Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwanza kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii iliyopo hapa mbele yetu, hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye masuala ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali unavyoiona kama ambavyo Mheshimiwa Mnyika alianza kuongea toka mwanzo kwamba kimsingi kuna hali mbaya sana kwenye suala la maji na Wabunge wote waliosimama hapa wamekuwa wakilalamikia suala hili. Niungane na Mheshimiwa Mnyika lakini pia niungane na hotuba yetu ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuitaka Serikali irudi na kufanya marejeo kwenye hii miradi yote ya maji kwa ajili ya kupata value for money kwa sababu kuna miradi mingi imesimama na tunaamua kufanya hii kazi kisiasa, tunapeleka pesa kidogo kidogo kwenye maeneo mengi ambayo hayawezi kuleta tija kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwashukuru sana wa-missionary wa Ndanda kwa sababu bila wao eneo kubwa sana la Mji wa Masasi pamoja na maeneo ya Ndanda tungekuwa na kiu kuu. Kutokana na uvumbuzi wao uliofanywa miaka ya 1960 na marehemu Bruda Lucas, Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi, wametuwezesha kupata maji eneo kubwa, kata nane za mwanzo ambazo ni Ndanda, Mwena, Chikundi mpaka kufikia Kata ya Chigugu pamoja na Kata ya Chikukwe. Tatizo kubwa tulilonalo hapa ni ucheleweshwaji wa uanzishwaji wa mradi huu. Mradi ule umeendelea kutengenezwa pale, tumepokea mabomba tunashukuru lakini pia matenki yameendelea kujengwa kwenye lile eneo pamoja na vizimba kwenye maeneo mengi sana, sasa tatizo mkandarasi anashindwa kuendeleza ile kazi yake kwa sababu hapati pesa kwa wakati kiasi kwamba wananchi wanaanza kukata tamaa na hawajui kwamba maji wataanza kupata lini kwenye eneo hili. Kwa hiyo, bado mpaka sasa hivi wanahangaika na visima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukumbuke sisi watu wa Ndanda tuna maji mengi tu na nilishwahi kusema hapa hata siku ya kwanza kabisa naanza kuchangia nilisema kwamba tatizo kubwa tulinalo watu wa maeneo ya Ndanda kwenye hizo kata nilizozitaja ni miundombinu. Sasa miundombinu imetufikia lakini kazi hii inashindwa kukamilika zaidi ya mwaka wa pili sasa hivi kwa sababu pesa zinapelekwa taratibu. Ni bora hizi pesa zikapelekwa kwa haraka ili ikiwezekana mradi huu ukamilike tuwaondolee kero wale wananchi wa hayo maeneo niliyoyataja ikiwemo pamoja na Maparagwe na Vijiji vya Mbemba na Mbaju. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliseme hapa, Jimbo la Ndanda limegawanyika kwenye jiografia mbili; kuna upande wa Mashariki pamoja na upande wa Magharibi. Upande wa Magharibi miaka ya zamani kama mtakumbuka tulikuwa tuna miradi iliyokuwa inafadhiliwa na JICA na DANIDA. Kwa bahati mbaya sana ukienda Kata za Mlingura, Namajani na Msikisi, maeneo haya yote yalikuwa na miradi mikubwa sana ya maji na maji haya yalikuwa yanatokea kwenye Kata ya Namajani. Pale kuna visima, kwenye vile visima vinatakiwa visafishwe na kuboresha miundombinu kwa sababu mpaka pump house ziko pale mpaka sasa hivi, matenki nayo yako pale, kwa hiyo, tunahitaji kuboresha ile miundombinu pamoja na kusafisha visima kwa gharama ya karibia shilingi milioni 300. Nilivyoongea na yule mtaalam wa maji mara ya mwisho alisema hivyo lakini Serikali haijatekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa hapa wanatuletea mipango mikubwa sana wakati sisi tunahitaji maji kwa haraka tuweze kuwasaidia watu wetu. Serikali inawaza kutengeneza mabwawa na niliongea hapa wakati fulani na Mheshimiwa Waziri na nimeona kwenye kitabu hapa, ukurasa wa 79, wametaja na kijiji pekee ambacho tumepata maji siku za karibuni kwa gharama isiyozidi shilingi milioni 60. Sasa tunawaza kurekebisha mabwawa, kuna Bwawa la Lukuledi na Mihima, tunawaza kutengeneza Mabwawa maeneo ya Chingulungulu, kimsingi maji ya Mbwinji yaliyokwenda Jimbo la Ruangwa, Nachingewa yanatoka Jimbo la Ndanda, Milima ya Nangoo, kwa hiyo, tuna maji mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiomba sisi, badala ya ninyi kufikiria kuhusu kutengeneza mabwawa tupeleke miundombinu ili haya maji yanatopelekwa maeneo hayo niliyoyataja yaweze kufikia eneo kubwa la Jimbo la Ndanda tena kwa gharama nafuu sana tofauti na gharama mnazozifikiria ninyi. Tuwaombe kabisa Serikali kwamba mtakapokuwa mnafanyia kazi miradi hii mtushirikishe sisi wenyeji wa haya maeneo, tunaweza tukawafahamisha, tukawaonyesha vyanzo vizuri zaidi kuliko vile ambavyo nyinyi mnafikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine liko kwenye Kata yangu moja ya Chiwata. Kata hii kijiografia iko juu kabisa ya mlima ambako tunapaka kati ya Makonde plateau pamoja na milima ya upande wa Masasi. Bahati mbaya sana Kata ya Chiwata ndiko ambako iko shule kubwa kabisa ya sekondari na sasa hivi imekuwa A-level, shule ya Tiija lakini kuna shida kubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati tulifikiri kwa sababu mradi wa madini ulikuwa unaendelea pale na wale wawekezaji walikuwa tayari kusaidia maji kwenye lile eneo, inahitajika kama shilingi milioni 300 mpaka shilingi milioni 400 na Waziri tumeshaliongea jambo hili. Naomba nikusisitize tena, ili tuweze kupata maji safi na salama Chiwata yanayotoka kwenye vyanzo vya maji vya Kambona ambavyo mimi navijua, wewe haujawahi kufika pale, tunahitaji kupata pump, tunahitaji pia kutengeneza tenki kwenye maeneo ya Chibya Sekondari ili tuweze kusambaza kwenye haya maeneo yote na hivi ndivyo inatakiwa ifanyike mtushirikishe. Sasa mnawaza kupeleka pale maji sijui kutoka kwenye source gani wakati kuna chanzo cha gharama nafuu sana cha maji ambacho kitasaidia haya Serikali kuweza kubana matumizi kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango mwingine ni wa kupeleka maji kwenye hizo kata nilizokwambia. Kwa mfano, ukisoma kwenye hii taarifa ambayo iko kwenye ukurasa huu wa 29 nilivyoitaja hapa mwanzoni wanaelezea kuhusu Mradi mkubwa sana wa maji ya Mbwinji lakini naomba tu nikutaarifu kwamba huu Mradi wa Maji ya Mbwinji ulikuwa na andiko lake toka mwanzoni kabisa na walisema wataanza kuhudumia wenyeji wa maeneo husika. Sasa hivi naongea na wewe lakini ukienda kwenye Kata za Nanganga pamoja na mradi ambao ulifanyika kwenye eneo hilo kupeleka maji vijiji vyote, mradi uliofanywa chini ya kiwango na mkandarasi yule bado yupo amefanya ubadhirifu mkubwa lakini amekuwa akilindwa na watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana hii miradi tumeigeuza kuwa ya kisiasa. Viongozi wa kisiasa kwenye maeneo yetu ndiyo wanaopewa kusimamia miradi hii. Makusanyo yanayopatikana kwenye miradi hii watakapotumia vibaya hakuna mtu