Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Nianze kwa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa maamuzi yake makubwa na ya msingi kabisa ya kuamua kutoa elimu bila malipo. Hili jambo limekuwa zuri na limeongeza sana wanafunzi kwanza kuanzia shule ya msingi na sekondari, lakini jambo hili limekuja na changamoto nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kwenye miundombinu ya elimu msingi, kwenye shule zetu za primary kuna upungufu wa madarasa kwa asilimia 85, kuna upungufu wa vyoo kwa asilimia 83, kuna upungufu wa walimu kwa asilimia 60. Sekondari vivyo hivyo, hii ni kutokana na ripoti ya CAG, madarasa kwenye sekondari ni asilimia 52, maabara asilimia 84, madawati asilimia 86.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwiano wa ongezeko la wanafunzi kuanza shule na uwiano wa miundombinu bado havilingani. Tumeongeza wanafunzi kwa asilimia 17 lakini mpaka hivi tunavyoongea ni asilimia moja tu ya madarasa ndiyo yameongezeka, inafika mahali darasa moja linakuwa na wanafunzi 100 – 150. Kiuhalisia hili suala linakuwa gumu na vilevile hatuwezi kupata elimu ambayo itakuwa bora kwa uwiano mwalimu mmoja na wanafunzi 150. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wenzangu wamezungumzia kuhusu upungufu wa walimu. Kuna upungufu mkubwa sana wa waalimu, hususan walimu wa sayansi. Nikitoa mfano Wilayani Mwanza kwenye Jimbo la Buchosa, kuna shule hakuna kabisa walimu wa sayansi na mwisho wa siku tunakuja tunategemea wanafunzi wa form two wafanye mitihani ya Taifa ya NECTA ambayo inahusisha na masomo ya sayansi. Hawa wanafunzi tunawadahili vipi kama hakuna mwalimu na mwisho wa siku tunataka wafanye mitihani na wafaulu mitihani yao. Hili suala linakuwa ni gumu kwa kweli na nadhani ifike wakati muafaka sasa tuangalie kwa jicho la kipekee suala la kuongeza walimu shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumzia pia kuhusu suala la elimu kuwa chini ya TAMISEMI. Ni maoni yametolewa na Wabunge wengi na pia Kamati pia imezungumzia hili suala ifike mahali sasa, suala la elimu lijitegemee kama elimu. Itakuwa rahisi ku-monitor na itakuwa rahisi vilevile kufuatilia, ufuatiliaji wake itakuwa tunajua ni nani yuko accountable na hili suala. Mwisho wa siku ndiyo tunaongea shule hazina walimu, ukienda kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu anakwambia siyo la kwangu liko TAMISEMI, lakini ingekuwa chini ya Wizara moja inakuwa rahisi na uwazi pia ungepatikana ukaonekana na kujua ni namna gani tunaangalia suala la elimu kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeongelewa ni suala la adhabu ambayo imetolewa mwaka jana baada ya mitihani kuibiwa. Kilichofanyika kwenye shule za private ni kama uonevu. Shule za private baada ya mitihani kuibiwa, mitihani imerudiwa na shule za private zimefungiwa haziwezi kufanya mitihani kwenye shule zao. Wanafunzi inabidi watoke shule moja waende shule nyingine wakati wa kufanyia mitihani, lakini kwenye Wilaya ya Chemba, Halmashauri ya Chemba ni shule pia zimefutiwa mitihani lakini kwa sababu ni shule za Serikali, bado wao wanafanya mitihani kwenye shule zao. Naomba Mheshimiwa Waziri akija kujibu atuambie hii adhabu imetokana na nini na kwa nini kunakuwa kuna double standard. Shule za Serikali zinapewa adhabu tofauti, shule za private zinapewa adhabu tofauti, Mheshimiwa naomba ukija ku-wind up utuambie ni nini kinapelekea suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hiki kitabu cha ripoti ya wizara, page namba 146 naomba nisome, kinaandika, kuandika muhtasari wa lugha ya Kichina kidato cha tano na cha sita ambayo inafundishwa katika shule za sekondari kumi na sita, zimetajwa shule hapo. Naomba ifike mahali tuwe na kipaumbele tujue tunataka nini. Kama mpaka leo…
MWENYEKITI: Malizia, malizia!
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia. Kama mpaka leo hatuna vitabu vya darasa la kwanza mpaka la tatu kwenye shule za primary, hatuna Mtaala ambao unatuelezea kwenye shule za msingi, sasa inakuwaje tunaanza kuanza kuandika Kichina na tunatengeneza muhtasari wa South Sudan wakati hapa penyewe Tanzania ambapo darasa la kwanza mpaka la tatu hawana vitabu mpaka leo.