Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukupongeza wewe na pia kwa kuwapongeza Mawaziri; Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kusema ukweli wanahangaika sana, wanafanya kazi sana, miradi ya maji imeongezeka, maji yameongezeka, lakini tatizo moja bado watu wanahitaji maji. Ninavyoongea sasa hivi, ni asilimia 64.8 ya wananchi wamefikiwa vijijini na asilimia 80 mijini wamefikiwa na maji. Kwa hiyo, watu bado wanahitaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikileta mfano mmojawapo kwa Mkoa wangu wa Morogoro, ambao ni mkoa uliojaliwa ambao una mito mingi sana, lakini mpaka sasa hivi sehemu nyingi za Mkoa wa Morogoro wana matatizo ya maji. Kwa mfano, nikija kwenye Mji mdogo wa Gairo, Malinyi, Vijiji vya Morogoro Vijijini, Mvomero pamoja na Kilosa bado wana matatizo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa maji ambao ni wa Manispaa Morogoro ni tatizo mpaka sasa hivi kwani umechukua muda mrefu. Ni kweli naamini Serikali inajitahidi na imesema kuwa kuna Euro milioni 70 ambayo itafadhiliwa itasaidia pamoja Serikali pamoja na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), lakini tatizo ni kuwa mpaka sasa hivi umechukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri wanajua tatizo la Morogoro na tatizo la manispaa, nilishaongea na Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge wameongea naye na amekiri kuwa kweli ni tatizo. Naomba atuambie tufanyeje Mkoa wa Morogoro hususan manispaa ili upungufu wa maji uweze kwisha na wananchi waweze kupata maji. Ninavyoongea hivi, Kola A, Kola B na Mkundi hawapati maji kabisa na wale Kata zinazopata maji hazipati maji ya kutosha, wanapata maji pungufu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atujibu tufanyaje kama kuna uwezekano wa kuona tufanyeje ili waweze kupata maji waweze kuchukua hatua hiyo tukiwa tunasubiri huo mradi mkubwa unaoshirikisha Bwawa la Mindu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka mitatu sasa hivi imepita tunajadili kuhusu kuongeza tozo ya maji kutoka Sh.50 kwa lita mpaka Sh.100 lakini mpaka sasa hivi bado utekelezaji ndio tatizo. Humu Bungeni tulishapitisha, lakini tatizo ni utekelezaji, sijui kwa nini; Mheshimiwa Waziri naomba atujibu. Naamini kuwa kama tungekuwa tumeongeza hiyo tozo au tumechukua njia nyingine ya kuongeza huo Mfuko wa Maji wa Taifa tungekuwa tumeweza kupata maji mengi ya kutosha na hasa maji huko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inathibitishwa kuwa mwaka huu Aprili, fedha zilizotolewa kwa miradi ya maendeleo asilimia 67 zilitoka kwenye Mfuko wa Maji na asilimia 17 tu zimetoka kwenye vyanzo vingine vya maji. Naomba waweze kutueleza tutafanyaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Ujenzi wa Bwawa la Kidunda tangu nimeingia humu Bungeni nasikia ujenzi wa Bwawa la Kidunda, ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Naomba kujua ingawaje na leo wameweka ujenzi wa Bwawa la Kidunda, lakini inaonekana kuwa bado hakuna hela na bado hakuna mfadhili. Kupanga ni kuchagua, naomba tuone tufanyaje kwani kwenye Bwawa la Kidunda linasaidia sana kuongeza maji kwenye Mto Ruvu; Ruvu Chini na Ruvu Juu pamoja na megawatt 20 za umeme pamoja na maji ya umwagiliaji. Kwa hiyo, nafikiri na barabara ya kutoka Ngerengere kwenda mpaka Kidunda. Naomba na yenyewe iweze kupewa kipaumbele hili jambo la Kidunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini yaani huyu ni mfadhili mkubwa sana. Naishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini, ila ninachoshauri ikisimamiwa vizuri na ikapewa hela ya kutosha, naamini kuwa itafanya kazi nzuri na maji yataweza kuongezeka Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, nikiongelea Morogoro, vyanzo vya maji vingi vimeharibika. Tulikuwa na Misitu ya Uluguru, maji zamani na ninyi mnajua ilikuwa inaimbwa kuwa maji yatiririka milimani Morogoro lakini sasa hivi nenda hakuna maji yanayotiririka; vyanzo vimeharibika, mito inakauka, mito inakuwepo wakati wa mvua. Kwa hiyo, hii ni kama kokote kule, kwa hiyo naomba katika vyanzo vya maji waendelee kutoa elimu tuone wakisaidiana pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu kutunza vyanzo vya maji. Vyanzo vya maji sera zipo, naomba sera zitiliwe mkazo kusudi tuweze kupata maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa uvunaji maji. Miongozo na sera zilishatolewa kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi lakini sera hazitekelezwi. Naomba kwa kusaidiana na Wizara zingine, hii nasema nina uhakika nayo kuwa zilishatolewa, kwa hiyo naomba sana waweze kutekeleza na kusimamia hizi sera na miongozo kusudi uvunaji wa maji hasa kupitia kwenye mapaa ya majumba kwenye taasisi na nyumba ya mtu mmoja mmoja iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa kulipia maji kabla ya kutumia (prepaid). Prepaid ni mfumo mzuri, huu mfumo hausumbui, kwenye ziara zetu tumekutana nao Arusha na Kishapu, watu hawasumbuliwi. Kwa hiyo, nashauri kuwa kwa kusaidiana na TAMISEMI na Wizara zingine, huu mfumo wa prepaid uweze kutumika kusudi watu waweze kutopata matatizo wakati wa kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya maji huchukua muda mrefu kukamilika kwa sababu fedha zinazotolewa hazitoshi, tumeona mpaka Aprili ni asilimia 51 tu imetolewa. Kwa hiyo, nashauri kuwa hela zote ambazo zitapitishwa za maendeleo ziweze kutolewa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha naamini ananisikia kusudi tuweze kupata maji, maji ni muhimu, maji ni uhai; naomba sana fedha itolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji Chalinze ni wa muda mrefu ambao huu Mradi wa Maji Chalinze Awamu ya Tatu umesimama, mkandarasi alishindwa na mpaka sasa hivi bado hajatafuta mkandarasi mwingine. Mheshimiwa Waziri wa Maji afanye juhudi sana ili tuweze kupata mkandarasi mwingine kwani huu mradi wa Chalinze unasaidia hata Vijiji vya Morogoro ikiwemo Kidugalo, Ngerengere pamoja na vijiji vingine vya Chalinze. Mtiririko wa fedha za miradi ya maendeleo naomba utiliwe mkazo kusudi ziweze kutolewa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ukusanyaji wa maduhuli, imejitahidi kukusanya maduhuli kwa sababu kufikia hadi Machi imekusanya asilimia 81. Kwa hiyo, naamini kuwa ikijitahidi kukusanya maduhuli hata miradi mingine itaweza kuendelea kuwa mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naipongeza Serikali kwa miradi mikubwa yote inayotekelezwa ikiwemo mradi wa Lake Victoria ambao unaleta maji mpaka Tabora, Uyui, Shinyanga na mahali popote. Wanafanya vizuri ila naomba wajitahidi wananchi bado tunahitaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)