Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru, kwanza kabisa katika mchango wangu niungane na watanzania wote na IPP Media kutoa pole kwa kuondokewa na mwekezaji makini na mahiri bwana Dkt. Reginald Mengi, naamini tunapozungumzia pengo, Dkt. Mengi ameacha pengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika historia nafikiri tukichimbua historia ni mtanzania ambaye ameacha rekodi ambayo haijawekwa na mtanzania tangu nchi hii iumbwe katika rekodi tulizonazo. Ni mojawapo ya matajiri, wapo matajiri wanaomzidi fedha lakini moyo wake na nafsi yake imefanya mengi kama jina lake lilivyo. Nathubutu kusema hata kama kuna mabaya ambayo anayo kama binadamu lakini mazuri yanafunika mara mia tano mara elfu moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nipende kupongeza bayana hotuba ya Kambi ya Upinzani na pia hotuba ya Kamati Huduma ya Jamii. Naamini Mheshimiwa Waziri na Msaidizi wake na watendaji wao wakizisoma vizuri hotuba hizi na ushauri uliotolewa nafikiri tutapiga hatua moja kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, napenda tutambue kabisa unapozungumzia afya, unapozungumzia ustawi wa jamii ndio msingi wa shughuli zingine zozote ambazo zinafanywa ndani ya nchi. Ni kama mtu ambaye ninaamini hawezi kuanza kununua tairi kabla hajanunua gari, kununua spear tairi inakuja baada ya kununua gari. Mambo yote yanayofanyika bila Wizara hii bila idara ya Wizara hii kupewa bajeti kadri tunavyozipitisha ndani ya Bunge hili tutakuwa hatuwatendei haki watanzania tunao wawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kila Mbunge anayesimama hapa ambaye amezungumza mapungufu mengi yaliyopo. Hotuba zote mbili za Upinzani pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii zimeeleza hali halisi iliyopo huko. Lakini pia tunaponzungumzia ukosefu wa fedha inasikitisha inapokwenda au inapopelekea kwamba hata pesa zinazopitishwa ndani ya Bunge hili, sasa zinapolewa pungufu kwa kweli inaonekana sisi wenyewe wasimamizi tunaosimamia Serikali au wapishi wetu ambao ndio waliokabidhiwa dhamana ya kuweza kusimamia hii mifuko na hazina fedha ya nchi hii kuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukosefu wa bajeti au kutotimilisha bajeti maana yake ni kutotimiza huduma zilizotarajiwa kwa wananchi wetu. Ninaamini huenda na hili ndiyo tatizo ambalo hata ndani ya Manispaa yangu ya Bukoba katika bajeti hii tunayoelekea kuimaliza tulipangiwa 1.5 bilioni kwa ajili ya hospitali yetu inayotakiwa kuwa hospitali ya wilaya ambayo mpaka sasa hivi ina jengo moja tu linalohudumia watu wa OPD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa tunashindwa kuiita hospitali ya wilaya au kituo cha afya, nashindwa kuelewa, sasa kwa kuwa labda imebakia miezi kama miwili hivi, nafikiri Mheshimiwa Ummy atakapokuja na Msaidizi wake mtaniambia labda miezi miwili hii fedha itatoka ili tuwe na hospitali ya Wilaya. Na katika hili nafikiri ifike mahala nchi yetu uwekwe utaratibu kitu gani kinapelekea hospitali iitwe hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Mkoa, Hospitali ya Rufaa, Zahanati, kituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiriki tuchukue hatua tuweke category kama tunataka hospitali iitwe ya Wilaya au ya Rufaa basi iwe imetimiza masharti fulani, iwe na vifaa vya aina fulani, iwe na capacity ya aina fulani isiwe ni majengo tu, kukuta bango ndio hospitali ya Mkoa, hospitali Rufaa X-ray hamna MRI hamna, madaktari hamna. Kwa kweli nafikiri ni ushauri wangu kama yanayofanyika kwenye hoteli, unapojua unakwenda five star unajua utakuta huduma ya aina gani sasa hili lipelekwe hata kwenye hospital zetu vinginevyo tutakuwa tunadanganyana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine niseme kabisa nimnufaika wa NHIF na ninawapongeza sana taasisi hii kwa afya yangu wamekuwa wadau muhimu kwa kuendelea kuwa na afya njema nawapongeza sana wamenihudumia sana. Nimekuwa nahudumiwa vizuri bila shaka kwa sababu bima yangu ni kubwa. Ambayo inaniruhusu kupata matibabu yoyote na weza nikapata madawa yoyote naweza nikapata vipimo vyoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kuwa nimekuwa nahudhuria katika matibabu pia nimegundua wananchi wa kawaida wanavyo kufa. Watu wana kufa si kwa sababu ya kile ambacho tunaambiwa kwamba bwana ametoa na bwana ametwaa. Nafikiri Bwana anatoa lakini wapanga mipango wanatwaa kwa sababu naamini asilimia 95 ya magonjwa yameshafanyiwa research namna ya kutibiwa. Sasa watu wanakufa kwa utapia mlo, watu wana kufa kwa sababu utumbo umejikunja kwa kweli naamini bwana akweli anatoa tunashukuru na tutakuwa jina halihimidiwi bali tunadhihaki jina la Mwenyenzi Mungu tukienda namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya watumishi nafikiri kuna haja ya hata kuweka category tunapojumuisha kwamba watumishi wote wasipandishwe mishahara, watumishi wote wasilipwe pesheni. Lakini naamini kuna kila sababu ya kuwaangalia watumishi wetu wa idara hii, kuna kila sababu tukianzia watu wote, nafikiri mlikwenda shule. Katika shule zetu na vyuo vyetu watu wanaominika kuchimba sana na kubundi ni madaktari, na wanasoma kwa miaka mingi tukiwapeleka jumla jumla na watumishi wengine hatuwatendei haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza watumishi wa Idara ya Afya, miongoni mwa watu wanaokwenda sambamba na kiapo chao ni watu wa sekta hii. Ni watu ambao hata wafanyiwe vituko gani wanakomaa wanatimiza viapo vyao. Hebu fikiria kuna idara, kuna sekta ambayo anaweza akaenda akachakachua cement, kwenye kujenga daraja, lakini hakuna daktari au nesi ambaye ameambiwa akupige dawa ya kiwango fulani akakudunga sindano ambayo inazidi kiwango kile ili ufe au daktari pamoja na uwezo wake wakati wa kufanya operation au kukupiga nusu kaputi ile anaweza akakumaliza. Lakini pamoja na kwamba hajalipwa mshahara, hajalipwa mapunjo anakomaa anaamua kutimiza kiapo chake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tufike mahali tuwaangalie watu hawa ili tuweze kuwatimizia haki sambamba na huduma na aina ya commitment ambayo wanakuwa nayo katika kazi yao.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Kama haiwezekani nafikiri yale masharti ambayo yaliwekwa ya watu kutofanya kazi za ziada, naomba daktari aruhusiwe kuweza kutafuta kipato cha ziada cha kufidia pato dogo mnalomlipa. Nafikiri ipo haja kubadilisha utaratibu hawa watu wakapata fursa ya kujiongezea kipato kama mmeshindwa kuwalipa sawa sawa na haki yao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiaria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lwakatare kengele ya pili ililia.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.