Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa hii nafasi. Kwanza naomba nianze kwa kuunga mkono hoja, pili naomba niipongeze sana Serikali kwa kuitendea haki Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo na nchi kwa ujumla. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Profesa Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Kalobelo na watendaji wote ndani ya hii Wizara ya Maji kwa namna ambavyo wanatekeleza majukumu ya Serikali, na sisi Waheshimiwa Wabunge wanatupokea Wizarani, wanatusikiliza na kutekeleza yale ambayo tumeyaomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba niipongeze Serikali kwa kuuweka Mji wa Mpanda katika fedha za mkopo wa kutoka nchi ya India, takriban zaidi ya milioni 500, yaani kwenye fedha za dola. Ninatumaini maji yakifika katika Mji wa Mpanda yatafika pia na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na kuhusiana na changamoto ambayo Mheshimiwa Waziri alizieleza katika hotuba yake ya bajeti. Changamoto ya kwanza ambayo aliieleza ni kuhusiana na utekelezaji wa miradi ambao haujafanyika kutokana na changamoto ya kifedha, kutopata kwa wakati au kwa uchache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali isikilize kwa makini na ilichukue jambo hili. Haiingii akilini, sisi Waheshimiwa Wabunge tunawakilisha vijiji takribani vijiji elfu kumi na mbili mia nane na kitu, ndio tunawakilisha hivyo vijiji; na ndio ambao tunajua changamoto zilizoko katika maeneo yetu ya jimbo na vijiji vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi kule wanapenda sana na watafurahi sana kama watapata maji, katika mikutano yetu hakuna mkutano ambako utakwenda usipewe kero ya maji; akina mma hadi wanalia, na inatia uchungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya 2020 kwa vijijini ni kwamba tufike asilimia 85, ni jambo ambalo tumebakisha miezi tisa ya utekelezaji, hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wote na Kamati kwa ujumla; kwamba kuongeza fedha ambayo itakuwa ring fenced iingie kwenye Mfuko wa Maji ili kutunisha na tuwe na fedha ya uhakika ya kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo ya maji; aidha kwenye mafuta au kwenye mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano uchukue asilimia kati ya 2 mpaka 5 anapo-recharge kwenye aidha MB za internet au kwenye muda wa maongezi tutapata fedha za kutosha, kilio kina wenyewe, hatuwezi kutegemea zaidi mikopo na misaada kutoka nje ya nchi, lazima tujikamue sisi wenyewe. kuna watu wanasema hapa kuongeza tozo hizi unaongeza mziko kwa wanachi. Hivi nyumba yako ikivuja jirani atakutengenezea? Lazima tufanye sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Serikali, Juni 2016 tulihitimisha bajeti, lililalamikiwa sana, Juni, 2017 lilisemwa sana, Juni 2018 limesemwa sana. Hebu ifike mahali tulikubali, jinsi gani wananchi wetu wanavyoteseka, wanatoka saa tisa, saa kumi kuchota maji ya kwenye madimbwi; wanakoswakoswa kuliwa na fisi na simba; sisi ndio tunajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ilichukue, kama kuonesha u-serious wa jambo hili, wananchi wanavyoumia na sisi ndio tunaowawakilisha, ndio tunawasikiliza, kama kuna namna ya kuonesha kwamba liko serious kweli kweli; kama ukisema kutembea uchi humu ndani niko tayari kutembea uchi kuonesha kwamba liko serious; I am ready. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Abraham aliambiwa atoe sadaka akamtoa mwanaye isaka baadaye akaambiwa chinja kondoo huyu hapa. Kama kuna namna yoyote ya kutoa sadaka ili kuonesha kwamba jambo hili lina umuhimu sana mtuambie tufanye; lakini tunaomba Serikali, tozo hii ni ya umuhimu kuliko jambo lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijijini tunachukua asilimia 65 ya wananchi walioko vijijini, watu takriban milioni 25, Mheshimiwa Waziri umeandika kwenye hotuba yako, lakini ndio watu wanaoongoza kwa kuteseka kupata maji safi na salama. Mfano mzuri Halmashauri ya Nsimbo, as I speak now 41 percent ndio wanaopata maji safi na salama, 41 percent. Bilioni 351 