Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze na hoja ya matokeo ya kidato cha nne na darasa la saba na namna yanavyo-reflect uhalisia. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi, matokeo ya kidato cha nne, ya mwaka 2017 nitaitaja Mikoa nane ya mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga ilishika nafasi ya 24, Ruvuma ilishika nafasi ya 25, Mjini Magharibi nafasi ya 26, Lindi nafasi ya 27, Kusini Pemba nafasi ya 28, Kaskazini Pemba nafasi ya 29, Kusini Unguja nafasi ya 30, Kaskazini Unguja nafasi ya 31. 2018 Tanga 24, Mtwara 25, Mjini Magharibi 26, Lindi 27, Kusini Pemba 28, Kaskazini Pemba 29, Kusini Unguja 30 na Kaskazini Unguja 31.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amejifunza nini kwenye matokeo haya? Mikoa ni ile ile na kwa bahati mbaya mikoa yenyewe iko kwenye Ukanda mmoja, Ukanda wa Pwani. Tunapozungumzia inclusive education lazima iambatane na inclusive performance ambayo itakuja kuleta inclusive development. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ukanda mmoja, watu wanafanya vizuri ukanda mwingine watu hawafanyi vizuri, tunakwenda kutengeneza matabaka katika Taifa letu. Mheshimiwa Waziri wa Elimu lazima aipitie Sera ya Elimu, lazima matokeo haya yamfundishe jambo, kwa nini Lindi kila siku wanakuwa wa mwisho? Kwa nini Kusini Unguja kila siku wanakuwa wa mwisho? Kwa nini Tanga kila siku na mikoa yenyewe yote iko kwenye Ukanda wa Pwani? Mimi siamini kama watu wanaokaa Ukanda wa Pwani, hawana akili, siamini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vigezo vingi vya kupima kwamba uelewa wao ni mkubwa na performance zao katika maeneo mengine ni mzuri. Hawa watoto wa pwani sio kwamba hawapendi elimu, kuna watu wanakuja na majibu mepesi kabisa, watu wa pwani hawapendi elimu, hawapendi kusoma, sio kweli. Wanasoma, ukiwapeleka madrasa mtoto amesoma juzuu thelathini, amehifadhi, anaweza akasoma Quran vizuri, kwa nini ashindwe kusoma kitu alichofundishwa kwa Kiswahili? Yaani mtu anaweza kutafsiri Kiarabu alichofundishwa, lakini eti kujibu methali ya haba na haba, hujaza kibaba, anafeli? Kuna namna lazima tutafakari na tujiulize, tusiwe na majibu mepesi, jambo hili ni kubwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine amezungumza Mheshimiwa Mbatia, inawezekana Kilimanjaro wanaonekana nafasi ya kwanza kwa sababu ya idadi ya shule za private, nadhani kama Serikali inataka wajitathimini waone performance ya shule za Serikali, watoe matokeo ya shule za Serikali peke yake kwanza, halafu wawe na matokeo ya shule za Private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lindi mathalani, Lindi shule za private hazifiki hata sita, ina maana hii competition inayokwenda, inakwenda Canossa na shule zingine zinakwenda kupambanishwa na shule hizi za kayumba zilizopo Lindi. Hakuna shule za private Lindi, sidhani kama Kaskazini Pemba au Kusini Pemba kuna shule za private. Kwa hiyo mtai-label hii mikoa kama ni mikoa ya mwisho kila siku, kumbe hawapambani shule za Serikali na shule za Serikali, wanapambana shule za Serikali na shule za private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hoja very sensitive, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuiangalia, lazima tuwe na inclusive education ili tuweze kuja kuwa na inclusive development, vinginevyo tutatengeneza matabaka ambayo wakati mwingine yanaweza kuja kuleta matatizo, haiwezekani kila siku Mikoa ya Pemba ndiyo ya mwisho. Bahati mbaya sana, panapotokea matokea ya kuwa wa mwisho, wanaoathirika ni Maafisa Elimu wa Mikoa, utasikia kila siku, Afisa Elimu wa Mkoa Lindi kabadilishwa, Afisa Elimu wa Mkoa sijui Mtwara kabadilishwa, Afisa Elimu Mkoa wa Tanga anabadilishwa na sio kubadilishwa, wakati mwingine kwenye mikutano hii ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, na