Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii. Kwanza niishukuru sana Serikali, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu. Profesa Mbarawa nakuamini sana na nakuheshimu sana. Katibu Mkuu wa Wizara hii namheshimu sana na namwamini sana kwa sababu ya utendaji kazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitazungumzia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria peke yake. Tarehe 5 Februari, 2016, niliuliza swali, lilikuwa linasema hivi: “Je, ni lini mradi wa ujenzi wa bomba la maji ya Ziwa Victoria kutoka Magu, Sumve, Malya utaanza?” Tarehe 5 hiyo, Serikali ikasema: “Kazi ya upimaji pamoja na usanifu itakamilika Aprili, 2016 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017 baada ya usanifu kukamilika”. Kwa maana hiyo, usanifu umeshakamilika, mradi huu ulitakiwa uanze mwaka wa fedha 2016/2017. Cha kushangaza, kama nilivyosema, Profesa Mbarawa nakuheshimu sana, Katibu Mkuu, nakuheshimu sana na hasa tunaposimama sisi Wabunge wakongwe humu ndani na huwa hatupendi kusimama na kuanza kulaumu lakini hii inasikitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha zaidi, kwenye kitabu chako hiki, ukurasa wa 155, umetenga shilingi milioni 200. Unasema, shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Mji wa Malampaka, Sumve na Malya. Najiuliza, kwa mtu mwenye akili yake timamu kabisa, maji unayatoa Ziwa Victoria mpaka Malampaka kwa shilingi milioni 200? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha huwezi ukasema ni za usanifu ni za ujenzi. Sasa shilingi milioni 200 unajenga choo au unajenga mtandao wa mabomba kutoka Mwanza, Ihelele, Magu, Sumve, Malya, Malampaka kwa shilingi milioni 200? Mheshimiwa Waziri, with due respect, hebu tuangalie sasa mambo haya mengine jamani haya, hivi hawa wataalam wetu hawa wanatusaidia au hawatusaidii? Unatenga shilingi milioni 200, usanifu umeshakamilika, no doubts, sasa hizi shilingi milioni 200 Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa, Katibu Mkuu, Dkt. Mkumbo ni za nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, niombe sana kwa kweli mliangalie suala hili. Hata kama ungekuwa ni wewe leo, Waziri na Waziri mwingine tu, kwa hali kama hii, hivi unaweza ukasimama ukasema naunga mkono hoja, naunga mkono bajeti, kwa milioni 200 zinakwenda kufanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wataalamu wako mradi huu ni wa siku nyingi muuangalie. Ukitazama miradi mingine iliyoanza na imekamilika, huu ukaachwa, Maswa, Itilima, Bariadi, Busega imeshakamilika na Magu uko njiani kwenda kukamilika. Huu sasa mmeweka kama kisiwa, Jimbo la Sumve na Malampaka, tumewakosea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ahadi hii siyo ya leo. Alikuja Rais wa Awamu ya Nne, pale Ngudu, Waziri Mheshimiwa Maghembe alikuwepo na akaambiwa kwamba mradi huu tunataka ukamilike mwaka 2015 lakini haukukamilika. Akaja Waziri Mheshimiwa Lwenge, mradi haukukamilika, akaja Mheshimiwa Kamwelwe na nimekaa naye na nimekwenda mpaka ofisini kwake anasema mradi huu utaanzia Fela - Sumve – Malya - Malampaka, kwenye kitabu hiki mnakuja kutenga shilingi milioni 200!

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, hivi mnataka Mbunge kama mimi mzoefu humu ndani nisimame na kupiga kelele kila siku humu ndani? Hata ile heshima tu, Mheshimiwa Mbarawa nakuheshimu sana lakini tutazame basi suala hili. Ni bora kabisa msingetenga hata senti tano, ndiyo maana nauliza hizi shilingi milioni 200 mmezitenga ni kwa ajili ya nini? Kwa sababu siyo za usanifu maana ulishakamilika siku nyingi na maeneo ya kuweka matenki yameshaainishwa, wataalamu wenu wamekwenda kule wakasema tenki litakaa hapa na mtiririko utakuwa hivi, mradi huu utapitiwa na vijiji zaidi ya 40 mpaka Malampaka, kazi imeshafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake aje na majibu ya mradi huu. Kwa sababu majibu haya ambayo anasema kazi ya upimaji tayari, ujenzi wa mradi utatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017, haya ni majibu ya Serikali, lingekuwa ni swali la nyongeza ingekuwa suala lingine. Swali la nyongeza unaweza ukalibabaisha lakini jibu hili ninyi wenyewe mmeandika kwa maana ya kwamba utafiti mmeshafanya na majibu ya wataalam mmeshaletewa na ndiyo maana mkasema mradi huu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 utaanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo siyo majibu yangu, ni majibu ya Serikali. Majibu haya pia yalitolewa humu Bungeni. Wananchi wote wa Jimbo la Sumve, Wilaya ya Kwimba na Malampaka walisikia majibu haya ya Serikali na wakashangilia, leo ni miaka minne mradi hata kuanza bado leo tunakuja kutenga shilingi milioni 200! Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana, wataalamu tafadhalini sana, mradi huu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano lakini na ahadi ya Mawaziri humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, utakapokuja kusimama kuhitimisha Mheshimiwa Waziri, uniambie mradi huu utakamilika lini. Pamoja na kazi nzuri sana unayofanya, basi mradi huu nao uingizwe kwa mwaka huu. Donyoadonyoa kila sehemu mnakoweza ili upate angalau shilingi bilioni 2 au 2.5 ili mradi huu uanze kwa mwaka huu wa fedha. Kwa sababu haiwezekani nitakapotoka hapa nakwenda kule jimboni, tumeshawaambia siku nyingi mradi huu unaanza, nikienda kule nawaambia nini hawa wananchi wa Jimbo la Sumve? Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa nawaambia nini kwamba huu mradi ni kiini macho, mbona hautekelezwi, leo tunatenga shilingi milioni 200?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuwa upande mwingine huko labda ningesema lakini niiombe sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali yangu sikivu, kama nilivyosema kwamba nawaheshimu sana Mawaziri na wataalamu, mradi huu naomba upangiwe utaratibu wa kuanza kwenye mwaka huu wa fedha 2019/2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini niseme kwa sababu nawaamini, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)