Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Naomba nianze kwa kuipongeza sana Wizara. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wengine kwa kazi nzuri kwa kweli ambayo tunaona mnaifanya. Hata ukiangalia michango ya Waheshimiwa Wabunge toka nimekuwa Mbunge kwenye Wizara ya Maji kipindi cha bajeti, kidogo hii bajeti ya 2019/ 2020 imejikita kushauri Wizara iweze kuboresha yale ambayo hayakukaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Wizara kwa kutusaidia mradi mkubwa wa maji pale Geita Mjini. Nilichokuwa naiomba tu Wizara, ijaribu kuangalia, kwa sababu huu mradi sehemu unapowekwa, lile tanki kubwa likiwekwa vizuri linaweza kumaliza kabisa matatizo ya maji Geita Vijijini na Geita Mjini. Kwa hiyo, ni vizuri upembuzi yakinifu ukafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, huwa napata taabu sana, najiuliza sijui watu wengine huwa wanafanyaje; nimejaribu kuona Wizara ya TAMISEMI kwa Mheshimiwa Jafo, imeanzisha TARURA; pamoja na changamoto ilizonazo, lakini kiukweli tunaanza kuona mabadiliko yanayofanyika kule vijijini. Najaribu kuangalia hata Wizara ya Afya, Mheshimiwa Ummy amefanya vizuri sana. Tumejenga hospitali, zahanati, vituo vya afya, magari, kila mtu kiukweli tunaona kazi zinafanyika. Tatizo, najiuliza huku kwenye Wizara ya Maji kuna mchawi gani?

Mheshimiwa Waziri, lazima tukueleze ukweli. Mheshimiwa Rais anapozunguka kila siku anakueleza kuna wezi, hushughuliki nao; anakueleza, Wizara imeoza, hushughuliki nao; Waheshimiwa Wabunge humu, nimemsikia ndugu yangu Mheshimiwa Keissy jana amesema kuna mwizi kaiba, haushughuliki nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu naomba nitoe ushauri wangu, hata kama tungeongeza shilingi 200/=, hii Wizara ina wezi, zitaenda kuliwa. Ukimsimamisha kila Mbunge humu ndani, kila atakayesimama ana mradi wa maji lakini umepigwa; kila anayesimama humu, atasema mimi nina mradi, lakini umepigwa.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na mradi wa Chankolongo kwa dada yangu Mheshimiwa Lolesia toka mwaka 1978, umekamilika mwaka huu. Tuna mradi kwa Mheshimiwa Hussein Nassor Nyang’hwale, umepigwa mabilioni, umekamilika term hii. Kila Mbunge atakayesimama hapa ana mradi lakini umeibiwa. Sasa ninachouliza Waheshimiwa Wabunge tunataka kubebesha mzigo wananchi wetu mara kwenye simu, mara kwenye mafuta, tukaongeze hela kwa watu wanaotuibia hela, haiwezekani. Hayo ni mawazo yangu, haiwezekani. Tutafute kwanza mchawi wa hii Wizara. Profesa fukuza wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli tuseme tu wazi, alifumua Mainjinia nchi nzima. Leo TANROADS imesimama, ilikuwa na wapigaji. Sasa wewe kila siku Mheshimiwa Rais akienda huko, kisima; jana nilikuwa naangalia kwenye TV, Mheshimiwa Rais kasimamishwa huko aliko Mbeya watu wanalalamika kisima kimechimbwa kwa shilingi milioni 475. Kuna Mkurugenzi, kuna engineer na ziara mnaenda.

