miundombinu ya shule zetu naitambua, lakini natambua pia kazi hiyo wanashirikiana vizuri na TAMISEMI. Sikupata fursa kuchangia wakati wa TAMISEMI lakini lazima niseme hapa kwamba halmashauri ya mji wa Masasi ambayo ndiyo Jimbo langu, limepata fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na shule za sekondari. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika fedha hizo tumepata pia bahati ya kupata fedha za kujenga shule mpya, shule ya msingi, shule ya kisasa kabisa yenye thamani ya zaidi ya milioni mia saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara tena kwa kazi kubwa ya kuimarisha vyuo vyetu vya maendeleo kwa kweli vyuo vya maendeleo ya wananchi vilikuwa vimeachwa kwa muda mrefu bila ya kufanyiwa matengenezo yoyote kiasi kwamba hata wale waliokuwa wanakwenda kusoma pale kwa kweli walikuwa hawapo katika wakati mzuri. Lakini niseme tu kwamba vyuo hivi ni vyuo vya wananchi masikini wananchi wa kawaida kabisa ambao kimsingi wanavitegemea sana katika kujenga stadi zinazoweza kuwafanya waweze kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi, katika awamu ya pili kimetengewa fedha zaidi ya shilingi milioni mia tano katika kuimarisha miundombinu yake. Niipongeze sana Wizara kwa uamuzi huu wa kukiboresha chuo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwaombe sasa Serikali waone namna wanavyokwenda kwenye stage nyingine ya kuimarisha sasa ujifunzaji wa vijana wetu katika vyuo hivi. Kuna tatizo kubwa sana la walimu katika vyuo hivi, lakini pia kuna tatizo kubwa sana la vifaa vya ufundi katika kujifunza vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Masasi, kinahitaji walimu 24 lakini kina walimu sita tu kina upungufu wa walimu 18. Nilikitembelea Chuo hiki nikakisaidie kompyuta chache lakini hazitoshi hawana vifaa vya kufundishia, hawana vifaa vya kufundishia aina mbalimbali za ufundi hata baadhi ya vifaa vinakuja vinakuwa ni mali tu ya waalimu na wanafunzi kwa kweli hawapati muda wa kushirikishwa kikamilifu katika kujifunza. Wizara ione namna ambavyo inaboresha vyuo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo wazo tunavyo vyuo vya watu wenye ulemavu, watu wenye ulemavu watu wasioona tunavyo vyuo. Nchi hii ina sita sita tu vyuo hivi viko chini ya Wizara yenye dhamana inayoshughulikia walemavu. Lakini ninaushauri kwamba ni vema sasa Serikali ione kwasababu Wizara hii ndiyo yenye Sera ya Elimu na ndiyo yenye methodology, nashauri vyuo vyote vile sita ambavyo tunavyo ambavyo kwa kweli vipo katika hali mbaya sana vichukuliwe na Wizara ya Elimu ili viweze kupata huduma inayostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vyuo hivi sita vilivyopo katika nchi hii chuo kimoja kipo katika Jimbo langu la Masasi, kinaitwa Chuo cha Wasioona cha Mwengemtapika, Chuo hiki sasa kimebaki majengo tu hali ni mbaya sana, naomba Waziri Serikali ione namna ambavyo Wizara ya Elimu inaweza kupewa dhamana ya kuviendesha na vyuo hivi navyo ili viweze kutoa mafunzo yanayostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kama alivyosema Mbunge aliyetangulia ni muhimu sasa hata katika vyuo hivi kufanya elimu jumuishi tufanye inclusive education tuungane wale wasioona na watu wenye maumbile mengine ya kawaida ili waweze kufanya kazi zao kwa vizuri zaidi, tusiwatenge na huko ndiko dunia inakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la elimu ya ufundi, Mheshimiwa Mbunge aliyepita amezungumza kwamba miongoni mwa mambo ambayo yanatusumbua sana ni kutoona kwamba kila