Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naunga mkono hoja hii. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na uongozi wote wa Wizara hii kwa kuiongoza vyema Wizara hii na mengi yameonekana kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii iongezewe bajeti, hasa katika kuboresha miundombinu katika shule za msingi. Nyumba na madarasa yaliyojengwa kabla ya Taifa kupata uhuru yamechakaa sana na mengi kubomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Wanging’ombe pamoja na Mbunge tumehamasishana kujenga maboma ya madarasa na nyumba za walimu. Kwenye Ilani ya CCM 2015 - 2020 imeelekeza kushirikisha nguvu za wananchi na Serikali itapeleka mchango wake katika bajeti ya TAMISEMI na Wizara. Fedha zimekuwa zinatengwa lakini zimekuwa hazipelekwi kwenye Halmashauri husika. Naomba Wizara iliangalie jambo hili ambalo wananchi wametekeleza wajibu wao. Wilaya ya Wanging’ombe mpaka Oktoba, 2018 inahitaji shilingi bilioni moja kukamilisha maboma katika Sekta ya Elimu ikiwepo sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wameongelea suala la uhaba wa walimu, ninazo shule zaidi ya 20 zenye walimu chini ya watatu kwa shule zenye madarasa hadi darasa la saba. Naomba Serikali iajiri walimu na itoe mgawanyo sawa. Nimeona shule za mijini zina mlundikano wa walimu kwa kisingizio cha kuolewa, kukaa karibu na hospitali na kadhalika. Shule zilizo vijijini zimesahauliwa. Naomba jambo hili lirekebishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alipofanya ziara Mkoa wa Njombe, Aprili, 2019, ametoa maelekezo kwamba majengo yaliyopo Kijiji cha Soliwaya, Wanging’ombe ambayo yalitumiwa na wasimamizi wa ukarabati wa barabara ya Nyigo – Makambako – Igawa yaanzishe Chuo cha VETA Wilaya ya Wanging’ombe. Halmashauri ya Wanging’ombe imemwandikia barua Mheshimiwa Waziri juu ya suala hili na nakala iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu, ninayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Wanging’ombe wanataka kujua, hili agizo la Mheshimiwa Rais litatekelezwa lini? Naomba Mheshimiwa Waziri wakati unaahirisha bajeti yake aseme kitu, wananchi wa Wanging’ombe wasikie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa namwita Mheshimiwa Waziri Comrade kwa jinsi alivyo sikivu kwa hoja za Wabunge na ninayo imani kuwa katika hili atalitengenezea utaratibu; ili litekelezwe wapewe, uwezekano. Tayari Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wameshaiandikia Halmashauri ya Wanging’ombe utayari wao wa kukabidhi majengo hayo kama tulivyoomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wameongelea kuhusu hoja ya kuboresha utaratibu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuo Vikuu ambao umeleta malalamiko na kiasi fulani kinawabagua wahitaji. Kwa kuwa fedha hizi ni mkopo na utatakiwa kurudishwa, kigezo cha kuangalia aina ya shule walizosoma hakina tija kwa sababu walio wanafunzi wanaopata ufadhili wengine wazazi wao wamekosa uwezo wa kuwapeleka vyuo vikuu. Naomba sana wanafunzi wote wapewe mikopo hata kama viwango vitatofautiana, lakini kuwakatalia kabisa kumesababisha watoto wengi kukosa elimu ya vyuo vikuu.