wakati mwingine wanadhalilishwa pia. Sasa inawezekana unamlaumu huyu, kumbe yeye shule zake ni sa Serikali tupu. Anapambanishwa na maeneo ambako kuna shule nyingi za private. Hili ni jambo, ni jambo ambalo linahitaji tafakuri ya kina, na lazima waliangalie kwa umakini mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya hadhi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere; hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu, alitembelea katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, nami ni mhitimu wa kile chuo na Mheshimiwa Waziri niliona aliambatana naye na Mheshimiwa Waziri Mkuu akatoa maagizo kwamba kile chuo kipandishwe hadhi ya kuwa Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki moja baadaye ndani ya Bunge hili hili, mimi nikauliza swali lile lile, likajibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri, akasema kwa sasa Serikali haina mpango wa kukipandisha hadhi Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ni-contrary na kile alichokieleza Mheshimiwa Waziri Mkuu pale chuoni siku ile walipokwenda, sasa wanafanyaje kazi Mawaziri? Huku Mheshimiwa Waziri Mkuu anaagiza, kuwe na Chuo Kikuu kipandishwe hadhi, huku majibu ya Serikali ndani ya Bunge kwamba kwa wakati huu hakuna, lakini Mheshimiwa Waziri, hoja yangu ni nini? Hoja yangu kwanza ni kuthamini mchango wa Muasisi wa Taifa hili juu ya Sekta ya Elimu, kwanza hiki Chuo ndiyo chuo cha kwanza kabisa cha wazalendo kujengwa na wazalendo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wenzetu kwenye Mataifa ya wenzetu, Baba zao wa Mataifa yao, wale Waasisi wa Mataifa wote, wamepewa majina ya Vyuo Vikuu. Ukienda Kenya leo, unakuta Kenyata University, ukienda South Africa kuna Nelson Mandela University, ukienda Ghana unakuta Kwame Nkurumah University, kwa nini Tanzania hakuna Mwalimu Nyerere University, kuna shida gani, kwani kuna ukakasi gani? Elimu inayotolewa ni ile ile, kuna ukakasi gani wa kukipandisha hadhi Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuwa University?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nimeona katika ukurasa wa 184 mwaka huu wanaenda kutoa na Shahada za Uzamili, sasa kama wamefikia mpaka hatua ya kutoa Shahada za Uzamili? Kwa nini wanapata ukakasi wa kukipandisha hadhi chuo hiki kuwa Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mwaka juzi, mwaka jana na mwaka huu nasema, juu ya shule ya Sekondari ya Mchinga na Mheshimiwa Maftaha alitoa ushahidi hapa, shule ina vigezo, ina madarasa mengi, ina Walimu wengi, Walimu karibu asilimia 95 ni graduates, kuna shida gani kuipandisha hadhi ya kuwa high school? Jimbo la Mchinga hakuna shule ya high school hata moja, shule zote za sekondari zinazalisha watu wanaokwenda high school wanakwenda nje ya maeneo yale na wakati mwingine wengine wanaachwa wanakosa nafasi kwa sababu ya uhaba wa shule za A-level.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliangalie sana, mwaka huu tumeanza mchakato wa kujenga mabweni na nina hakika mpaka mwakani tutamaliza, wananchi wamehamasika sana, hebu waiweke kwenye mpango shule hii kuifanya ni miongoni mwa shule za high school itatusaidia sana kuondoa gharama za vijana wanaokwenda maeneo ya mbali kwenda kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mnafiki kama sitasema kuhusu Walimu, mimi mwenyewe nimefundisha miaka mingi najua maisha ya Walimu bado yana changamoto, mishaharara wanayopata ni midogo, lakini pia suala la upandishaji wa daraja. Walimu wamekaa wanatega masikio kusikia kesho Mheshimiwa Rais atasema nini, lakini kama hakuna itaenda vilevile, itapita bila bila tu kama hakuna chochote, wana-demoralize watu na matokeo yake performance inakuwa ndogo kwa sababu Walimu wana matatizo mengi kabisa, wengi tulikuwa Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. (Makofi)