asilimia 51 tunaisoma kwa sababu tuliikopa kwa wakandarasi kufanya certificates zikawa Wizarani, ndizo zimelipwa, hiki ndicho kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kwamba tumepeleka pesa, utaratibu kwa ajili ya kudhibiti (control) na ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma alichangia kwamba tukiongeza fedha ndiyo upigaji unaongezeka, no! Serikali imebadilisha utaratibu, una-design mradi unaleta wizarani wana-approve unarudisha, unatangaza ndio unapata mkandarasi anafanya. Sasa hivi mmesema kwamba akifanya kazi work execution ya 30 percent ndiyo u-raise certificate, fedha inapigwa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya RAS lazima ikakague ndiyo certificate ije wizarani na wizarani wanarudi maeneo mengine wanaenda wanakagua ndiyo wana-release fedha kwenda kwenye halmashauri. Sasa upigaji, sawa upigaji unaweza ukawepo hao ni binadamu lakini not to that extent kama ilivyokuwa kule nyuma. Niombe sana maji ni uhai na maji ni siasa, let us do everything lakini kwenye maji please the government accept this fifty or other charges. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la usanifu wa miradi; tu-improve kwenye usanifu wa miradi. kuna mahali mtu ana- design mradi tumeshakutana kwenye Kamati ya LAAC, mradi umeenda kwenye mlima halafu tena tuna-raise up maji yakishindwa kwenda ni hoja. Mkandarasi anajenga according to the line na wengine wanapendekeza force account kwenye miradi ya maji, naomba niseme not everything unaweza kufanya kwa force account. Tumefanya kwa vituo vya afya lakini technicalities nyingine kwenye maji huwezi ukatumia force account; mambo ya reversion, pressure na nini, utaokota tu mtu barabarani aje ajenge kama kwenye nyumba, haiewezekani, hatuwezi kufanya kitu kwa force account. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuna ahadi ya Serikali kwenye Jimbo la Nsimbo, alivyokuja Waziri Mkuu katika Mkoa wa Katavi, Serikali iliahidi kutoa maji Kolongo kuleta Katumba lakini pia maji Kolongo yapo Nsimbo yanalisha manispaa hatunywi hata tone. Kata ya Mtapenda iliahidiwa maji, naambiwa kwenye kanadarasi iliyopo sasa hivi haipo, kwa nini. wananchi wamesema hawataruhusu maji kupita Mtapenda kwenda Ilembo. Kwa hiyo, naomba wizara muhakikishe Kata ya Mtapenda inakuwepo na tenki la zamani lipo na ni kilometa nne tu na ndiyo njia hiyo hiyo. maji hayatapita Mtapenda ya Ikolongo kwenda sehemu yoyote lazima Mtapenda wanywe maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wataalam; hii ni changamoto na Waziri amesema lakini tuombe muendelee kuwajengea uwezo na tukisema mtaalam huyu ana-dilly-dully na nishukuru tu tumeanzisha RUWASA, tumeondoa ukiritimba kidogo kwenye manunuzi. Nimewahi kuingilia manunuzi kwenye halmashauri yangu, Mkurugenzi akawa na wasiwasi na nini na nini, tukasema what’s for? Tumevunja mkataba wa kwanza na huu, watu wanatumia hela zao certificate mpaka wizarani ndio watu walipwe, tuwe na mkandarasi ambaye yupo committed kwa hiyo ndio kidogo ikaenda. Kwa hiyo, ukiritimba huu naipongeza sasa Serikali kuanzisha RUWASA kwa hiyo, tunatumainia sasa kasi tunayoisifu kwenye TARURA, sasa ndio itaenda kwenye RUWASA, natumainia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, RUWASA ili iweze kufanya kazi kama tunavyosifu TANROAD na TARURA, lazima wawe na cash flow ya kutosha kwa hiyo naomba mruhusu sana hii tozo ya 50 kwenye mafuta au twende kwenye mawasiliano. Hilo ndilo ambalo tutaliunga mkono na tutakubaliana wote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukubwa wa bajeti sio tija, tija ni utoaji wa…

MWENYEKITI: Malizia!

MHE. RICHARD P. MBOGO: tija ni utoaji wa fedha. Bajeti ya wizara hata ikiwa bilioni 450 lakini 100 percent zinapatikana, tunatekeleza miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niombe mamlaka zote ambazo zinakusanya fedha vizuri, ziondoke kwenye huu mgao, mgao tupewe halmashauri za vijijini ambazo hatuna mamlaka na hatukusanyi fedha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, asante sana. (Makofi)