Mheshimiwa Spika, nashauri Waheshimiwa Wabunge, tusijaribu kuongeza hela, hizi hela ni nyingi sana. Tusijaribu kabisa. Kama tumetumia leo shilingi bilioni 300 na kitu, hii kitu haiwezekani kuwaongezea wezi hela, tutafute kwanza mchawi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kule vijijini mimi huwa najiuliza, Maprofesa wetu na Mainjinia, ukitoka hapa kwenda Mwanza utaona madaraja zaidi ya 1,000. Madaraja kazi yake ni kupitisha maji; maji yanaachwa tu yanasambaa yanaenda kupotea maporini. Ikija hela ya utafiti, watafiti wanaenda ku- drill kwenye milima ambako hakuna maji. Tunakosa maji na hela zimelipwa, haiwezekani. Naomba kabisa, suala la kuongeza hela shilingi 50/=, kama Waheshimiwa Wabunge tutajaa kingi hii ya kukubaliana naye, anayebeba mzigo ni wanyonge walioko kwetu. Kuna watu wanaishi kwa kipato cha shilingi 5,000/=, analima mchicha, ukamwambie akatwe shilingi 50/= anampigia mtu njoo ununue mchicha wangu shambani, hiki kitu hakiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba, Profesa anafanya kazi vizuri sana, Profesa Mkumbo anafanya kazi vizuri, Naibu Katibu Mkuu Engineer jamani, mkishindwa term hii labda tufute tu hii Wizara. Kwa sababu mimi najiuliza, hili suala kuanzia Profesa Mwandosya alishindwa maji, akaja Prof. Lwenge akashindwa, akaja Profesa Maghembe akashindwa, hebu jaribuni basi na darasa la saba. Mimi nitaziba mitaro tu, yatajaa maji kwa watu wote humu ndani. Hiki kitu hakiwezekani. Serikali mjiulize mara mbili. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana jana nilikuwa nasikia ndugu yangu Mheshimiwa Mboni hapa analia, ooh, Mheshimiwa Mbarawa tupe maji, Mheshimiwa Aweso tupe maji, Mkumbo tupe maji. Huyu atatoa maji wapi? Angekuwa Mheshimiwa Mwijage na Mbunge wa Bukoba wangetoa maji. Hawa watu wa hapa Singida utatoa maji, hayo maji yana chumvi, haiwezekani. Nilichokuwa naomba, tuangalie kwanza tatizo tulilonalo ndani ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, hakuna sehemu ambayo Mheshimiwa Rais anapata shida kubwa ya maswali na Waheshimiwa Wabunge tunadhalilika kwa sababu ya maji.

Mheshimiwa Spika, natoa mfano, kwenye Wilaya yangu nilikuwa na mradi huo niliosema wa Chankorongo, tumejenga miaka 20 na kitu hauishi; mara tanki linapasuka, mara linafanya hivi. Akaja Mheshimiwa Jafo, nikamwambia mimi ni mkandarasi wa darasa la saba, lakini nina wasiwasi na huyu engineer, hebu tukague cheti chake. Huyu engineer gani anatengeneza bwawa linafumuka? Tulipokagua tukakuta ana cheti cha environmental. Tukafukuza, maji yameanza kutoka. Hivi Profesa unataka ufundishwe design gani?

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tusijaribu kuingia kingi ya kutoa shilingi 50/=, hakuna 50 inayotoka, wananchi wetu ndio tutakaowapa mzigo. Kama tunataka kuongeza shilingi 50/=, lazima tuangalie anayeongezewa mzigo ni nani? Sisi Waheshimiwa Wabunge tunavaa suti, tuna mshahara mzuri. Kuna watu kule wanauza mchicha, wanauza dagaa, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu wazuri sana, sipigi debe, mimi natoka Kanda ya Ziwa. Kuna engineer anaitwa Sanga kule, miradi yote inayoshindikana kutoka Halmashauri anapewa, anakesha vijijini kule, kamaliza mradi wa Lolesia, kamaliza Chato, kamaliza mpaka Musoma. Engineer Sanga, kwa nini watu wazuri kama hawa wasipandishwe vyeo ili uzuri wake ukaonekana nchi nzima? Kuna watu wabovu kabisa wamekalia madaraka, hela zinatumwa Halmashauri halafu tena zinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameenda Lindi amekuta Mhindi ameshalipwa hela mradi hautoi maji. Alivyosema nyang’anya Passport, watu wameanza kushughulika na hela zililipwa. Chalinze hivyo hivyo hela zimeliwa; Morogoro, kila mahali, halafu tukaongeze tena hela ndugu zangu. Ukienda kwa Mheshimiwa Keissy hela zimeliwa.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hili suala la kuongeza hela, tuondoeni hayo mawazo Waheshimiwa Wabunge, tushughulike na hela tulizonazo. Hizi shilingi bilioni 600 zikienda zote; na ushauri wangu kwenye Serikali, ili kuondoa hii kesi, toeni hela kwa muda muafaka. Hizi shilingi bilioni 600 zikitolewa kwa muda muafaka, watu wote watajaa maji.

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo ushauri wangu. Nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Haya, ushauri huo.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.