Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji na pia nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya. Nianze kwa kuipongeza Wizara nikianza kumpongeza Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na watendaji kwa kazi ambayo wanaifanya. Ninaimani kabisa kwamba wakiwezesha pesa za kutosha wataweza kufanyakazi nzuri zaidi kuliko ambavyo sasa hivi wanafanya.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi zangu hizo, ningependa kuchangia maeneo mbalimbali yanayogusa katika eneo langu. Kwanza nianze na ule Mradi wa Maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Mtwara Mjini. Mradi ule ukitekelezwa utapeleka maji katika vijiji vya Mtwara Vijijini zaidi ya 30, lakini mpaka sasa hivi mradi huu umekuwa ukisuasua. Ukikutana na watendaji wanakwambia mradi upo, wakati mwingine ukikutana na Waziri anasema huu mradi haupo. Kwahiyo ningependa Waziri atakapokuja kutoa majibu atuambie Mradi huu waKutoa Maji Mto Ruvuma upo au haupo na kama haupo sisi wa Mtwara Vijijini vile vijiji ambavyo vilipangiwa kupata maji kutoka katika mradi huu vitapelekewa maji kwa mradi gani?

Mheshimiwa Spika, katika kupitia bajeti nimekuta sehemu imeandikwa kwamba mradi wa kutoa maji mto Ruvuma kupeleka Mtwara kwa gharama ya shilingi bilioni moja. Kwa kweli imenitia wasiwasi hivi kweli unaweza ukatoa maji Mto Ruvuma ukafikisha Mtwara Mjini kwa shilingi bilioni moja au hii ni token tu kama mradi utakuwepo wataongezea pesa au bado wako katika kusuasua uwepo au usiwepo. Kwahiyo Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo pia nataka ufafanuzi ni suala la mradi wa maji katika Mji wa Mtwara na Babati, yenyewe imetengewa Sh.2,500,000,000 kwa kweli kwa miji miwili na Mheshimiwa Waziri ametembelea katika Mradi wa Mtwara nilikuwepo, ameona changamoto zilizopo, maji yanayokwenda katika Mji wa Mtwara zaidi ya kuyatibu hayachunjwi, yanakwenda na rangi yake ileile. Mheshimiwa Waziri kazi ni kubwa inayotakiwa kufanyika pale.

Mheshimiwa Spika,tunayomiradi ya maji ambayo ni mibovu, tunao Mradi wa Kitere, ambao unatakiwa upeleke maji katika Vijiji vya Chemchem,Nakada, Chekelenina Lilido, lakini mradi huu ulijengwa muda mrefu na sasa hivi unahitaji ukarabati mkubwa, lakini nimeangalia kwenye hii bajeti sijaona. Tunao Mradi waMbuo – Mkunwa,Mradi huu unaitwa Mbuo- Mkunwa lakini Mkunwa hata hayo maji hawajayaona, upanuzi kila siku utafanyika, utafanyika. Mradi huu tumewapa MTUWASA lakini pamoja na kuwapa MTUWASA hatuoni kasi wala manufaa ya kuwapa wao, tulitegemea baada ya wao kupewa huu mradi, basi vijiji vyote vinavyotakiwa kuhudumiwa na mradi huu wangekuwa wameshafikiwa.

Mheshimiwa Spika,nimpongeze na nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa Mradi wa Lyowa kwasababu amenihakikishia kwamba pesa zimeingia, nami nitafuatilia kujiridhisha kama pesa ya kununua pump imekwenda ili mradi huu uweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika,tunayo changamoto ya upatikanaji wa maji ya uhakika katika Mradi wa Mbawala Chini, ambao wenyewe unatakiwa kuwahudumia wananchi wa Manispaa ya Mtwara, Mbawala lakini na Kata ya Nanguruwe na wenyewe mara nyingi umekuwa unapata uharibifu wa mitambo, lakini hata usambazaji wake na wenyewe haujafikia kiwango ambacho kinahitajika.

