Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza natumia fursa hii kutoa pole kwa jumuiya nzima ya wafanyabiasha, wadau wa habari, wadau wa viwanda na familia ya mzee wetu, Mheshimiwa Reginald Mengi. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kimya toka Wizara hii imeanza kuchangiwa, nilikuwa nasikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu na nilikuwa napitia kumbukumbu za Bunge kuangalia michango ya mwaka 2018, nimekuta kwa sehemu kubwa malalamiko yetu Wabunge ni yale yale yanajirudiarudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiit, kwa sababu mwaka 2018 tulilalamikia juu ya ubadhirifu kwenye miradi ya maji, kuwepo na miradi ya maji isiyotoa maji na mambo kama hayo; na Serikali ikaahidi yafuatayo, naomba kunukuu maneno ya Mheshimiwa Waziri aliyoyasema: “Kuna haja ya kuunda timu ya wataalamu watakaopitia miradi yote iliyotekelezwa kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mnapendekeza. Mlipendekeza kwamba iingie Kamati ya Bunge, lakini kabla hamjafika hapo, sisi tayari tumeshaunda na kamati hii itasimamiwa na Profesa Mbwete wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iliacha au ilikataa Wabunge tusiunde kamati ya kuchunguza ubadhirifu na miradi ya maji ambayo haitoi maji kwa kisingizio cha kwamba Serikali imeunda Kamati ya Profesa Mbwete, lakini Mheshimiwa Waziri alipokuja kutoa hotuba yake Bungeni, hajaeleza hiyo Kamati ya Profesa Mbwete imebaini yapi, watu gani wamechukuliwa hatua mpaka sasa na nini kinaendelea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, naomba baada ya kuhitimishwa hoja hii nitoe notice kabisa ya kupendekeza kuundwe Kamati Teule ya Bunge ili ipitie taarifa ya Profesa Mbwete lakini iende mbali zaidi kushughulikia ubadhirifu na ufisadi wote ulioko kwenye miradi ya maji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo la kwanza. Niliomba nianze nalo. La pili ni juu ya takwimu zinazotolewa na Serikali hapa Bungeni kuhusiana na hali ya upatikanaji wa maji. Serikali inasema, kwa wastani hivi sasa, vijijini maji yanapatikana kwa asilimia 65 na mijini kwa asilimia 80. Sasa nawaomba Wabunge wenzangu, hizi takwimu za Serikali zisikubalike kwa sababu hazilingani na hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushuhuda tu wa majibu ambayo yametolewa na Serikali hapa Bungeni na Mheshimiwa Naibu Waziri, mwezi Aprili, 2019, Naibu Waziri, juu ya upatikanaji wa maji Jimbo la Kibamba ambapo alisema upatikanaji wa maji ni asilimia hii hii 80, lakini alitoa majibu ya uongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuingia kwa undani katika hili kwa sababu ya muda, naipa nafasi Serikali pengine wakati wa majumuisho, irekebishe hii kauli. Kwa sababu Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye hotuba yake ukurasa wa nane, sehemu ya tano, wameeleza kiunagaubaga kuanzia aya ya 27 mpaka aya ya 35 ushahidi wa namna ambavyo maelezo ya Serikali hayakuwa ya kweli kwa kueleza kata kwa kata, mtaa kwa mtaa, hali halisi ya upatikanaji wa maji. Nami nafahamu kwa takwimu za ukweli, upatikanaji wa maji kwa Jimbo la Kibamba haujavuka asilimia 65 mpaka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali ije ieleze ukweli na Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri wafike Jimbo la Kibamba washughulikie hayo matatizo ili upatikanaji ufike hizo asilimia ambazo wanazieleza hapa Bungeni. Hilo ni jambo la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu hali hii siyo ya Kibamba peke yake, ni maeneo mengi nchini takwimu zinatolewa siyo za kweli, hiyo Kamati Teule ya Bunge itakapoundwa, pamoja na mambo mengine ikachunguze ili zipatikane takwimu sahihi za hali ya upatikanaji wa maji hapa nchini, Bunge liweze kuchukua hatua kwa niaba ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, tunaitwisha hii Wizara mzigo mkubwa ambao kwa kweli ni mzigo wa Wizara ya Fedha. Mzigo wa fedha kutokutolewa kwa wakati kwa ajili ya miradi ya maji. Tunavyozungumza hivi sasa, mpaka mwezi Aprili, ukilinganisha kiwango tulichopitisha kwenye bajeti na kiwango cha fedha kilichotolewa, fedha ambazo Serikali haijatoa bado kwa ajili ya Wizara ya Maji, kwa miradi ya maendeleo peke yake ni shilingi bilioni 329. Kati ya hizo, fedha za ndani ambazo Serikali haijatoa mpaka hivi sasa ni shilingi bilioni 288. Sasa kama Serikali hii ina uwezo wa kujigamba inalipa fedha taslimu kwa ajili ya kununua ndege, kwa nini haitoi fedha kwa ajili ya miradi ya maji? (Makofi)