anayekwenda kuwahoji hasa wanaotokea kwenye chama tawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mradi wa maji uliopo kwenye Kata ya Nanganga haufanyi kazi kwa sabau tu yule mkandarasi alijenga chini ya kiwango, lile chujio la maji pale limeharibika, halijakarabatiwa na mpaka sasa hivi mradi huo haujapokelewa ambapo tunashindwa kupeleka maji kwenye Kata ya Nanganga kwenye vijiji vya Mkwera, Chipite, Nangoo, Lumumburu pamoja na vijiji vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Mawaziri mnapopata nafasi na nakumbuka Mheshimiwa Waziri Kamwele alipokuja alisema kabisa kwamba Bodi ya Maji inayosimami ile ambayo iliundwa na wananchi kwenye hii Kata ya Nanganga ivunjwe kwa sababu imekuwa ikifanya ubadhilifu na watu wanapohoji viongozi wetu wa Serikali za Mitaa na wengine wanawachukulia hatua ambazo sio stahiki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kweli tukIamua kwa mfano Mheshimiwa Mbunge alietoka sasa hivi anaongea habari ya shida ya maji Kwimba. Kwimba ipo karibu na Ziwa la Victoria wala sio mbali kutoka huko, sasa kama mtu aliyeko Kwimba analalamika kuhusu maji sishangai na watu wa Shinyanga na kwingine wakalalamika kwa sababu kidogo wako mbali na hili ziwa. Kwa hiyo, maeneo yenye vyanzo vya maji tuache kufikiria miradi mikubwa sana twende tukaboreshe ile miradi midogo iliyopo kwenye haya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini tuna tatizo kubwa sana la maji pia kwenye Jimbo letu la Masasi na Masasi ni nyumbani kwangu nina wajibu wa kuwasemea watu wa Masasi. Tuna shida moja tu Masasi wanapewa maji kutoka kwenye watu wa MANAWASA. MANAWASA ndio wanaosimamia chanzo cha maji cha Mbwinji, mpaka sasa hivi ninaongea na wewe ukiangalia kwenye bajeti iliyopangwa huku ndani wanasema watawapelekea maji wote huo mradi unakaribia kukamilika na najua Katibu yuko hapa anasikiliza naweza nikampa maelezo ya ziada baadaye kutokana na muda tulionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu wazi kwamba mkandarasi ambaye alipelekwa kwenda kufanya tathimini kwa ajili ya kutaka kuanza ule mradi ambao wanasema unakamilika mwezi Juni mwaka huu anashindwa kuendelea na kazi kwa sababu hana pesa ya kufanya hiyo kazi ambayo nyinyi mnasema mlishamfanyia commission ili aweze kuanza. Na hii itasaidia kupata maji safi, hata maji tuliyopeleka huko Nachingwea, Maji tuliyopeleka Rwangwa na ndio maji hayo yanayokwenda Masasi. Lakini yanazidi kuwa machache kwa sababu chujio lile sio zuri tena ni dogo liliwekwa kwa ajili ya kuzalisha maji machache pale, sasa tunahitaji kupata chujio kubwa ili tuweze kupata maji safi na salama Masasi na maeneo mengine yote yanayozunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilisema tuwashukuru sana Wamisionari bila wao huu mtandao mzima wa maji tunaoongelea hili eneo la Kata ya Mwena mpaka kufika Kata ya Chikukwe basi kungekuwa kuna shida kubwa sana. Na maji tunayotumia eneo hili ni safi na salama kwa sababu ndio chanzo cha mwanzo kabisa kabla ya chanzo cha Mbwinji kupeleka maji Masasi, kilikuwa kinatumika chanzo cha Mwena ambako ndiko yanakotoka…ahsante ninaiomba wizara pamoja na kazi nzuri wanayofanya waongeze…

MWENYEKITI: Unga mkono Mheshimiwa, mmh maji yatafikaje kama huungi mkono .

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja ya Kambi Rasmi. (Makofi)