Mheshimiwa Spika,tunazo kata ambazo kwa kweli zinachangamoto ya upatikanaji wa maji kwa kiasi kikubwa, Kata ya Lipwidi, Kata ya Mangopachanne, Kata ya Madimba na Kata ya Tangazo tunao mradi, lakini kuna vijiji ambavyo bado havijafikiwa na mradi huu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri nimeangalia kwenye bajeti kuna miji kuna miradi, nimesoma, nimeangalia katika mkoa wangu, naona Mradi wa Makonde, nimeuona Mradi wa Mangaka nimeiona miradi mingi, lakini mradi haswa wa kuhudumia Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara nimejaribu kuutafuta mradi hasa wa kusema huu ndiyo utasaidia kuondosha kero ya maji katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini sijauona.

Mheshimiwa Spika,Mheshimiwa Waziri alipotembelea Mkoa wa Mtwara aliuona Mradi wa Maji wa Msanga Mkuu, aliona changamoto ya maji kubadilika rangi, ambapo hata wananchi wanaogopa kunywa maji yale kutokana na rangi na alituahidi kwamba angeleta pesa za kuwezesha mradi ule ili lijengwe chujio dogo la kuweza kusafisha yale maji. Nimejaribu kuangalia humu sioni chochote.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumza, inaonesha Wizara baadhi ya Halmashauri au Mikoa hawajui ilivyokaa au ikoje. Nimeangalia ukurasa wa 163, nikaangalia pesa ambazo zimeenda kwenye mikoa kwenye miradi mbalimbali, nimesikitika kuona kwamba wilaya yangu kwa Wizara ya Maji inaonesha kwamba wamenitengea pesa nyingi, lakini kiuhalisia hizo pesa haziji kwenye wilaya yangu. Inaonesha wilaya yangu nimetengewa shilingi milioni 943 ambapo shilingi milioni 20 zinaenda Kilambo, milioni 70 zinakwenda Msanga Mkuu, milioni 93 zinaenda Nanyamba - Malanje na milioni 630 zinaenda Mradi wa Maji wa Ujenzi wa Chipango, Namyomyo, Manyuli,Mnavirana Mkaliwata. Hivi vijiji huu mradi ni wa Wilaya ya Masasi DC, zaidi ya shilingi milioni 630.

Mheshimiwa Spika, sasa huko wakikaa wanaonesha kwamba milioni 600 imeenda Mtwara DC, kuna milioni 128 ambazo ni za maji Nanyamba - Mbembaleo. Kwahiyo kiuhalisia Mtwara Vijijini imepata milioni 90 peke yake, lakini hapa inaonesha zaidi ya milioni 900 imeenda Mtwara Vijijini.Hii si haki na naomba hizo pesa ambazo zinaonesha milioni 600 zimekwenda Mtwara Vijijini wakati zimeenda Wilaya ya Masasi, basi watafute popote zinapopatikana ziweze kuja Mtwara vijijini ili tuweze kuondoa changamoto. Kwa sababu Masasi kama Masasi wamewatengea pesa zao, tena nyingi bilioni 1.8, halafu wakachukua milioni 600 badala ya kupeleka Masasi ikaonesha wamewapa bilioni 200 na nukta zake kule wamekuja kuziweka Mtwara Vijijini, kama zilikuwa zinafichwa sijui, lakini sidhani kama ni kwa bahati mbaya. Naomba hizo milioni 600 nilizokuwa nimetengewa zije zote Mtwara Vijijini na Masasi wawawekee kwamba wamewapelekea bilioni 200.

Mheshimiwa Spika, napenda nirudie tena kuwaomba, wakati wa kuandaa hizi bajeti na takwimu zetu na vijiji tujiridhishe, kwasababu nitaonekana mlalamishi, nimeletewa milioni 900, wakati kiuhalisia nimeletewa milioni 90. Nisikitike sana kwa hilo na nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu anijibu pesa hizo ambazo zilistahili kwenda Mtwara Vijijini zitapelekwa lini na miradi ya Mtwara Vijijini itatekelezwa vipi?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)