level ya education lazima iwe level of exit. Lazima iwe level ambayo inaweza kumfanya ajitegemee, hili ni jambo la msingi sana kuliko mambo mengine yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ina mambo mengi, lakini miongoni mwa mambo hayo ni kuwajenga vijana wetu kifikra na kuwajenga vijana wetu kiustadi ili waweze kujitegemea. Katika shule za msingi katika miaka ya 70 mpaka miaka ya 80 karibu na 90, ukisoma malengo ya shule ya kuhitimu shule ya msingi, ilikuwa ni kumuwezesha mtoto anayehitimu shule ya msingi na kushindwa kuendelea mbele aweze kufanya kazi za kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la msingi sana kipindi kile tulikuwa tuna shule ambazo ni shule za msingi lakini ni shule za msingi zenye fani za ufundi, tulikuwa tuna shule za msingi zenye fani za kilimo. Ni lini tumefanya utafiti tukaona ni dhambi kuendelea na shule za msingi zenye mashamba? Ni lini tumefanya utafiti tukaona ni dhambi kuendelea na shule za msingi zenye karakana ya ufundi wa kawaida kama ufundi seremala, ili baadhi ya watoto watakaotoka pale ambao wameshindwa kuendelea au hata kama waliweza kuendelea wanaendelea katika elimu ya sekondari huku wana skills wana-study zinazoweza kuwafanya waweze kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ione namna ambavyo itarudisha elimu ya ufundi na kuimarisha vyuo vya ualimu ambayo vilikuwa ni vyuo vya ufundi kutoka katika elimu ya msingi mpaka katika elimu ya Chuo Kikuu. Wabunge wengine wamezungumza inawezaje unamfundisha mtu Bachelor degree ya Education ukitegemea aende kufundisha baadaye unataka ajitegemee wakati hakuna msingi wowote huku chini uliojengwa wa kumfanya aweze kujitegemea hapo baadaye ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya shule za private zipewe mwongozo wa kuwa shule za private za msingi ambazo zinatoa elimu ya ufundi, na elimu ya kilimo, lakini baadhi ya shule zetu za zamani ambazo zilikuwa zinatoa mafunzo ya ufundi ziendelee kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nieleze suala la elimu nje ya mfumo rasmi, tangu 2016 katika hotuba zote nilizochangia kwenye Wizara ya Elimu nimezungumza kuhusu non formal education, nashukuru leo Mheshimiwa Ngombale naye amezungumza. Nimekuwa nikisema kwamba Wizara ya Elimu siyo Wizara ya wale waliopo madarasani ni wizara ya watanzania wote. Wapo watanzania wengi sana ambao wanauhitaji wa elimu lakini hawajajengewa fursa za makusudi za kuipata elimu hiyo, wapo watanzania wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alitoa tamko la kwamba watoto ambao wanapata ujauzito hawataendelea kusoma katika mfumo rasmi, tamko lile lilikuwa linamaana sana lakini halikuwa linamaanisha kwamba watoto hawa hawawezi tena kupata fursa ya elimu. Fursa zipo lakini wizara ina mikakati gani kusaidia watu hawa? Wizara ina mikakati gani kuwasaidia watoto hawa wanaopata ujauzito nje ya mfumo rasmi waweze kusoma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunafahamu kwamba tunawasajili watoto wa miaka sita, miaka saba kwenda shule za msingi tunajua watoto wangapi wa miaka minane na miaka tisa wapo huko mitaani na hawapati fursa ya kwenda katika mfumo rasmi wa elimu? Tunajua kwamba kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kinaongezeka kila siku? Serikali inakuja na mkakati gani? Tukipata majibu ya Waziri anayoweza kutuambia kuna program ya MEMKWA na nilikuwa ni mwezeshaji huko wakati wangu, tunaweza tukaambiwa kuna mukeji …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)