Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nianze kwa kupongeza sana Wizara hii kwa wasilisho wao, nikupongeze Waziri (shemeji yangu), nikupongeze Naibu Waziri (kaka yangu) lakini pia na Makatibu wote Wakuu na watendaji wa Wizara kwa kazi nzuri ambayo tunathibitisha kwamba mnaendelea kuifanya. Pia naunga mkono hoja hii iliyopo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Mji wa Kondoa imeendelea kukua na kuongeza uhitaji wa huduma kwa maeneo mbalimbali. Hospitali ya Kondoa Mjini inahudumia zaidi ya halmashauri tano, tunazungumzia Vijijini, Chemba, Kiteto mpaka Babati na Katesh wengine wengi wanategemea huduma ya Kondoa Mjini. Mara baada ya barabara yetu kumalizika, uhitaji umekuwa mkubwa kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wale watu ambao tulikadiria wataudumiwa na hospitali ile takribani 60,000 sasa imekwenda zaidi ya wagonjwa, siku hizi wanawaita wateja, zaidi ya 400,000 au 500,000, sasa tumekuwa na upungufu mkubwa sana kwanza ni suala la ambulance. Nimekuwa nikipigia kelele sana kuhusiana na kupata ambulance. Tumejitahidi tukakarabati iliyokuwa mbovu lakini tunaomba sana tupate ambulance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya barabara ile ya kutoka Dodoma kwenda Kondoa kumalizika ajali zimeongezeka, uhitaji wa wagonjwa kupatiwa rufaa kwenda Dodoma umekuwa mkubwa lakini hatuna ambulance. Mwaka jana hata Mbunge mwenzetu mmoja alipata ajali pale tulilazimika kuungaunga, unaomba Chemba, Kondoa Vijijini na ile mbovu ya kwetu kuwaleta majeruhi hapa Dodoma. Tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri na timu yako angalia Hospitali ya Mji wa Kondoa ipate ambulance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa uongezekaji wa mahitaji ya huduma hivyo hivyo hatuna X-ray. X-ray yetu imekuwa ni ya muda mrefu ni ya toka 2000, inaharibika mara kwa mara, ni ya zamani kweli kweli, inakaa hata miezi mitatu mpaka sita, sasa inatokea ajali watu inabidi kupata X-ray tu waje mpaka Dodoma. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri tuangalie kwenye hili suala la X-ray kwenye Hospitali ya Mji Kondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuipongeza Serikali yetu kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya barabara. Sasa barabara imekuwa nzuri lakini pia na ajali na watu wanaopoteza maisha wanaongezeka, mochwari yetu ni ndogo na ya zamani sana, kichumba kile ni kidogo hata maeneo ya kuoshea, fridge ni mbovu na imezeeka. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri tuangalie kwenye Hospitali yetu ya Mji Kondoa tuweze kupatiwa mochwari itakayokidhi mahitaji na haja ya huduma za afya pale Kondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mtanzamo huo huo tena bajeti yetu kwenye basket fund inatuangalia sisi watu wa Kondoa peke yake ilhali tunahudumia watu zaidi ya 400,000 au 500,000. Sasa hivi bajeti yetu kwa mwaka tupo kwenye milioni 32 wakati tukiangalia mahitaji inakwenda kwenye milioni 100 mpaka milioni 120. Hebu na hapo pia mtufikirie tuweze kuwahudumia wagonjwa ambao wanaitegemea Hospitali hii ya Mji Kondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu wa Mji wa Kondoa imegawanyika katika kanda kama tatu. Kanda ya kwanza ya Kusini, Kanda ya Kati ndiyo Hospitali ya Mji ipo pale na Kanda ya Kaskazini. Tunazo zahanati na tunashukuru Serikali tumepata kituo cha afya kimoja kwenye hii Kanda ya Kusini kwenye Kata moja Kingale. Watu sasa kutoka Ukanda wa Kusini wanakwenda kupunguza uhitaji wa kwenda mjini kwa ajili ya kufuata huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoomba tupatiwe walau kituo kingine cha afya kwenye hii Kanda ya Kaskazini katika Kata ya Kolo na jambo ambalo nimeliongea sana kwenye Bunge letu hili Tukufu ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu wananchi hawa wa kutoka Ukanda huu wa Kaskazini kutafuta huduma za afya kwenye Hospitali ya Kondoa Mji. Tukipata Kituo cha Afya, Kata ya Kolo, matokeo yake tutakuwa tumewasaidia watu wote wa Ukanda huu wa Kaskazini pamoja na Kata za Bolisa na majirani wa Sowera na kadhalika. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tuweze kupatiwa kituo hiki cha afya ili tusogeze huduma karibu kadiri ya mpango na sera zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)