Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu Mheshimiwa Prof. Ndalichako na Naibu Waziri, Mheshimiwa Ole Nasha na Makatibu kwa hotuba yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi nzuri sana inayofanywa na Serikali hii ya Awamu ya Tano ikiwemo ukarabati wa shule kongwe nchini. Ongezeko la mikopo elimu ya juu, ukarabati wa ujenzi wa vyuo nchini na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata ufafanuzi kwa mambo yafuatayo: ukarabati wa shule ya Lugalo Sekondari Mkoa wa Iringa. Shule hii inafundisha pia watoto wenye uhitaji maalum. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha shule hii inapatiwa kipaumbele katika ukarabati wa miundombinu ikiwamo na ujenzi wa uzio kwa sababu wanafunzi wenye uhitaji maalum wanasoma kwa shida sana? Naipongeza Serikali kwa kupeleka vifaa kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie Sera ya Elimu ya kubadili mitaala mara kwa mara bila kuwapatia mafunzo walimu. Changamoto hii ni kubwa sana. Serikali inaweka mkakati gani wa kuhakikisha kabla ya kubadilisha mitaala waalimu wapatiwe mafunzo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wetu wengi wanafanya kazi nzuri katika mazingira magumu. Je, nini mkakati wa Serikali kutoa motisha kwa walimu wa shule zinazofanya vizuri kwenye matokeo ya Kitaifa? Ni vema zingeandaliwa tuzo maalum ili kuleta hamasa kwa shule na walimu wengi kufanya vizuri. Sambamba na hilo, walimu wamekuwa na changamoto kubwa sana ya upandishwaji wa madaraja kwa walimu walioajiriwa kuanzia mwaka 2012 - 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH);ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha inatenga pesa ya kutosha ili tafiti ziweze kufanyika? Kwa sababu maendeleo ya kisayansi na teknolojia ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi katika Taifa lolote lililoendelea tunategemea sana kiwango cha ugunduzi na ubunifu unaotokana na elimu bora inayotolewa. Vijana wetu wamekuwa na ubunifu mbalimbali, sijaelewa Serikali inawasaidiaje wabunifu au wagunduzi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mkurugenzi, ameweza kusimamia vizuri sana japo kuwa uangaliwe utaratibu wa kutoa mikopo watoto yatima waliokuwa wanasomeshwa na mfadhili, uwepo utaratibu wa kuwatambua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.