Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kidogo hoja hii ya Maji. Namshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii kwa sababu ni Mungu pekee anayetupa haya yote. Naishukuru Serikali sana kwa kuliangalia jambo la maji na hasa katika Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu na mikoa mingine kame kwa kutuletea maji ya Ziwa Victoria, ahsante sana Serikali kwa jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Igunga tumekuwa na tatizo la maji la siku nyingi kwa sababu ni wilaya kame, lakini wametuletea mradi huu ambao kwa kweli utatusaidia sana. Mradi huu utafikia kwenye Jimbo la Igunga kata kama sita hivi ambazo ni Kata ya Nanga, Mwamashiga, Bukoko, Itumba, Mbutu na Itunduru. Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuangalia hali ya maji katika jimbo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema Wabunge waliotangulia kuna miradi mingi sana ambayo imetekelezwa, ilitekelezwa ikafikia kiwango cha kufanya kazi, lakini ikatelekezwa ama kwa sababu chanzo cha maji hakikupatikana ama miundombinu haikujengwa vizuri. Kuna mfano wa Mradi wa Maji Kata ya Itunduru, kule Jimbo la Igunga, mradi huu ulijengwa mwaka 2010. Miundombinu ya kupeleka maji kwenye kata hiyo na hasa Makao Makuu ya Kata ilijengwa vizuri ikiwepo tank pamoja na mabomba lakini chanzo cha maji kilikosekana, hata hivyo, mkandarasi alilipwa akaondoka. Wananchi tangu wakati huo leo mwaka wa kumi wanailalamikia Serikali mmetutengenezea mradi tunaangalia tu mabomba tunaangalia tank.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsumbua sana Waziri wa Maji juu ya jambo hili na naomba niliseme tena, naomba Mheshimiwa Waziri katika kutekeleza Mradi wa Ziwa Victoria atupelekee maji pale ni kuunganisha tu na tumepeleka hata design pamoja na bajeti ni shilingi milioni 100 tu, ukitoa hizo unaweza ukafanya adjustment na mradi wetu ukapata maji, sio mbali sana kutoka bomba kuu la maji. Wananchi wa Itunduru wataishukuru sana Serikali, watafurahi sana na kwa kweli wataipenda Serikali yao, tafadhali sana namwomba Mheshimiwa Waziri anisikilize juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mambo mengi ya kusema sana, lakini naomba niseme Wilaya ya Igunga kuna sehemu ambazo hakuna maji ya chini, kwa hiyo kuna vijiji ambavyo tumechimba maji tumepata na tumepewa katika bajeti hii baadhi ya vijiji kuchimba maji. Hata hivyo, sehemu zingine kata nyingi kama kata saba hizi ambazo hazifikiwi na huu Mradi wa Ziwa Victoria hazina maji ya chini, tunajenga vibwawa, tumejitahidi. Namshukuru sana Mheshimiwa aliyekuwa Mbunge kabla yangu mimi alisaidia sana kujenga mabwawa kwenye kila kijiji na hasa kata na mimi nimeendeleza jambo hilo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo. Naiomba Serikali, naomba sana Wizara, wanapoangalia maeneo ambayo yana matatizo ya maji sana kama mikoa ya kwetu ile ambayo ni kame, basi watusaidie kutoka kwenye Mfuko wa Maji kutusaidia kujenga haya mabwawa madogo madogo wakati tunasubiria usambazaji wa maji ya Ziwa Victoria kwenda kwenye kila kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo la mwisho kuhusu Mfuko wa Maji. Najua Wabunge tumesema sana juu ya jambo hilo kwamba tuwaongeze huo Mfuko ili upate fedha za kutosha kama ilivyo kwenye umeme. Tunasema umeme kwenda kila kijiji na kuna fedha kule REA tumeweza kabisa kabisa, sasa kwa nini tusiwe na REA ya maji ambayo ina uwezo wa kufanya na tuseme maji kila kijiji. Kwa wananchi wetu hili ni jambo kubwa na ni tatizo kubwa sana ambalo tukiweza kulitekeleza hili tutalitendea haki Taifa hili jambo zuri sana, tuweze kuwatua ndoo wananchi wetu, akinamama wa vijijini wanahitaji kutuliwa ndoo kichwani. Kwa hiyo mimi naomba pamoja na kelele ambazo zimepigwa mwanzoni mwanzoni hapa kuomba shilingi 50 ziongezwe, nasema tu kwamba ni lazima tutafute vyanzo hata kama sio shilingi 50, basi tutafute vyanzo ambavyo tutatunisha huu Mfuko uweze kuwahudumia wananchi wetu. Serikali wakilifanya hili la maji vijijini watafanya kazi nzuri sana na wananchi watafurahi sana na wataipenda Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema, ukokotoaji wa percentage ya coverage ya maji kwenye vijiji haufanywi vizuri, Wabunge wengi wamesema na ndugu yangu, kaka yangu Chiza amesema. Kule kwetu Mwamashimba kule, Mwamakona, Mwanyalali kule na sehemu zote zile ambazo ni mbuga ambako ni ziwani hakuna maji chini, unaona calculation anasema maji asilimia 30. Kweli ukienda kule unakuta visima havina maji vyote au unakuta hakuna kisima kuna kibwawa kimoja kinachokauka lakini asilimia 30 coverage, wanafanyafanyaje? Naiomba Serikali kwenye jambo hili wafanye evaluation ya nchi nzima tena upya ili tuweze kupata percentage ya coverage ya maji inayolingana na ukweli na tukiweza kufanya hivyo tunaweza kutafuta fedha kwa sababu tutajua gravity ya tatizo lenyewe, lakini kwa jinsi hii tunaonekana kama vile maji tumepiga hatua, lakini tuna hali mbaya sana kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba niishukuru Serikali tena kwa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda Nzega, Igunga na Tabora na Katibu Mkuu aliniambia wanaweza kufikisha hata kwenye jimbo la jirani la ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu pale Shelui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana, naomba kuunga mkono hoja. Mungu awabariki sana, ahsante sana. (Makofi)