Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako na kuchangia hoja hii ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwanza napenda nimpongeze Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Katibu Mkuu - Dkt. Chaula kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze kwa moyo wa dhati kabisa jinsi Serikali ya Awamu ya Tano inavyofanya kazi ya kujenga hospitali pamoja na vituo vya afya. Naomba nishukuru kwa moyo wa dhati kabisa kwa Serikali kuweza kusaidia Hospitali ya Maweni kwa kupeleka shilingi milioni 500 ili kuendelea kuimarisha hospitali ile ambayo inatumiwa na wananchi wote wa Mkoa wa Kigoma. Ahsante sana, tunaamini pesa hizo zikifika zitaendelea kukarabati hospitali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru Serikali kwa kuweza kukubali kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kakonko. Waziri Mkuu alipokuja alikubali kupeleka shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kakonko na tayari shilingi milioni 500 zimepangwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. Nashukuru kwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya Hospitali ya Kasulu DC, tayari fedha zimeshafika na tayari wameshaanza ujenzi. Nashukuru na ujenzi wa hospitali inayoendelea katika Wilaya ya Buhigwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia wakati huu vituo vya afya vinakarabatiwa na vingine vinajengwa, tunaishukuru sana Serikali. Naomba vituo hivyo vinavyojengwa ambavyo vipo tayari na vingine ambavyo bado viweze kupelekewa madaktari, wauguzi pamoja na vifaa tiba, sambamba na wataalamu wa dawa za usingizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi kwa Waziri wa Afya pamoja na Katibu Mkuu, kwa sababu wao ni akina mama, vipo vituo vingine karibu na hospitali ya wilaya lakini kuna maeneo mengine yapo mbali kabisa. Kwa mfano, kutoka Kasulu Mjini kwenda eneo moja la Kitanga ni kilometa 123 lakini hawana kituo cha afya. Lipo eneo lingine tena linaitwa Kagera Nkanda, kutoka Kasulu Mjini ni kilometa 78. Naomba kwa vile wao ni akina mama washirikiane na Waziri wa TAMISEMI kuona ni namna gani wanaweza kuwasaidia akina mama ambao wanaishi umbali mrefu sana na hawana vituo vya afya ili tuweze kupata vituo vya afya katika maeneo hayo ambayo yako mbali kutoka Wilaya ya Kasulu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile katika Wilaya ya Kakonko, Gwanuku wameshapata kituo cha afya lakini Mgunzu pamoja na eneo moja linaitwa Muhangi na wao wako mpakani hawana vituo vya afya. Naomba na wao waangaliwe kwa sababu wako mpakani waweze kupewa vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nilichotaka kuzungumzia, mara nyingi sana wananchi wanapoenda kutibiwa katika maeneo mbalimbali wakipangiwa kwenda maabara kupima hawezi kurudi bila kuambiwa kwamba hajapatikana na tatizo la UTI. Kila vipimo vinapotoka mgonjwa akipimwa ni lazima ataambiwa kwamba ana tatizo la UTI. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Ndugulile atueleze ni kwa nini wagonjwa walio wengi hasa vijijini na hata mijini hawawezi kutibiwa bila kuambiwa kwamba wana UTI? Ni kwa nini maeneo mengi wanapatikana na matatizo hayo? Nilitaka nijue ni vipimo gani vinavyotoa majibu mengi yanayofanana? Kwa sababu mimi napata wasiwasi isijekuwa kuna maeneo mengine watu wanaambiwa kwamba wana UTI kumbe watu wanafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wazee maeneo mengi wanalalamika kwa kutokupata huduma ya kutibiwa bure. Hiki kimekuwa ni kilio kikubwa cha wazee, maeneo mengi ukienda hata tunapoenda kwenye ziara wazee wengi wanatulalamikia kwamba Serikali ilisema itatoa huduma ya matibabu bure lakini bado huduma hiyo maeneo mengine hawajaweza kutibiwa bure. Yapo maeneo ambayo wanatibiwa bure lakini maeneo mengine bado wazee hawajapa huduma hiyo ya kutibiwa bure. Nafahamu Serikali yangu ni sikivu, itafanya utaratibu ili wazee hawa waweze kupata huduma bure na hasa walete sheria Bungeni ili iweze kufanyiwa utaratibu kusudi itambulike kihalali kabisa kwamba wazee wote sasa wanatakiwa kutibiwa bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba niunge mkono hoja lakini nisisitize hospitali na vituo vya afya vile ambavyo havina waganga na wauguzi wapatiwe wataalam hao ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)