T A A R I F A
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kusainiwa kwa fedha za Washirika wa Maendeleo hakujibu haja na hoja ya fedha za ndani ambazo Bunge lilipitisha ambazo Serikali inapaswa ilieleze Bunge, kwa nini fedha hizi hazijatoka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja kuchangia hii hoja hatatoa maelezo ya kuridhisha, nitaomba nafasi kutoa hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 69(1) ili bajeti hii isogezwe mbele mpaka kwanza Serikali itimize matakwa ya kutekeleza bajeti ambayo imekusudiwa na Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye hizi fedha za wahisani, mwaka 2018 tuliambiwa maneno kama haya haya juu ya fedha za India. Tuliambia Serikali imesaini mkataba wa dola milioni 500. Ninao ushahidi hapa wa Hansard wa kiwango kilichosainiwa. Hata kwenye hizo fedha za wahisani vilevile, kwa mujibu wa utekelezaji wa bajeti, kiwango cha fedha kilichotolewa hakijakamilika kwa idadi ya kiwango cha fedha ambacho kilipitishwa na Bunge. Kwa hiyo, hapa napo ipo hoja ya kujadili na Bunge lifanye kazi ya kuisimamia Serikali ili hatua ziweze kuchukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haiwezi kutekeleza Bajeti, ni kwa nini mwaka huu vilevile Serikali imeleta hoja, ikitaka fedha nyingi zitengwe, mabilioni yale yale, safari hii imepunguza kidogo; fedha za maendeleo zimepungua kutoka shilingi bilioni 673 mpaka 610, pungufu ya shilingi bilioni 63, lakini bado fedha ziko kule kule juu. Kama Serikali inajijua haina uwezo wa kupeleka fedha, basi ilete bajeti inayolingana na mahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu, Serikali hii ingeamua kipaumbele kiwe maji badala ya ndege fedha zingetengwa kwa ajili ya maji na wananchi wangekombolewa; na kwa sababu Serikali hii inajigamba wazi wazi kabisa kuleta maendeleo ya vitu, kama ndege, badala ya maendeleo ya watu kwenye miradi kama ya maji, tiba siyo ninyi kwa sababu hamsikii tena, tiba ni Watanzania, kujiandaa kuiondoa Serikali ya CCM madarakani kuanzia kwenye uchaguzi wa mitaa, kwenye vijiji, kwenye vitongoji, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ili kuingiza kwenye uongozi wa nchi Serikali ambayo itajali maslahi ya watu. (Makofi)
T A A R I F A
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo maeneo ya kimkakati ndiyo biashara ya ndege ambayo Shirika la Ndege linaendeshwa kwa hasara, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kushindwa tu kujua namna ambavyo maji ni kipaumbele. Maji ni kipaumbele, siyo kwa sababu tu ni huduma kwa wananchi, maji ni kipaumbele vilevile kwa sababu ni huduma ya kiuchumi ambayo ingewezesha uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni kipaumbele. Naomba vilevile Wizara itakapokuja kwenye majumuisho, ieleze ni kwa nini fedha za kujenga mradi wa Kidunda mpaka sasa hazijapatikana? Kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge, ninazo kumbukumbu za Bunge hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri akijibu Bungeni kuhusiana na hoja ya Kidunda, kwa sababu ya muda naomba nisiende kwenye ukurasa, lakini alilieleza Bunge kwamba Serikali iko kwenye majadiliano na NSSSF kwa ajili ya kutoa fedha za ujenzi wa mradi wa Kidunda na kwamba akaahidi ifikapo mwezi Julai, 2018 zabuni ya Bwawa la Kidunda ingetangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sasa hivi Serikali hii isiyowekea kipaumbele miradi ya maji, inasema kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ndiyo kwanza fedha za Mradi wa Maji wa Kidunda, zinatafutwa, mradi ambao ukitekelezwa, siyo tu utanusuru watu wa Dar es Salaam na Pwani; kwa sababu pamoja na kupanua Ruvu Juu na Ruvu Chini, kwa sababu ya mabadiliko ya nchi, wakati wa kiangazi, maji Dar es Salaam hayatakuwa yanapatikana ya kutosha, ndiyo maana tunahitaji fedha kwa ajili ya mradi wa Kidunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu mradi huu utasaidia kwenye maji ya viwanda na majumbani, mradi huu ungeweza kuzalisha megawatts…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Ahsante sana.
MHE. JOHN J.MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini suluhu ni kuiondoa Serikali madarakani. Ahsanteni sana. (Makofi)