Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema yeye ambaye ametupa zawadi ya uhai, ametupa zawadi ya afya, ametupa zawadi ya maji, ametupa zawadi ya ulinzi, na hakika tunasafiri na kurudi kwa sababu ya ulinzi wake. Mungu wetu ni mwema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tena kuchukua nafasi hii niweze kumuweka kila mmoja wetu hapa mikononi mwa Mungu aweze kuwatetea nakuwalinda kwenye Majimbo yenu kazi zenu ziweze kwenda salama.
WABUNGE FULANI: Ameeen!
MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Lakini zaidi ya yote tuombe maombi rasmi kwa ajili ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, hakika kabisa tumepata chuma, tumepata jembe, lakini tumepata baba yeye hakika ana upendo, ana huruma, anafanya kila kitu ili mradi kuhakikisha Watanzania tukoa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba apate kibali kwa watu wote wanaume, wanawake jina lake liwe sukari midomoni mwa watu, jina lake liwe chumvi na ulinzi wa Mungu uwe juu yake kwa jina la Yesu. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Ameen.
MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua pia nafasi hii niweze kumkumbuka Mheshimiwa Dkt. Reginald Mengi mfanyabiashara mashughuli pia tukikumbuka katika bajeti yetu ya maji yeye ndio aliyeanzisha maji ya chupa Kilimanjaro, yeye ameanzisha ITV mambo mengi tu amefanya, ana huruma anakula na watu wenye shida, watu walemavu, kwa hivyo amefanya kazi nzuri Mungu aiweke roho yake mahali peponi.
WABUNGE FULANI: Ameen!
MHE. DKT. MCH. GETRUDE P. RWAKATARE: Tunaomba pia kwa ajili ya faraja katika familia yake, tunaomba kuwe siku zote na amani Mungu atende na hakika msiba huu uishe salama kwa Utukufu wa Bwana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwisha kusema hayo ningependa niweze kutoa pongezi maalum kwa Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa kwa ajili ya kazi nzuri na timu yako mnayoifanya katika Wizara hii ya Maji. Kwa kweli tunaona mabadiliko makubwa na pia tunaona kwamba mko wasikivu katika mambo ambayo tunawashauri mnafanya na tunaona kwa kweli hata kule kwetu Kilombero kuna mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nijikite kwenye maji safi na salama hakika kabisa mnajua maji ni kila kitu na lengo letu ni kumtua mwanamke ndoo ili aweze kupumzika maji yafike nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano natoka Mkoa wa Morogoro kuna Mito 177 hiyo mito ni ya kudumu sio ile mito ya kukauka, pia katika Wilaya ya Kilombero ambako natoka pia kuna mito 38 ya kudumu na sio mito ile ya kukauka, tukijumlisha tuna mito mingi. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi hawajafikiwa maji safi na salama inabidi wakachote mtoni, inabidi wakatafute ni shida. Lakini nilikuwa naomba katika bajeti hii Mheshimiwa Waziri tunaomba utuhurumia watu wa Kilombero ya kwamba uweze kuangalia kwa maana maji yapo Mungu ametupa neema tatizo kubwa ni miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ni mibovu ni mizee ya siku nyingi na vilevile watu wengi wameongezeka zamani Kilombero tulikuwa watu 300,000 siku hizi tunakaribia milioni moja kwa sababu watu wengi wanahamia kwa ajili ya kilimo na kwa ajili ya kufuata maji. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri iangalie Kilombero kwa hali ya huruma kabisa tumevumilia miaka mingi. Nakumbuka ya kwamba miundombinu ile ilikuwa kama Ifakara Mjini ilikuwa ni ya watu 7000 enzi hizo sasa hivi wako watu wengi zaidi ya 300,000 yaani Mji wa Ifakara peke yake. Kwa hivi tunaomba kwa kweli mtusaidie ili na sisi tuweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumependa pia kumpongeza Waziri ya kwamba hakika kwa utendaji wake bora na timu yake tumeona ya kwamba sasa hivi kipindupindu ni kama kinatokomea vile kwa maana kwa kweli hatusikii tena magonjwa ya kipindupindu na hiyo ni kwa sababu maji yapo watu wanapata maji ya kutosha, watu wanapata maji na ndio maana unakuta magonjwa yale nyemelezi ya siku nyingi sasa hivi yamepungua. Kwa hivi tunasema ahsante kwa kazi nzuri mnayoifanya muendelee mbele ila zingatia Kilombero iipe kipaumbele cha peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tena nichukue nafasi hii nikiangalia kwamba sisi tunasema Kilombero ni ghala la chakula au Morogoro ni ghala la chakula lakini pamoja na kwamba Mungu ametubariki na mito 177 kimkoa, mito 38 Kilombero lakini ulimaji wa kilimo cha umwagiliaji ni percent 2.7 tu, maji yapo tatizo lile lile ni miundombinu mtusaidie kwa sababu sisi hatuna shida kama mmeweza kuchota maji kutoka kwenye maziwa mkawapelekea watu ni rahisi zaidi kama watu wana mito kila kitu kipo ni miundombinu tu kuwapelekea watu. Tena hii inakuwa ni kama ulinzi wa vyanzo vya maji kwa sababu kama watu watapata maji ya kutosha wana haja gani kuharibu vyanzo vya maji wale ndio wanakuwa walinzi wetu. Kwa hivyo tujitahidi kutoa maji ya kutosha ili watu wale wasiwe waharibifu wa vyanzo vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu nilikuwa napongeza Serikali kwa ajili ya mradi mkubwa wa Stigler’s Gorge kwa kweli ni mradi mzuri hakika kabisa utatupa umeme wa kutosha na hata ziada lakini ninavyoona kwa uharibifu wa bonde la Kilombero itakuwa ni ngumu ule mradi kuweza kwenda smoothly kwa sababu watu wengi wamevamia vyanzo vya maji. Kwa hivi dawa ni ile ile tufanye juu chini kwa uwezo wote kama ikiwezekana tukisambaza maji kila mahari watu waweze kupata maji ya kutosha kwa matumizi yao, kwa matumizi labda ya wanyama wao hakika tutaweza kuufanya ule mradi wa Stigler’s Gorge uweze kumalizika vizuri na hakika utakuwa Baraka kwa Tanzania nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ningependa pia kuwapongeza kwa ajili ya sehemu ambazo hazina maji naona mnasaidia kuweka visima lakini tatizo kubwa ni uangalizi management ndio inapungua kwa hivi tunaomba muimarishe kwenye upande wa management kwa sababu watu wengi wanakuwa wanaharibu ile miundombinu kwa hivi mwisho unakuta maji hayawafikii watu sawasawa kwa sababu wengine wanachukua njiani, wengine wanafanya hivi tuangalie pia management yetu katika wizara yetu ili hakika maji tunayowapelekea watu yawafikie na yaliwafikia ni ulinzi na kama ulinzi pia na hapo tunaweza kuwa tuna save pesa badala ya kupoteza pesa. Kwa maneno haya machache ningependa kuunga mkono hoja mia kwa mia na Mungu awabariki. (Makofi)