Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu lakini zaidi kwa maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwenye page yake ya 2, Waziri anakiri kwamba maji yana mchango mkubwa kwa maisha ya watu, kwa maendeleo ya uchumi na jamii. Kinachoshangaza Serikali haioneshi kuipa kipaumbele Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hata bajeti ambazo tunapitisha hapa, bajeti ya mwaka 2018/2019 tulipitisha shilingi bilioni 673 lakini kwenye hotuba Waziri anasema mpaka Aprili zimeenda shilingi bilioni 344 ambayo ni sawasawa na asilimia 51 tu na hizi zote ukiangalia sanasana zimetoka kwenye Mfuko wa Maji. Watanzania tumekuwa tukihangaika na maji, wengine wanapoteza maisha wakienda kutafuta maji wanaliwa na mamba, akina mama wengine wanabakwa na ndoa zinaharibika lakini haya yote Serikali haioni ni muda muafaka sasa wa kuweza kuwekeza kwenye Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya watu. Waziri ameendelea kukiri kwamba kiasi cha mtu anachotumia maji kimepungua kutoka zaidi ya 7,600 mpaka 2300 lakini hamna mkakati ambao unawekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niombe Wabunge, pamoja na kusema kwamba tupitishe hili Azimio la shilingi 50, sasa tuitake Serikali kama vile ambavyo inafanya kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, inapeleka hela hata ambazo zingine hatujapitisha hapa Bungeni iweze kuipa kipaumbele Wizara ya Maji ili once and for all tuwekeze kwenye miundombinu ya maji vijijini na mijini, tu-solve hili tatizo ili sasa huu Mfuko ambao tunaupigania ubaki kufanya maintenance ya ile miundombinu ambayo tumeweka vinginevyo hatuwezi kufikia hata uchumi wa viwanda bila maji. Naomba kabisa kama Bunge tuitake Serikali sasa ije kwanza na bajeti yenye uhalisia ambayo imesheheni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine nataka kuzungumzia kuhusu takwimu ambazo Waziri anatoa za Watanzania wanaopata maji. Vijijini mnatuambia asilimia 64 na wanasema wanazi-drive hizi kwa kuangalia zile center za kuchota maji, sijui ni vijiji vipi hivi.

Mheshimiwa Spika, mimi vijiji ambavyo nimepitia Tanzania hata kama mnafanya kwa average, sijaona vijiji ambavyo unaweza uka-generalize ukasema Watanzania kwa sasa wanapata maji kwa asilimia 64 na target mwaka 2020 mnataka muwe mmefikisha maji vijijini kwa asiimia 95. Tunavyoongea kufikia mwaka 2020 tuna mwaka mmoja tu lakini mnaweza mkaona uhalisia Wabunge wakisimama adha za maji wanazosema Majimboni kwao. Sasa hii asilimia 95 vijijini tutaifikia kweli au tumekuja hapa tunaongea tuna- document inapita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi mijini mnasema kwenye miji ni asilimia 64, mimi kwangu pale Tarime na nimekuwa nikisimama nalalamika pamoja na kwamba ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Tarime lakini ni kata mbili tu ambazo zina maji kati ya kata nane na hizo kata mbili sio wananchi wote ambao wameunganishiwa. Tunataka Serikali ituambie mikakati ambayo ina dhamira ya dhati ya kutekeleza Sera ya Maji ya Mtanzania kupata maji ndani ya mita 400. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia kusema tukiamua kuwekeza kwenye maendeleo ya watu inawezekana. Kama vile ambavyo Serikali ya Magufuli/CCM mmeamua kuwekeza kwenye miundombinu ambayo ni maendeleo ya vitu na tunaona kweli mmewekeza kwa zaidi ya asilimia ambayo tumepitisha hapa hivyo hivyo tupeleke kwenye maji ili tutatue na tutekeleze Sera ya Maji kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie sasa kuhusiana na Jimbo langu la Tarime. Tuna miradi mingi ya maji; kuna mradi wa Gamasala ambao umekwama ungeweza kusaidia kule Nyandoto. Waziri, Mheshimiwa Kamwelwe alienda akaona na nimeuliza swali hapa ukasema sasa fedha zimepatikana lakini mpaka sasa hivi navyoongea mkandarasi bado hajapelekewa fedha. Mheshimiwa Waziri unapokuja ku- windup naomba mtuambie ule Mradi wa Gamasala unaenda kukamilika lini na ni lini mkandarasi atarudi site?

