Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mfumo wa elimu Tanzania umezeeka, umechoka na umechakaa. Ukiangalia sheria iliyoanzisha sekta ya elimu ni sekta ambayo tunalingana umri. Mimi sasa hivi ni mzee. Mfumo wa elimu ambao hauwezi kujibu matatizo ya nchi, huo mfumo umezeeka, umechoka lazima uangaliwe kwa upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kitabu cha Kamati, ukurasa wa 12, nitanukuu baadhi ya maneno wanasema: “Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Kamati umebaini kuwa baadhi ya maoni yanaendelea kutekelezwa na baadhi bado hayajatekelezwa kabisa. Baadhi ya masuala ambayo Kamati inaona yana umuhimu lakini bado hayajatekelezwa ni pamoja na; mimi nachukua ile (c), kuangalia upya mfumo wa elimu yetu nchini ni jambo ambalo Kamati inaona halijafanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Biblia sehemu fulani inasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Sehemu nyingine Biblia inasema mkamate sana elimu usimwache aende zake, mshike sana maana yeye ndiye uzima wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka tu twende vizuri kama Waheshimiwa Wabunge. Watoto wanaomaliza darasa la saba ni wangapi ambao hawaendelei na sekondari? Watoto wanaomaliza form four ambao hawaendelei na form six ni wangapi? Watoto wanaomaliza form six ambao hawaendi vyuo vikuu ni wangapi? Mfumo wetu wa elimu ni mfumo unaowaandaa watu kwenda kuajiriwa si mfumo unaowaandaa watu kujitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuchukulie tu takwimu ya 2017/2018, waliofeli mwaka 2017 darasa la saba ni 247,915 sawa na asilimia 27. Mwaka 2018 waliofeli ni 210,215 sawa na asilimia 22. Hawa wanaenda wapi na wana ujuzi gani? Kwa hiyo, ni lazima mfumo wetu wa elimu tuupitie upya. Mataifa yote duniani ambayo tunasikia ni matajiri kamaMarekani, China, Finland na Uingereza lakini utajiri walionao sio raw materials bali ni brain na brain inahitaji uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu moja kwenye Biblia inasema bora hekima basi jipatie hekima, naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Narudia, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Maana yake uwekezaji kwenye elimu ni gharama na halikwepeki. Ili nchi yetu iweze kubadilika lazima mfumo wetu wa elimu tuubadili. Hiyo hatuwezi kuikwepa ni lazima tubadili mfumo wetu wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasema kwa mfano asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania ni wakulima, hivi tunawafahamu hao wakulima? Unadhani wakulima ni wale wanao-graduate, ni wenye PhD au ni maprofesa? Wakulima ni hawa waliofeli darasa la saba na form four, tumewapa skills gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni shahidi wakati naanza darasa la kwanza nilijifunza kupalilia na kutengeneza bustani shule ya msingi. Leo shule zote za msingi watoto anamaliza la saba hajui kushika jembe, tunamwandalia mazingira gani? Leo tunataka tupate wafugaji bora, kule shule ya msingi tunajua wafugaji ni darasa la saba, uongo? Wanaofuga ni darasa la saba, wana skills za ufugaji na agriculture?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri masomo ya kilimo yako wapi, tume-concentrate na masomo mengine masomo ya kilimo hakuna, masomo ya biashara hakuna, tumeondoa. Wakati umefika tuko kwenye karne ya viwanda lazima watoto wetu wapate masomo ya usindikaji, kilimo na ujasiriamali kuanzia shule za msingi and so forth kinyume na hapo haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba sana unilindie muda wangu, samahani. La pili ni lugha ya kufundishia na hapa naomba ninukuu abstract kidogo kutoka kwenye blog moja ya Science Direct kuhusu lugha ya kufundishia. Wanasema: “The importance of learning a foreign language in childhood. Among philosophers, empiricism and the psychologist, behaviourists believe that language is a social creature and like other social behaviours are aquired. Language learning is natural. Babies are born with ability to learn it and that learning begins at birth. Many experts believe that learning the language before the age of ten years allow children to speak correct and fluent as an indigenous person. Therefore, whatever the earlier children become familiar with the foreign language, he/she have better chance to speak proficiency. Research suggests that from birth through age ten is the best time to introduce new languages to a child.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya kujifunza shuleni lazima ianzie utotoni, lazima Tanzania tujue sisi siyo kisiwa. Hii biashara ya Kiswahili kuanzia darasa la kwanza then sekondari imeshapitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wapo wanaosema twenda kwenye Kiswahili, mimi niwaambie kama tunachagua kwamba ni Kiswahili tujuulize maswali, who are we trading with, tunafanya biashara na akina nani? Kama unataka kufanya biashara na China, Marekani, Rwanda, lugha sahihi siyo Kiswahili bali ni Kiingereza.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Ahsante, mengine uandike.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu nimalizie.
MWENYEKITI: Haya malizia sekunde kumi.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikiuliza hapa Wabunge, Mawaziri na watu wengine wenye pesa wangapi watoto wao wanasoma shule za Kiswahili kama sio English Medium, kama siyo shule za private.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. MARWA R. CHACHA: Kwa hiyo, English is the solution.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.