Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Maji. Niungane na Wajumbe waliotangulia kuwapongeza viongozi wetu; Waziri wa Maji, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri, Katibu Mkuu - Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu - Eng. Kalobelo, Wakurugenzi wa Wizara kwa maana ya Mkurugenzi Mkuu ma Mkurugenzi Msaidizi, Eng. Christian na watendaji ambao wako chini yao kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niipongeze Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini, Mijini na Usafi wa Mazingira (RUWASA). Tunaamini kwamba hii itakuwa ni suluhisho pia katika kuharakisha kupeleka huduma ya maji vijijini kama ambavyo tumeona mafanikio tulipoanzisha TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuanzisha ni kitu kimoja na ufanisi ni kitu kingine. Tumeona kuna upungufu wa watumishi; ili RUWASA waweze kufanya kazi vizuri lazima kuongeza watumishi lakini watumishi wenye sifa na ambao ni makini. Ili RUWASA waweze kufanya kazi yao vizuri na Mfuko wa Maji Taifa ni lazima kuongeza fedha ili waweze kutekeleza miradi ya maji kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jinsi ambavyo Mfuko wa Maji wa Taifa jinsi ambavyo wameweza kufanya vizuri, asilimia 67 ya miradi iliyotekelezwa imetokana na fungu ambalo liko kwenye Mfuko huu. Kwa hiyo, kwa kutenga fedha za kutosha kwenye kwenye Mfuko hii, itapelekea kutekeeza miradi mingi ambayo imekwama. Niungane na Wajumbe waliotangulia kusema kwamba shilingi 50 iongezwe; inatoka kwenye mafuta, mitandao ya simu, inatoka wapi, jambo la msingi ni tuongeze fedha katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwashukuru. Tumepokea shilingi milioni 208 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kulipa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya vijiji 10, Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Jimbo langu naweza nikagawa makundi ya miradi katika sehemu tatu, kama sio nne; miradi ya vijiji 10 ambayo imechukua sasa zaidi ya miaka mitano haijakamilika. Tumeomba shilingi milioni 400 certificate kwa ajili ya kulipa wakandarasi waendelee kumalizia miradi hii. Niombe Wizara hizi fedha zilipwe haraka iwezekanavyo ili waendelee kukamilisha miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa miji sita katika Mkoa wa Kagera. Ni mradi ambao ulianza kusanifiwa na Mhandisi Mashauri tangu miaka ya 2014. Huyo Mhandisi Mshauri akashindwa kuendelea na kazi akawa terminated. Nawashukuru kwamba sasa amepatikana Mhandisi Mshauri mwingine amesharipoti site tangu juzi. Kwa hiyo, niombe azingatie mkataba wa miezi nane ambao amepewa ili mradi huu uweze kutekelezwa kwa sababu uta-cover eneo la Mji wa Ngara Mjini lakini pia na vijiji saba ambavyo vimeongezwa; Vijiji vya Mrukurazo, Nyakiziba, Nterungwe, Buhororo, Kumtana, Kabalenzi na kadhalika. Kwa hiyo, niombe kwamba usanifu wa mradi huu uweze kufanyika kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mradi wa vijiji vitano. Nishukuru Wizara kwamba tayari mmetoa go-ahead, no objection kwamba waanze kutangaza. Vijiji vya Mkalinzi; Mrugina, Kata ya Mabawe; Kanyinya, Kata ya Mbuba; Kumbuga, Kata ya Nyamagoma; na Ntanga. Naomba tunapoanza kutekeleza bajeti Julai basi taratibu zote ziwe zimekamilika ili vijiji hivyo ambavyo vina adha ya maji viweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe kwenye fungu hilo kwa sababu tuna chanzo cha Mto Ruvubu na kutumia Mlima Shunga ambao ndiyo mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera, vipo vijiji katika kata hilo ambapo ndipo maji na mlima uliopo. Vijiji vya Kenda, Kagali na Mlengo visiachwe katika mpango huu, viongezwe ili wananchi ambao wapo katika eneo hilo wasiachwe nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, kwenye Mto huohuo wa Ruvubu na mlima huohuo ambao mradi huu ulikuwa ndiyo suluhisho kwa ajili ya vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara. Kwa sababu Mhandisi Mshauri atakuwa yuko site kwa ajili ya kuanza kusanifu mradi huu na chanzo ni hichohicho na mlima huohuo ambao utaweza kusambaza maji kwa mserereko wilaya nzima na hata nje ya wilaya. Ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais wakati namwomba mwaka juzi, 2017, alivutiwa kwa sababu alikuwa anaona ni mradi mkubwa unaweza ukatoa huduma kwa Wilaya ya Biharamulo, Wilaya ya Kakonko, tena wakati ule nilisema unaweza ukaenda mpaka Bukombe na Mbogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mradi huu muuchukulie kama mradi mkubwa ambao unaweza ukatoa suluhisho kwa maeneo mengi ambayo hayana vyanzo vya uhakika vya maji. Kwa hiyo, niombe katika bajeti hii, huu mradi wa Mheshimiwa Rais ambao tulimuomba uende sambamba na huu mradi wa miji sita kwa sababu chanzo ni hichohicho na sehemu ya ku-supply ni hiyohiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka kwenye mlima huu upo mlima mwingine mkubwa ambao kimo chake kutoka usawa wa bahari ni kama mita 1,400 hivi, huu wa Shunga ni 1,820, kwa hiyo huu Mlima wa Msumba ambao upo katika Kata ya Nyakisasa, Tarafa ya Rulenge, unaweza ukasambaza maji kwa mtiririko baada ya kupokea maji kutoka kwenye mlima huu kwa vijiji vyote vya Tarafa ya Rulenge na Tarafa ya Mrusagamba lakini ukapeleka hata Wilaya jirani ya Kakonko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe mradi huu Wizara muuangalie kama ni mradi mkubwa unaoweza ukatatua changamoto ya maji katika Wilaya ya jirani pia. Mhandisi Mshauri kama anao uwezo basi ni afadhali hii anayoifanya sasa hivi ya usanifu wa mradi wa miji sita aweze kuongezewa phase two kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa mradi huo mkubwa wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ambao unaweza ukawa ni suluhisho kwa maeneo hayo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeona jitihada za Wizara kwenye Wilaya ya Temeke, hususan maeneo ya Kurasini, pale ambapo tayari mmeshalipa nafikiri zaidi ya shilingi milioni 600 kama fidia kwa ajili ya kutengeneza sewage system. Naomba tu-adopt sasa technology mpya ya recycling. Kwa sababu bado ku-discharge maji machafu kupeleka ziwani au kwenye mito ni kuendelea kuchafua mazingira lakini tunaweza tukaendelea kufanya recycling ukawa ni mkakati mahsusi kwenye majiji, miji na halmashauri za miji kwa sababu hata haya maji safi na salama yanatokana na maji machafu tu isipokuwa tunayafanyia treatment yanakuwa safi na salama. Kwa hiyo, tukiandaa sewage systems, mahali pa kupokea yale maji machafu halafu tuka-recycle tutajikuta kwamba tunaendelea kutunza mazingira lakini pia na kutunza maji. Hata kama itakuwa ni miaka mingapi ijayo tutakuwa na uhakika kwamba hatupungukiwi maji kwenye vyanzo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niendelee kuwapongeza Wizara na niombe tuzingatie haya ambayo Kamati imeshauri kwa sababu Kamati ya Bunge ndiyo Bunge. Kwa hiyo, haya ambayo wameshauri, kama hii ya kuongeza fedha ili kuondoa changamoto hii ya fedha kwenye Mfuko huu wa Maji tuizingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishauri kwamba Wizara hii ya Maji lazima ifanye kazi sambamba na Wizara zingine; Ofisi ya Makumu wa Rais (Mazingira) na Wizara ya Ardhi ili kuhakikisha kwamba tunatunza vyanzo vya maji. Tunapotunza vyanzo vya maji maana yake ni kwamba tunaendelea kuwa na uhakika wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepitisha Sheria ya Watumiaji wa Maji, yapo maeneo ambayo lazima tuwe makini tunapoanza kutekeleza sheria hii hasa kwenye vyanzo kwamba watu wawe mbali na vyanzo vile vya maji. Hata kama kuna mahali ambapo pipes za maji zimepita, kuna umbali ambao hakuna shughuli za kibinadamu zinazotakiwa zifanyike katika maeneo hayo. Ni vizuri wakati tunaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo lakini wananchi waelimishwe zaidi ili waweze kujua sheria hizi na waweze kuzingatia ili wawe ndiyo watunzaji wa miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)