Mheshimiwa Spika, kingine ni kuhusu Bwawa la Nyanduma. Mmekuwa mkitenga shilingi milioni 300 na nashukuru na hapa mmetenga tena lakini mnatenga shilingi milioni 300 kwanza hazikidhi haja lakini tutashukuru zikija zitaweza kufanya ukarabati wa kuhakikisha kwamba wananchi wa Tarime hawapati yale maji ambayo wanayapata sasa hivi ambayo ni mchafu, unaweza ukafikiri ni ubuyu, chai ya maziwa imewekwa pale. Kwa hiyo, hizi shilingi milioni 300 ambazo mmezitenga hapa tungependa kujua sasa hivi mtazileta au itakuwa kama kila mwaka zinavyotokea kwenye kitabu lakini haziji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nishukuru, nimeona mmetenga zaidi ya shilingi bilioni 600 ingawa hazijanyambulishwa ambazo zitakuja Tarime, napenda kujua hizi zinaenda kwenye nyanja zipi, nimejaribu kutafuta sijaona. Maana najua tunawadai visima 23 ambavyo vipo tangu mwaka 2017/2018 na 2018/2019 lakini hazijaenda mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, pia niliuliza swali hapa ukanihakikishia kwamba umewaambia DDCA waende maana wanasubiria fedha, ukasema umeagiza waende mara moja, imepita takribani sasa hivi mwezi sijawaona kule Tarime. Napenda nihakikishiwe hawa DDCA wanaenda lini maana ulisema fedha zimeshapatikana ili sasa zile kata za pembezoni za Nyandoto, Nkende, Kenyemanyori na Kitale waweze kupata maji wakati huo sasa tukisubiria Mradi wa Ziwa Victoria ambao nao pia nashukuru mmeuweka hapa kwa zile fedha za India.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wakati tunasubiria huo mradi mkubwa kutoka Ziwa Victoria ambao utapeleka maji Rorya na Tarime, nitake kujua hivi visima 23 ni lini vinaenda kuchimbwa maana vipo tangu mwaka uliopita na uliniahidi. Kwa hiyo, mkitufanyia hayo walau zile taasisi mbalimbali ambazo zipo ndani ya Mji wa Tarime kuna magereza, hospitali na biashara nyingi maana Tarime ni mji ambao unakua wataweza kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, samahani, nataka kujua maana tusije tukasahaulishwa, Wabunge wote tunajua msisimko ambao tulikuwa nao Bunge la bajeti lililopita la mwaka 2018/ 2019. Kulionekana kuna ufisadi mkubwa sana, hata mimi mwenyewe nilisimama nikataja ufisadi ule wa mkandarasi kule Geita. Hata siku zile Mheshimiwa Eng. Kamwelwe akasema kwa kweli mimi naogopa hata msinipe tena hela mpaka tuhakikishe huu ufisadi ambao mmeutaja hapo umefanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tujue sasa kabla hatujawapa hizi hela ambazo Mheshimiwa Kamwelwe aliogopa kuzipokea, ule ufisadi wote ambao tuliutaja kwenye miradi mbalimbali ya maji hapa nchini mmechukua hatua zipi ili sasa muweze kutuaminisha sisi kwamba tunaweza kuweka fedha nyingi kwenye hii Wizara na zisipate ubadhirifu wowote ule. Kinyume na hapo hatuwezi kuja tu tunakaa hapa tunapitisha fedha zinaenda, zinatumika vibaya, leo ukikagua miradi mingi maji hayatoki, lakini fedha zinaenda tu, hii itakuwa siyo ufanisi wa Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwa kusisitiza kabisa na kwa nia ya dhati kabisa kwamba kama nchi maji ni mojawapo ya kichocheo cha maendeleo. Bila maji wananchi watakuwa wanapoteza muda mwingi kuliko kufanya kazi zao za shughuli za maendeleo. Bila maji safi na salama, tunakunywa maji watoto wetu wanapata vichocho. Ukishapata kichocho ina maana unaipelekea Serikali gharama kubwa ya kuweza kumtibu huyu mwananchi, kwanza anaacha kufanya kazi lakini pia inakuwa ni gharama kwenye hospitali zetu ambazo pia tunajua hazina madawa ya kukidhi mahitaji. Kwa hiyo, mwananchi asipopata tiba mbadala pia ina maana tunampumzisha kwa amani. Tukiwekeza kwenye maji tutaenda kuondoa haya yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuishia hapo lakini naunga mkono hoja ya upinzani, yale yote ambayo yamewekwa mle tuyachukue na tuyafanyie kazi na michango yote ya Wabunge ambayo ina tija tuifanyie kazi kwa maendeleo ya taifa letu, ahsante sana. (Makofi)